ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 15, 2013

KUNA NYAKATI MTAGOMBANA, MTANUNIANA, HIVYO HAIONDOI UKWELI KUWA MNAPENDANA - 6

Katika kipengele cha mwisho wiki iliyopita, nilieleza kuhusu kisasi. Nilifafanua kwamba wanaopendana haitakiwi kulipiziana visasi, maana athari yake ni kubwa zaidi. Aliyeanza huonekana anaonewa baada ya kulipiziwa.

Kulipiza kisasi maana yake humpendi, hapo inakuwa hakuna upendo. Na kama mtaendelea na uhusiano itakuwa sawa na kumvalisha bata viatu. Hamuwezi kufika mbali. Mapenzi yanajengwa na watu wawili wanaopendana, wenye dhamira ya kuishi kwa kuvumiliana.
Umewahi kuona wapi watu wanaopendana wakawa wanawekeana visasi vya kuumizana? Angalia jinsi mnavyopendana, hiyo ndiyo iwe nguzo ya maisha yenu. Amekukosea, muweke chini na umuelekeze madhara ya kile alichokifanya na uone kama kweli anajutia alichokifanya.
Sasa kama anajutia visasi vya nini? Ikiwa unaona bado yupo waluwalu endelea kumfundisha mpaka atakapokaa sawa. Imani kubwa kwangu ni kwamba inawezekana kakufanyia kosa kubwa lakini nyote mkawa mnapendana. Hiyo ni kweli, taswira ya aina hii imepitia kwenye uhusiano wa watu wengi.
Siku zote tambua kwamba kuna watu wazuri sana walionesha uzuri wao baada ya kukosea. Hivyo basi, ni kweli amepotoka na amekuumiza sana, lakini mpe nafasi ya kuonesha masahihisho yake. Jibu la maisha yenu ni kusahihishana na kutazama mbele kwa matumaini katika nyakati zijazo.

YAPI UNAPASWA KUYAZINGATIA
Umeshaona mambo ambayo kwa hakika unatakiwa ujiepushe nayo ili kuufanya upedo wenu uzidi kushika hatamu, vilevile kuna mambo ambayo ndiyo hasa unatakiwa kuyaweka mbele. Ni haya yafuatayo;

UPENDO
Kama utaongozwa na upendo kila siku utaona maisha ya uhusiano yalivyo mepesi. Mwenzi wako atakuudhi, ila hasira zako hazitafikia kiwango kibaya kama utaongozwa na mapenzi uliyonayo kwake. Hutamfikiria mambo mabaya kwa sababu unampenda.
Kama upendo wako ni wa wasiwasi, matokeo ndiyo yale. Amekuudhi kidogo hutaki kumsamehe, zaidi unakuwa unawaza tu kuachana. Mapenzi hayataki hivyo, muweke moyoni kwanza, halafu akikosea mwadhibu kama mwandani wako.
Kuna faida nyingi kutokana na wazo hili, kwamba mmekoseana, pengine wewe ndiye mwenye makosa. Hutaendekeza kiburi chako na matokeo yake utafanya juu chini kumuomba msamaha mpaka hali ya amani irejee katikati yenu.
Wanaopendana huwa hawakai wamenuniana kwa kipindi kirefu. Ni kweli kwamba maudhi hayakwepeki, yaani itatokea mmetofautiana lakini tofauti hizo zitakwisha ndani ya muda mfupi kwa sababu upendo ndani yenu utawalazimisha hivyo.
Nikuombe ndugu yangu uwekeze upendo wako kwake mpaka ukolee. Hakikisha naye anakupenda kwa kiwango unachostahili. Kama hatua hii ya mwanzo utaifanikisha, mengine yanayokuja yatakuwa mepesi. Hakuna dhoruba inayoweza kuwatenganisha ikiwa mnapendana. Labda kifo kwa sababu hiyo ni amri ya Mungu ambaye hashindwi na chochote.

UVUMILIVU
Mvumilie mwenzi wako kwa kila jambo. Jenga uhusiano wako katika misingi inayokubalika ili naye awe mvumilivu. Maisha yenu yanaweza kuwa murua sana kama nyote mtaishi kwa kuvumiliana kwa kila jambo. Hiki ni kipengele nyeti sana.
Usijiulize kwa nini wale waliachana, jibu ni moja tu kwamba walikosa uvumilivu. Wewe usiwe katika mkondo huo, kwani nanyi mkishindwa kuvumiliana, mtanyooshewa vidole kwamba mliachana kwa sababu hamkuweza kuvumiliana mlipopaswa kufanya hivyo.
Uvumilivu haufanyi kazi wenyewe, isipokuwa huhitaji kujiuliza na kujisahihisha mara kwa mara. Kuna sauti itakwambia utengane na mwenzi wako lakini wewe jiulize: “Je, nikiachana naye leo nitakuwa mvumilivu?” Bila shaka jawabu litakuwa kwamba utakosa sifa hiyo.

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: