ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 1, 2013

Mansour Yussuf: Nimekubali kufukuzwa CCM

  Asisitiza Wazanzibari humalizana wenyewe kwa wenyewe
Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid, amesema anakubali matokeo ya kufukuzwa uanachama wa CCM na hafikirii kufungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo.

“Lakini, mimi nitabaki kuwa muumini wa Muungano, ndugu zetu na mimi mwenyewe tunaishi na kufanya biashara Tanzania Bara… tunachohitaji ni muungano wa haki na heshima, kwa bahati mbaya kikulacho kimo nguoni mwako, Wazanzibari humalizana wenyewe kwa wenyewe,” alisema Mansour akijiamini.

Alisema tabia ya Wazanzibari hupenda kubaguana kutokana na asili zao, rangi na uzawa wao zitaendelea kukandamiza na kuwatatiza katika kusimamia madai yao ya msingi na hatma yao.


Tamko hilo amelitoa kwa mara ya kwanza toka atimuliwe kwenye chama, alipozungumza kwenye kongamano la wazi lililoitishwa na kamati inayojiita ya Maridhiano Zanzibar na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wanachama na wafuasi wa CUF visiwani humu.

Mbali na kuweka msimamo huo, alisema hafikirii kugombea uchaguzi mdogo utakaoitishwa kwenye jimbo hilo kupitia chama chochote cha siasa na kueleza kuwa hana ugomvi na CCM.

“Nimeyapokea maamuzi ya NEC ya CCM kwa mikono miwili, nimepewa pole nyingi kutoka kwa wanachama wa chama hicho, nitaendelea kuheshimu uamuzi huo kwa kuwa wamenipima na kuniona sitoshi, hiyo ni haki yao na kutokana na chama chao,” alisema Mansour.

Alisema kama suala la kupata riziki Mungu atamletea wepesi kwa njia nyingine na kusema jambo la kushukuru bado yuko salama na hakuna vitisho, bughudha wala kero anazopata ingawaje hadi wakati huu hajatambua ni kwanini umepitishwa uamuzi huo dhidi yake.

Aidha, alieleza kwamba mustakabali wake na siasa za Muungano haukuwa mzuri tangu alipoanza kuhoji hatua ya Zanzibar kutonufaika na maliasili ya gesi na kuwafananisha viongozi wake sawa na wezi wa mchana.

Mansour alisema wakati akiwa waziri wa nishati alishawahi kutishia kujiuzulu wadhifa huo kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar awamu ya sita, Dk. Amani Karume, baada ya kuelekezwa kwamba Zanzibar inufaike na asilimia 40 ya gesi asilia na Bara 60 lakini pendekezo hilo kutupiliwa mbali.

“Kitendo hicho ndicho kilichonisukuma mimi na Rais Dk. Karume kupeleka maamuzi mbele ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar, dhamira yetu suala la mafuta na gesi asilia liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano,” aliongeza kusema Mansour.

Alisema kwamba suala ya kupinga mfumo wa Muungano wa Serikali mbili limezungumzwa na wanachama wengi wa CCM, akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai na hakuna hatua walizochukuliwa kwa madai ya kukiuka sera hasa katika kipindi hiki cha mjadala wa wazi wa uundwaji wa katiba mpya.

Hata hivyo, alisema kwa wakati huu si muafaka wa kupelekeshwa hasa kwa vijana na kutaka wasikubali kusukumwa na kupangiwa hatma zao kwa ajili ya misimamo ya kisiasa na kivyama na kuweka nyuma maslahi ya nchi.

Alisisitiza kuwa vuguvugu la kudai Zanzibar iwe na mamlaka kamili limefikia hatua kubwa huku akifananisha dagaa wanapoingiliwa na nguru na kusema Wazanzibari wataendelea kuzungumzia madai yao bila ya kuhitaji sauti ya mtu yeyote.

Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Aboubakar Khamis Bakari, alisema rasimu ya mabadiliko ya katiba haifai kwa vile inainyima Zanzibar mambo mengi ya msingi na akasema ni lazima kuwe na uwiano wenye usawa kwa mawaziri na kwa wabunge.

Alisema muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na mataifa mawili yenye sifa sawa za kimamlaka na kutaka mfumo wa jumuiya ya Afrika Mashariki uzingatie katika uwakilishi wa wabunge na mawaziri bila ya kuangalia wingi wa watu katika kila Taifa.

Alisema kuna watu wamejawa na hofu ya kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu, jambo ambalo alisema si kweli kwa vile kila mshirika atabakia kushughulikia maendeleo ya serikali yake na kuchangia Serikali ya Muungano.

“Kuna viongozi wanataka uraisi wa Muungano mmojawapo akiwa Waziri Membe, cha ajabu hatetei maslahi ya Zanzibar, kuna ujumbe toka Muscat amekataa usitoe msaada wa wakfu alipotakiwa kusaini mkataba wa makubaliano, ataweza vipi mtu huyu kuitetea Zanzibar siku moja akiwa Rais?”alihoji Waziri huyo wa Zanzibar.

Katika hatua nyingine mjasiriamali, Eddy Riyami, alitangaza kupitia mkutano huo kimya kimya na kushindwa kusema ameamua kujiunga na chama kipi cha siasa na kusisitiza kuwa ataendelea kutetea maslahi ya Zanzibar katika mfumo wa Muungano.

Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe na mjumbe wa kamati ya maridhiano, Islami Jussa Ladhu alisema kamati imepeleka mapendekezo ya rasimu ya katiba baada ya kumaliza kuchambua na kutoa ushauri wao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: