
FURAHA ya ndoa ni pamoja na tendo la ndoa. Kwa hakika ni tendo ambalo linahitajikupewa nafasi na kufanywa kwa ukamilifu wake. Kusuasua, kulipua, kujifikiria mwenyewe au kushindwa kabisa ni tatizo.
Rafiki zangu nilianza wiki iliyopita kuelezea mambo ya msingi ya kuzingatia ili tendo hilo liwe lenye ubora na ladha ya kipekee. Ni fahari wanandoa wanapotoshelezana wao kwa wao ipasavyo.
Kama kawaida, lugha inayotumika hapa ni ya kirafiki kabisa kwa lengo la kufikisha ujumbe bila kuchafua hali ya hewa!
Wiki jana niliishia katika kipengele cha nguvu mbadala ambapo nilisema kwamba, wapo baadhi ya watu hujidanganya kwa kujiingiza katika matumizi ya vilevi na dawa za kuongeza nguvu wakiwa na imani kuwa watakuwa bora katika eneo hilo – siyo kweli.
Sylvester Nicholaus, Mtaalamu wa Saikolojia ya Uhusiano wa Uingereza anafafanua katika moja ya makala zake mtandaoni: “Wakati mwingine unaweza kutumia dawa halafu zikazidi hali ambayo inaweza kuongeza maumbile ya mwanaume na hivyo ‘kumkimbiza’ mke nyumbani, hizi dawa siyo nzuri kwa jumla.”
Anaendelea: “Mfano mzuri ni dawa za kuongeza matiti, makalio na hips, tunaona madhara yake. Sasa kwa nini hizi za kuogeza nguvu? Lazima zitakuwa na matatizo.”
ACHA PAPARA
Hutakiwi kabisa kuwa na papara na tendo lenyewe, acha haraka. Tulia, lakini wakati huohuo ukihakikisha kwamba, huna mawazo na wala huna mashaka na uwezo wako. Amini kwamba unaweza kumfurahisha mwenzi wako na wewe pia utafurahia tendo hilo.
Ukiwa na papara, katu huwezi kufurahia tendo la ndoa, kwani utakuwa unawaza kujifurahisha mwenyewe, jambo ambalo siyo zuri. Kabla ya kuanza kufanya chochote, ni vyema mkafanya maandalizi kwanza.
Maandalizi humfanya mwenye shauku ya kutaka kujua atakachokipata kutoka kwako. Fanya mambo yako taratibu, ukihakikisha ndoa yako inakuwa salama na mwenzi wako akiwa hafikirii kabisa kukusaliti!
LUGHA LAINI
Kumbuka kwamba wewe na mwenzi wako mpo kwenye uwanja mwanana, uwanja wa mahaba na siyo uwanja wa ngumi! Kama ndivyo basi, hata lugha ambayo itatakiwa kutumika katika uwanja huo, lazima iendane na mazingira. Hivyo basi, ni lazima lugha tamu na laini itumike.
Epuka kabisa kutumia maneno makali au kuamrisha, kukumbusha ugomvi uliopita na mambo mengine kama hayo. Kuwa mstaarabu, tumia lugha nyepesi yenye bashasha, ambayo itamfurahisha mpenzi wako.
IBUKA MSHINDI
Kwa kufuata taratibu hizo hapo juu, hakika utafurahia tendo na ndoa na mwenzi wako hatafikiria kukusaliti au kuwa na mpenzi mwingine nje ya ndoa.
Kumbuka tendo la ndoa ndiyo msingi wa ndoa yenyewe hivyo kushindwa kwako kutimiza wajibu wako ni sawa na kumwambia mpenzi wako afanye maarifa ya kupata pumziko lingine nje ya ndoa yenu.
Upo tayari kuona jambo hilo likitokea? Bila shaka hakuna hata mmoja ambaye anaweza kujibu ndiyo...hili ni jambo la hatari sana katika maisha ya ndoa.
Fuata misingi hiyo makini na kwa hakika utafurahia sana kuingia ndani ya ndoa yako. Kuna kitu umejifunza?
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment