ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 1, 2013

Janga la jengo la Westgate

Harakati za jeshi la Kenya kulikomboa jengo la Westgate

Ilikuwa hotuba iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu kuu na wakenya pamoja na nchi zingine duniani ambao raia wake walinaswa katika shambulizi la kigaidi katika jumba la Westgate mjini Nairobi.
Katika hotuba yake kupitia televisheni Jumanne, Rais Kenyatta alisema "operesheni imefika kikomo. ''
Hotuba hiyo bila shaka iliwatuliza watu kote nchini, katika nchi ambayo ilitikiswa vibaya sana na shambulizi ambalo kwa kweli halikutarajiwa, dhidi ya jengo la maduka la Westgate na ambalo hutembelewa na watu wa tabaka mbali mbali , wanadiplomasia na hata wakenya wenyewe pamoja na watalii.
Familia kote nchini na katika sehemu zingine duniani , mfano Australia, Canada, China, Ufaransa, Ghana, India na Uholanzi , Peru, Afrika Kusini, Korea Kusini, na Uingereza pamoja na Marekani, walisubiri kwa zaidi ya siku tatu kufahamu ni lini wanajeshi wangeweza kumaliza mapambano dhidi ya magaidi hao.
Wengi pia walisubiri kwa hamu na gamu kujua hali ya wapendwa wao waliokuwa wamenaswa katika jengo hilo
Hakuna hata mtu mmoja alithubutu kupuuza ukubwa wa shambulizi hilo, hasa kwa kuwa shambulizi lenyewe lilifanywa na kundi la magaidi waliokuwa wamejihami vikali na kutotaka kushauriana na magaidi hao ambao lengo lao lilikuwa kuwaua watu wengi iwezekanavyo.
Maswali mengi kuliko majibu

Licha ya watu hatimaye kupumua kufuatia taarifa kuwa mashambulizi yalikuwa yamekwisha, hotuba ya Rais ilizua maswali mengi kuliko majibu.

Hadi leo haijulikani idadi kamili ya watu waliokuwa wameshikwa mateka, idadi ya waliofariki na idadi ya wale wasiojulikana waliko.

Lakini matumaini ya hata kumpata mtu yeyoye aliye hai kwa sasa hayapo hasa baada ya Rais kusema kuwa baadhi ya ghorofa za jengo hilo ziliporomoka.
Sehemu ya jengo la Westgate lilivyoporomoka

"mwishoni mwa opereshemi, ghorofa tatu za jumba la Westgate ziliporomoka, na bado kuna miili iliyonaswa chini ya vifusi, ikiwemo miili ya magaidi,'' alisema Rais Kenyatta kwenye hotuba yake.

Hakuna maelezo kuhusu kilichosababisha kuporomoka kwa ghorofa hizo. Je ziliporomoka kufutia mlipuko wa bomu? Na je ilisababishwa na bomu? Na je nani alisababisha mlipuko huo, ilikuwa magaidi au jeshi la Kenya?
Ndio maswali yaliyoulizwa laikini hakuna majibu.

Mnamo Jumatatu, siku ya tatu ya shambulizi, kulikuwa na makabiliano makali ya risasi , milipuko na moto ulioambatana na moshi mkubwa uliokuwa unafuka kutoka kwa jengo hilo kwa zaidi ya saa tano.

Kwa mujibu wa waziri wa usalama, Joseph Ole Lenku, washambuliaji waliwasha moto na kuchoma magodoro na vifaa vingine ili kutatiza shughuli za jeshi kuwakabili.

Mnamo siku ya Jumatatu katika kilie kilichoonekana kuwa shughuli ya mwisho ya operesheni ya jeshi, waziri alisema kuwa mateka waliokolewa.

Lakini baada ya kumsikiza Rais aliyetangaza kukamilika kwa operesheni hiyo, ilikuwa wazi kuwa mateke bado walikuwa wamenaswa katika jengo hilo na wengi walifariki.
Je kulikuwa na washambuliaji wanawake?

Magaidi walikuwa wamejihami vikali tayari kukufa . Serikali awali ilisema kuwa idadi yao ilikuwa kati ya 10-15 ndani ya jengo hilo. Rais alithibitisha kuwa magaidi watano kati yao walikuwa wamefariki wakati wa operesheni ya jeshi.

Pia kulikuwa na ripoti kuwa washukiwa kadhaa walikamatwa walipokuwa wanajaribu kutoroka.
Picha ya magaidi walioshambulia Kenya.Je kulikuwemo wanawake?

Miongoni mwa magaidi hao, kumekuwa na tashwishi kuwa alikuwa mwanamke aliyeongoza mashambulizi hayo.

Wakati mkuu wa majeshi Generali Julius Karangi, akiambia waandishi wa habari kuwa uraia wa washambuliaji unajulikana, bado kulikuwa na dalili ya mchanganyiko katika taarifa za serikali.

Katika taarifa yake Rais Kenyatta alisema kuwa wanawake walikuwa miongoni mwa magaidi

Hata hivyo siku iliyofuata taarifa ya waziri wa usalama ilisema kuwa hapakuwa na mwanamke miongoni mwa magaidi hao, alisema wote walikuwa wanaume lakini baadhi walikuwa wamevalia nguo za kike kujidai kuwa ni wanawake.

Ikiwa Bwana Karangi anasema kuwa uraia wa washambuliaji unajulikana , inakuwaje kwamba kuna taarifa zisizooana kuhusu tukio hilo lote? na kama magaidi waliuawa wengi wanahoji wapi ishara ya kuthibitsha hilo? hata kama ni picha ya nyuso zao?

No comments: