ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 8, 2013

KUNA NYAKATI MTAGOMBANA, MTANUNIANA, HIVYO HAIONDOI UKWELI KUWA MNAPENDANA-5

TUKIWA kwenye kipengele cha kisasi kama moja ya vitu ambavyo unapaswa kujiepusha navyo, nilisema kuwa hiki ni kitu kingine ambacho unatakiwa kukipiga vita kila siku kama kweli unataka uhusiano wako udumu. Mwenzi wako amekukosea sawa lakini wewe utaharibu zaidi ikiwa utaamua kumlipizia. Hebu jikite katika kusahihisha tofauti zenu na kweli ziishe.
Ikiwa unataka uhusiano wako uendelee mbele, vilevile uwe wenye afya bora kila siku, hakikisha unaachana na mambo ya kisasi. Amekukosea, umemsamehe baada ya hapo maisha yaendelee mbele. Acha chuki zisizokwisha, vinginevyo mapenzi yatakushinda.
Unapomlipizia kisasi unakuwa unahamisha kosa moja kwa moja kutoka kwake hadi kwako. Wengi waliothubutu kufanya hivyo uhusiano wao ulivunjika. Kisasi ni mpango wa Shetani. Hebu mkemee maana huko anapokuongoza sipo panapotakiwa. Anakupoteza.
Yupo mtu ambaye alimfumania mwenzi wake, kweli palichimbika. Baada ya siku kadhaa waliketi na kumaliza tofauti zao. Miezi miwili baadaye aliyefumania naye akatoka na mtu mwingine kisha akafanya juu chini ili mwenzi wake aone. Matokeo yakawa mabaya kupita kiasi.
Kwanza unajidhalilisha, inakuwaje uende ukatembee na mtu mwingine ili kumkomoa mwenzi wako? Je, kama uliona hujamsamehe ni kwa nini usikatae msamaha wake? Kwa wenye akili timamu kila wanaposikia stori ya kisasi, yule aliyelipiza ndiye huonekana hamnazo.
Tambua kwamba katika kisasi unakuwa hulipizi bali nawe ni mtenda. Maisha ya jino kwa jino hayafai, unatakiwa kuwa mtu mwenye kusamehe na kuondoa kifundo. Achana na viapo visivyo na maana, kwani mara nyingi ndivyo husababisha uamue kulipiza kisasi.
Anapokutendea kosa na pale anapokuja kukuomba msamaha kitu cha kufanya kupima upendo wako kwake, je, anakupenda? Kama jawabu ni chanya halafu nawe ukaridhika naye kutoka moyoni, basi jambo la kufanya ni kumsamehe na usibaki na kitu chochote moyoni mwako.
Kulipiza kisasi maana yake humpendi, hapo inakuwa hakuna upendo. Na kama mtaendelea na uhusiano itakuwa sawa na kumvalisha bata viatu. Hamuwezi kufika mbali. Mapenzi yanajengwa na watu wawili wanaopendana, wenye dhamira ya kuishi kwa kuvumiliana.
Umewahi kuona wapi watu wanaopendana wakawa wanawekeana visasi vya kuumizana? Angalia jinsi mnavyopendana, hiyo ndiyo iwe nguzo ya maisha yenu. Amekukosea, muweke chini na umuelekeze madhara ya kile alichokifanya na uone kama kweli anajutia alichokifanya.
Sasa kama anajutia visasi vya nini? Ikiwa unaona bado yupo waluwalu endelea kumfundisha mpaka atakapokaa sawa. Imani kubwa kwangu ni kwamba inawezekana kakufanyia kosa kubwa lakini nyote mkawa mnapendana. Hiyo ni kweli, taswira ya aina hii imepitia kwenye uhusiano wa watu wengi.
Siku zote tambua kwamba kuna watu wazuri sana walionesha uzuri wao baada ya kukosea. Hivyo basi, ni kweli amepotoka na amekuumiza sana, lakini mpe nafasi ya kuonesha masahihisho yake. Jibu la maisha yenu ni kusahihishana na kutazama mbele kwa matumaini katika nyakati zijazo.
Muhimu kuzingatia ni kwamba mapenzi ni sanaa ya peke yake. Hayahitaji busara ya hali ya juu kuweza kuyatendea haki. Kuna watu ambao Mungu amewatunuku maarifa na hekima sana lakini yanawashinda. Kuna kitu kidogo mno ambacho kila mtu akikitumia, kitamsaidia sana.
Uhusiano wa kimapenzi unahusisha moyo. Kila siku ongea nao, jadiliana nao, uulize maswali mengi kadiri unavyoweza kisha ukupe majibu kuhusu nini unataka. Weka pembeni tamaa, ongea naye akwambie hitaji lake halisi kabisa halafu fanyia kazi hilo linalohitajika.
Wewe upo radhi kumshikilia mwenzi wako ambaye moyo wako unakuamrisha usimwache lakini yeye hasikii. Kama ndivyo, basi hutakiwi kuinua mikono. Tuliza kichwa kidogo, isome akili yake, ikiwezekana ingia ndani ya ubongo wake. Jitahidi ugundue nini anawaza kuhusu mapenzi.
Usiishie hapo, jibiidishe kutambua kile ambacho kinamnyima usingizi kuhusu wewe. Je, unakosea? Basi fanya marekebisho haraka.

Itaendelea wiki ijayo

GPL

No comments: