
Watanzania wawili walifariki papo hapo na mmoja kufia hosipitali. Mtu mwingine, raia wa Afrika Kusini, alijeruhiwa vibaya katika shambulio hilo. Mmiliki wa duka la Maisha Tuck, Ashim Nassoro, alisema kuwa aliona kundi la watu wakiwa na bunduki za aina ya AK-47 na pistols wakipiga risasi nje ya duka lake.
Bw. Nassoro alidai waliouawa walikuwa marafiki zake, alisema yeye alikuwa nyumbani na mke wake na mtoto wake, ambapo ni karibu na duka hilo aliposikia milio ya risasi.
Nasroro aliongeza kuwa alikuwa anawajuwa Watanzania hao kwa sababu wote wanatoka Tanzania na wamekuwa wakiishi pamoja tokea walipowasili Cape Town miaka mitano iliyopita. Mtu mwingine aliyeshughudia tukio hilo alisema kuwa waliowauwa Watanzania hao walikuwa hawana wasiwasi na walirudi kwenye gari yao taratibu na kuondoka eneo la tukio.
Kufuatia tukio hilo, polisi ilimkamata Abdus Salaam Ebrahim ambaye ni kiongozi wa kikundi kinachopiga vita dhidi ya uhalifu na madawa ya kulevya nchini humo kinachojulikana kama People Against Gangsterism and Drugs (Pagad). Abdus Salaam Ebrahim amefikishwa mahakami leo kwa mashtaka ya mauaji.
Hata hivyo, mahakama imeyaondoa mashtaka hayo kwa muda kufuatia ombi la mwendesha mashtaka ili kuruhusu uchunguzi zaidi kufanyika. Wakati hakimu akiyandoa mashtaka hayo, wafuasi wa kikundi hicho cha Pagad waliokuwa wamejazana mahakamani hapo walishangilia huku wakisema “Allahu Akbar”. Majina ya Watanzania waliouawa hayakuwekwa kwenye charge sheet.
Pagad ni kikundi kilichoanziswa mwaka 1995 kupambana na uhalifu na madawa ya kulevya kwenye jiji la Cape Town baada baada ya juhudi za serikali kulegalega. Kampeni ya kikundi hiki ilianza mwaka 1996 baada kumkamata, kumpiga na kumchoma moto hadi kufa Rashaad Staggie ambaye alikuwa kiongozi wa kikundi cha uhalifu jijini Cape Town. Serikali ya Afrika Kusini ilishawahi kudai huko nyuma kuwa Pagad ni kikundi cha kigaidi baada ya kudaiwa kulipua kwa bomu hoteli ya Planet Hollywood mwaka 1998. Hata hivyo, Pagad ilipinga kuhusika kwenye shambulio hilo.
Kikundi hiki kilipotea lakini kikaja kuibuka tena kuanzia mwaka 2011 na kampeni yake ya kuchukua mitaa inayotawaliwa na uhalifu na biashara ya madawa ya kulevya. Wadadisi wa mambo wanadai kuwa kurudi tena kwa Pagad kwa gia ya kupambana na uhalifu, hasa madawa ya kulevya, itafanya hali kuwa mbaya hasa kwenye jimbo la Western Cape.
Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la milipuko ya mabomu kwenye sehemu zinazouza magari na pia kwenye nyumba za makazi ya watu zilizopo Athlone na maeneo mengine jijini Cape Town. Matukio haya yamekuwa yakitokea zaidi kwenye nyuma za makazi zinazotuhumiwa kutumika kufanyia biashara ya madawa ya kulevya. Kikundi cha Pagad kimekanusha kujihusisha na matukio hayo.
No comments:
Post a Comment