ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 4, 2013

SABABU ZINAZOWEZA KUMGEUZA MPENZI AKAWA ADUI YAKO-2

NI wiki nyingine tena tunapokutana katika busati letu la mahaba ambapo kama kawaida tunajuzana na kujadili mada mbalimbali zinazohusu uhusiano wa kimapenzi. Wiki iliyopita tulianza kujadili mambo ambayo ukiyafanya katika uhusiano wa kimapenzi, yanaweza kumfanya mtu anayekupenda akageuka na kuwa adui yako.

Tuliona jinsi mazoea ya kumpuuza mwenzi wako na kutomsikiliza yanavyoweza kumbadilisha mtu ambaye awali alikuwa akikupenda kwa moyo wake wote na kukuona kama adui mbaya. Leo tunaendelea kuangalia mambo mengine ambayo usipoyazingatia yanaweza kujenga uhasama kati yako na tulizo la moyo wako.

USIPENDE KUKUMBUSHIA YA ZAMANI
Kuna baadhi ya watu ambao katika uhusiano wao wa maisha, hutumia makosa au udhaifu wa wenzao ambao uliwahi kutokea siku za nyuma kama fimbo ya kuwachapia wenzi wao inapotokea wamekorofishana. Yawezekana umpendaye ana historia mbaya, pengine aliwahi kufanya au kutokewa na jambo fulani kwa kupenda au bila kupenda.
Inapotokea anaamua kukwambia mwenyewe maisha yake ya nyuma, anategemea kwamba utaupokea udhaifu wake na kuukubali. Mathalani mwenzi wako aliwahi kubakwa au aliwahi kuingia kwenye uhusiano na mtu asiye sahihi, akaishia kumtesa na kumuachia majeraha makubwa.
Hiyo isiwe sababu ya kumkumbushia mambo hayo au kumtolea kashfa inapotokea mmekwaruzana. Ukifanya hivyo atakuchukia na taratibu atajitenga mbali nawe.

MSHIRIKISHE KWENYE MIPANGO YA MAISHA
Hakuna kitu ambacho humvuta mwenzi wako karibu kama kumshirikisha umpendaye katika mambo mbalimbali yanayohusu maisha yako. Epuka kuishi kwa udikteta kwamba ukiamua jambo wewe basi hakuna wa kupinga.
Badala yake, jenga mazoea ya kumtaarifu mwenzio kabla au muda mfupi baada ya kufanya jambo fulani. Muombe ushauri, mueleze unachokifikiria na kwa pamoja shirikianeni kupata suluhu za matatizo mbalimbali ya kimaisha.
Kwa kufanya hivyo, utamfanya awe na amani ndani ya moyo wake na kuona kwamba unamjali kutoka ndani ya moyo wako. Atazidisha mapenzi kwako na kamwe hawezi kwenda mbali na wewe lakini ukifanya kinyume chake, utakuwa umemfukuza mwenyewe kutoka kwenye himaya yako.

TENGA MUDA WA KUWA NAYE KARIBU
Bila kujali unafanya kazi gani, una majukumu mengi kiasi gani au una ubize wa hali gani, ni lazima utenge muda maalum ambapo utaachana na kila kitu na kukaa na umpendaye.
Mnaweza kuutumia muda huo kucheza michezo mbalimbali ya kimapenzi, kutembea pamoja sehemu zilizotulia kama ufukweni au kwenye bustani nzuri za miti na maua, kwenda sehemu tofauti na mliyoizoea na kufanya mambo ambayo yataziunganisha hisia zenu.
Hakuna jambo linalorutubisha uhusiano kama kutenga muda maalum wa kuwa na umpendaye na kumfanya ajihisi amani ndani ya nafsi yake. Ukiona shughuli zako ni muhimu zaidi kuliko umpendaye, upo kwenye hatari kubwa ya kumpoteza kwa sababu atakuchukia na mwisho ataenda zake.

ONESHA MSIMAMO, JIAMINI
Kuna baadhi ya watu ambao uhusiano wao wa kimapenzi upo kwenye mashaka muda wote. Unayempenda anapokuwa mbali nawe, haimaanishi anakusaliti kwa kutoka na watu wengine.
Jiamini kwamba alikupenda wewe na ndiyo maana yupo na wewe na inapotokea mwenzio anakuhisi vibaya, muoneshe msimamo wako kwamba kamwe huwezi kurubunika kirahisi.
Ukifanya hivyo, utamfanya mwenzi wako awe na amani moyoni hata unapokuwa mbali. Pia wewe mwenyewe utakuwa na imani naye na utazidisha mapenzi.

GPL

No comments: