ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 8, 2013

BIBI TITI ALIVYOMWAGA FEDHA KUMUUA NYERERE


Bibi Titi Mohamed.
JUMAMOSI Agosti 1, 1970 Mahakama Kuu ya Tanzania iliambiwa na mkurugenzi wa mashitaka jinsi Bibi Titi Mohamed alivyogharamia mapinduzi ya kumuua Julius Nyerere na kuiangusha serikali yake.
Mahakama iliambiwa kuwa Bibi Titi katika siku isiyojulikana aliitisha mkutano na katika kikao hicho, Michael Kamaliza alimshauri mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Leballo aende London kwa Oscar Kambona kumwomba atume fedha zaidi ili kufanikisha mpango wao wa mapinduzi.
Kamaliza alimtaka Chipaka amwandikie barua Kambona na kumtumia noti ya shilingi 10/- ili Kambona aitie saini ije isaidie katika kuwashawishi wabunge na baadhi ya mawaziri kumuunga mkono Kambona.
Noti hiyo pia ilikuwa isaidie katika kuchangisha fedha za mapinduzi na kuwashawishi watumishi wa TANU na NUTA kuipinga serikali.
Mkurugenzi wa mashitaka alisema; “Kamaliza alimwambia Leballo kuwa hakukuwa na shaka wafanyakazi wa Tanzania wangeliunga mkono mpango wa mapinduzi kwa sababu Rais alikuwa amemwondoa (Kamaliza) kutoka NUTA kinyume cha matakwa ya wafanyakazi.
“Leballo alikutana na Bibi Titi nyumbani kwake tarehe Juni 23 na mama huyo alimweleza alikuwa amekwenda Nairobi kwa muda wa siku nne na kwamba alimpigia simu Kambona kutoka Nairobi na kumtaka atume shilingi milioni moja (1,000,000/-) kwa ajili ya mapinduzi katika muda wa wiki mbili.
“Titi akampa Leballo shilingi 400/- na kusema kwamba alikuwa amepokea shilingi 2,000/- kutoka kwa Kambona, 1,000/- za Chacha kwa matumizi madogo madogo. Titi alimwambia Leballo atampa shilingi 600/- baada ya siku chache na alifanya vile tarehe 26, Juni”. Fedha hizo zilitolewa mahakamani kama ushahidi kamili.
“Tarehe 28 Juni, Chacha alipanga kukutana na Leballo tarehe 30 Juni ili amjulishe Leballo kwa Meja Herman.
“Chacha na Luteni Kanali Marwa walikwenda nyumbani kwa Leballo tarehe 30 Juni saa 3 usiku. Chacha na Leballo walikwenda katika chumba cha kulala na kumwacha Luteni Kanali Marwa sebuleni.
“Huko chumbani Chacha alimwambia Leballo kwamba alikuwa tayari kuipindua serikali kama angelipwa shilingi 20,000,000 na akamtaka Leballo amwambie Kambona atume fedha hizo kwa haraka.
“Leballo na Chacha walikutana tena tarehe 3 Julai huko makao makuu ya Jeshi kwa maombi ya Chacha. Chacha alimwambia Leballo kwamba alikuwa amesikitishwa na ukawiaji wa fedha.
Akamtaka Leballo aende huko Lugalo barracks katika bwalo la maafisa ambapo Kapteni Lifa Chipaka atamtambulisha kwa Meja Herman.
“Leballo alikwenda kule, akamkuta Kapteni Lifa anamsubiri. Kapteni Lifa alimwambia Leballo kwamba hakuwa anamwamini Meja Herman katika mpango wa mapinduzi kwa sababu alikuwa chotara kutoka Iringa na kwamba yeye angempa orodha ya maofisa ikiwa pamoja na jina la mtu mmoja kutoka kisiwani. Kutoka kwenye orodha hiyo mtu wa kuongoza mapinduzi angechaguliwa. Baadaye Kapteni Lifa alimfahamisha Leballo kwa Meja Herman.
“Baada ya mkutano huo Leballo alionana na John Chipaka na Kamaliza wakiwa pamoja katika ofisi ya shirika la wafanyakazi la NUTA. Wote walizungumza na kumtaka Leballo aende London kwa Kambona kumtaka atume fedha zaidi.
“Kama saa kumi na robo alasiri siku hiyo Leballo aliitwa tena kwenye ofisi hiyo. Aliwenda na kumkuta Kamaliza peke yake. Kamaliza alimwambia kwamba alikuwa amemtuma mtu mmoja kwa Kambona “U That” akalete fedha.
“Kamaliza akamwambia Leballo kwamba yeye alipendelea Meja Herman aongoze mapinduzi kuliko Chacha”.
Washitakiwa saba ambao wamekana mashitaka matatu ya uhaini na moja kuficha siri ya uhaini ni Gray Likungu Mattaka, John Dustan Lifa Chipaka, Bibi Titi Mohammed, Michael Marshal Mowbrya, William Makori Chacha na Alfred Philip Millinga.

GPL

No comments: