ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 14, 2013

AMANI NDIYO MTAJI WETU MKUBWA - JOHN SAMUEL MALECELA

 Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. John Samuel Malecela akisisitiza jambo wakati alipokuwa akibadilishana mawazo na Baadhi ya   maafisa wa  Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  ( hawapo pichani) na  wajumbe wanaohudhuria  mikutano ya Kamati Kuu Sita za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mhe. Malecela ambaye yuko Jijiji New York kwa ziara  binafsi akifuatana na  Mkewe Mhe. Ann Kilango,  alisisitiza sana umuhimu wa watanzania wote bila ya kujali itikadi na tofauti za kisiasa,  kuhakikisha wanaulinda mtaji wao mkubwa   ambao ni amani. 
 Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako  Manongi na  Mkewe  Upendo wakifuatilia mazungumzo hayo ambayo yalifanyika  katika makazi ya Balozi , mazungumzo yaliyoambatana na chakula cha jioni.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa,  Balozi  Celestine Mushy akiwa na maafisa wengine wakimsikiliza  Mhe. Malecele
 Baadhi ya Maafisa kutoka Wizara  ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Bi. Upendo na Bi. Tuusume
 Afisa Mambo ya Nje,  Bi Ramla akiwa na  mmoja wa wajumbe wanaohudhuria mikutano inayoendelea katika Umoja wa Mataifa
 Chakula cha jioni kikiendelea kuliwa

Na Mwandishi Maalum
Waziri Mkuu mstaafu Mhe.  John Samue Malecela  ameeleza kwamba, hakuna mtaji  mkubwa ambao watanzania wanauhitaji kama amani.
 Ameyasema hayo  mwishoni mwa wiki  wakati alipokutana na kubadilishana  mawazo  na  maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  pamoja na wajumbe  wanaohudhuria  mikutano  inayoendelea ya   Kamati Kuu Sita za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mazungumzo hayo yaliyoambatana na  chakula cha jioni yalifanyika  katika Makazi ya Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi
“ Naomba niliseme hili, ninasema hivi ,   hakuna mtaji mkubwa tunaouhitaji watanzania  wote bila ya kujali itikadi  wala tofauti zetu za kisiasa kama  amani” akasema Mhe. Malecela .

Na kuongeza. “Nchi yetu  inaoutajiri usioelezeka, hakuna wilaya isiyokuwa na utajiri kuanzia gesi, madini ya kila aina,  ikiwani  madini ya namna   ya urani hadi  makaa ya mawe, nchi yetu ni tajiri sana. Tunahitaji mitaji ya kuendeleza  utajiri huu. Lakini  nasisitiza sana utajiri huu tulionao hautakuwa na maana yoyote kwetu watanzania kama hatutadumisha amani, upendo,  mshikamano na uzalendo”.
Waziri Mkuu  mstaafu  na ambaye amefuata na  mkewe  Mama Ann Kilango yupo jijini   New York kwa ziara binafsi.
Akasema uchimbaji wa gesi ukianza na uchimbaji wa madini ya urani ukianza, pamoja na mipango mbalimbali ya maendeleo inayoendelea hivi sasa,  basi miaka kumi ijayo Tanzania itapiga hatua kubwa sana  za  kiuchumi na kimaendeleo.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Malecela  licha ya kuzungumzia umuhimu wa amani  na matumizi mazuri ya raslimali , pia alizungumzia  mafanikio na changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa hivi sasa.
Kwa upande wa maendeleo  hakusita kuzungumzia mpango wa serikali wa kuwa na shule za   sekondari kila kata na kusisitiza kwamba ingawa uamuzi huo umekuwa ukipingwa au kulalamikiwa na baadhi ya watu lakini ni mpango ambazo umewapatia fursa vijana wengi ya kupata  elimu ya sekondari na matunda  yake yanaonekana.
Kwa upande wa ujenzi wa miundo mbinu na hususani barabara,  Mhe.  John Malecela, amesema Serikali ya Mhe. Rais  Jakaya Mrisho Kikwete inafanya kazi kubwa na nzuri ya  kuendeleza ujenzi wa mitandao ya barabara nchi nzima.
“ Kusema ukweli, Mhe. Kikwete anajitahidi sana katika eneo hili hakuna nchi katika eneo la Afrika  Mashariki ambayo  inaweza kushindana nasi kwa upande wa barabara.” Akasema  Mhe.  Malecela
Na kuongeza  serikali haijaishia katika ujenzi wa barabara lakini pia inaendelea na jukumu  uimarishaji wa reli,ujenzi na upanuzi wa bandari  ukiwamo  ujenzi wa  bandari mpya katika eneo la Bagamoyo. Bandari aliyoieleza kwamba  itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuegesha meli  kubwa na zenye uwezo wa kubeba tani nyingi za mizigo.
Akizungumzia uzefu wake katika  tasnia ya  diplomasia na ushirikiano wa  Kimataifa.  Mhe, John Malecela ambaye pia ni mwanadiplomasia mkomavu aliwataka  maafisa hao kutoyumba pale inapobidi kutetea misimamo na  maslahi ya nchi yao.
“ kwa kweli  ninawaonea huruma sana Mabalozi wa wakati huu, mnafanya kazi katika mazingira magumu sana, enzi zetu nakumbuka nikiwa  hapa Umoja wa Mataifa  miaka michache baada ya kupata uhuru Balozi ulikuwa na nguvu ya kusimama kwenye  majukwaa ya kimataifa na kutetea jambo bila ya kuwaogopa wakubwa”. Akasema.
Na kuongeza, “ Kuna mkutano mmoja  nilitoa maneno makali dhidi ya  Balozi wa Israel wakati ule.  Baada ya  mkutano ule, Balozi yule alikuja ofisini kwangu na kuniambia   maneno yale niliyoyasema hayakuwa  msimamo wa nchi yangu”.

“ Lakini pia  niliitwa nyumbani  na Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere. akaniambia John umezungumza nini huko, taratibu  hao ni wakubwa na mimi nikamjibu,  Mhe. Rais naamini nimekuwakilisha vizuri.  Ninachotaka kusisitiza  ni kwamba  msiogope kutetea maslahi ya nchi yetu licha ya changamoto za diplomasia za  nyakati hizi”.  Akasisitiza

1 comment:

Anonymous said...

Amani ni zao la matumaini, pindi matumaini yatakapotoweka kutakuwa na vurugu katika jamii.