ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 1, 2013

Barua ya wazi kwa Wapendwa Watanzania wenzangu

Na Mwandishi wetu
Kwanza nianze kwa kuwapa pole jirani zetu na ndugu zetu wakenya kwa tukio baya kabisa la ujasusi lilotokea mwisho wa juma lilopita. Ni jambo ya kusikitisha na lenye kujaa na maswali mwengi ya kujiuliza. Imefika mahali kuna watu hawathamini utu wala maisha ya binadamu mwenzake. Poleni sana ndugu zetu na tuko pamoja.
Mambo ya kujifunza:
1.     Mwenzako akinyolewa, na wewe anza kutia maji. Ninasema hivi kwasababu tusidhani kwasababu tupo mbali na Al-Shabab basi tuko salama. La hasha, hawa jamaa hawalali, na chokochoko  na dalili tulianza kuziona mapema kabisa. Tumeona  matukio ya mabomu na tindikali. Inatisha kabisa. Nashauri vyombo vya usalama vifunguke macho na viache kufanya mambo kwa mazoea, tubadilike na tujifunze mbinu mpya za kukabiliana na ugaidi. Tusione aibu kuomba msaada wa kitaalamu na vifaa kutoka kwa wenzetu waliotutangulia kiitelijinsia

2.     Somo la uzalendo ndiyo mahali pake hapa. Mtu mzalendo hawezi kuiuza nchi yake kwa ajili ya njaa zake. Kutokana na umbwe la umasikini kuongezeka, inakuwa rahisi sana mtu kukubali kushirikiana na watu wenye nia mbaya kuumiza nchi yetu. Hizo ni tamaa na badala ya kutatua matatizo inazidisha kwasababu:
a.     Utalii utakufa
b.     Wawekezaji wataogopa kuja kuwekeza
c.      Hata vile vichache tulivyo navyo vitahujumiwa
d.     Uhai wa kila mmoja wetu utawekwa rehani pamoja na aliyechonga line naye hatokuwa salama
e.     Kisiwa cha amani kitatoweka (Mungu atupitishie mbali)
f.       Tutaanza kunyoosheana vidole kati ya kabila na kabila, dini na dini, bara na visiwani. Hatutakuwa wamoja. Lazima tutaanza kutafuta mchawi
g.     Hata wenye mali hawataishi kwa amani,maana wao ndiyo watakaoviziwa kwanza; kama tulivyoona Westgate
Nini cha kufanya:
Nakumbuka enzi za Mwalimu kulikuwa na mabalozi wa nyumba kumikumi. Hawa watu walikuwa na nguvu sana kwenye eneo lao. Japo ilikuwa sera ya CCM,lakini kutokana na vyama vingi, basi tuifanye sera ya Taifa. Nakumbuka wakati wa utoto wetu ukipata mgeni lazima utoe taarifa kwa mjumbe wa nyumba kumi. Hii ilisaidia vitu vifuatavyo:
a.     Kujua mgeni ni nani, anakaa muda gani na anashughuli gani. Ikitokea uhalifu, basi inakuwa rahisi kupata pa kuanzia. Najua wengi mtasema mambo ya ujamaa, lakini tukumbuke ujamaa ndiyo unaofanya tunajiona wamoja. Yes, kuna mambo ambayo hayakwenda vizuri,lakini utu na undugu viliimarika. Ukiangalia jirani zetu ambao walifuata ubepari waligombana na kuuana, sisi tu ndiyo tulishikamana. Kuanzia  nyumba kumi, kata, tarafa, wilaya, mkoa hata taifa tulijivunia mshikamano na kila mtu alikaataa kurubiniwa kusaliti nchi yetu
b.     Pia ilisaidia mambo ya sensa. Balozi wa nyumba kumi alijua idadi ya watu wake hata mtoto akizaliwa leo. Kipindi cha sensa, walichokuwa wanafanya ni kuhakiki idadi, hata kama mmoja ameenda likizo au amesafiri mjumbe anajua mtu wake hayupo.
c.      Maswala ya sera za taifa kama elimu afya na uzazi wa mpango viliwezekana kutoka na ushirikiano na mabalozi wa nyumba kumi.
d.     Mwanzoni balozi alikuwa anajitolea, lakini kutokana na sababu za kiusalama, basi serikali iwape hata kifuta jasho, na baadae waingie kwenye maswala ya usalama wa raia.
e.     Tukishawawezesha hawa, basi kila mgeni anayeingia kwenye eneo lake lazima ajue au ajulishwe, la sivyo uhalifu ukitokea eneo lake yeye ndiye atakuwa wa kwanza kuhojiwa.
Mwisho nimalizie kwa kusema, kwa yaliyotokea kwa jirani zetu tusidhani sisi tuko salama. Hii kwetu ni nafasi nzuri ya kujiweka mguu sawa. Ulinzi mipakani iimarishwe, tuache kuweka siasa kwenye vitu vinavyohatarisha usalama wa Taifa letu teule. Porojo za mabomu ya Arusha, Zanzibar, Tindikali nk vizifanyiwe masihara hata kidogo. Wananchi wapewe taarifa ya kila jambo na watu wawajibike au wawajibishwe wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.

2 comments:

Anonymous said...

imenichafua habari hii yani katika dunia ya leo unadhani watanzania wako wachovu hivi hawafanyi research kujua lililotokea na wengine wapo serikalini wanajua mengi acheni hizo mungu alivyoshasema kwamba kwenye ukweli uongo unajitega so tusobiri uongo ya majanga haya kwani tuko mbali hata miaka kumi mitano tukiwa hai mtakuja juu ukweli wa mambo watanzania msipate pressure kuweni wenye akili za kufikira sio kila siku wafikiriwa

Anonymous said...

Mdau Asante sana kwa kuliona hilo, huo ndio ukweli mtupu. Tunaelewa serikali pamoja na vyombo husika havijakaa kimya vinakuwa makini, basi tuungane pamoja nao wananchi ukimhisi mtu mtolee taarifa. Kuna watu wako mahotelini kwa muda mrefu tu hawajaulikani wanafanya nini na wanalipa kila siku! Pili watu wanaoingia nchini wafahamike. Mnakumbuka Dodoma kulikuwa na shule ya sekondari iliyoanzishwa na mgeni hadi kufikia kidato cha pili ndio anajulikana baada ya kuwepo tatizo. Je alipatiwaje vibali kama sio kwa nguvu za mmoja au wawili kwenye ngazi husika!! Watanzania tuilinde nchi na wananchi wake.