ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 22, 2013

KUNA NYAKATI MTAGOMBANA, MTANUNIANA, HIVYO HAIONDOI UKWELI KUWA MNAPENDANA-7

Mantiki ya mada hii ni kwamba siyo mmegombana leo ndiyo mkachukua uamuzi wa kuachana ni vizuri kutambua kwamba zipo nyakati za misuguano lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba mnapendana. Nilishaeleza kuhusu mambo matano ya kujiepusha nayo.

Vilevile nikahamia kwenye mambo matano ya kuzingatia ili kukuwezesha kuvuka changamoto ambazo zitakukabili kwenye uhusiano wako. Wiki iliyopita nilikomea pale ambapo nilikuwa naanza kueleza umuhimu wa uvumilivu. Bila kuvumiliana, hakika hutaweza kuishi na mwenzio.

Mvumilie mwenzi wako kwa kila jambo. Jenga uhusiano wako katika misingi inayokubalika ili naye awe mvumilivu. Maisha yenu yanaweza kuwa murua sana kama nyote mtaishi kwa kuvumiliana kwa kila jambo. Hiki ni kipengele nyeti sana.

Usijiulize kwa nini wale waliachana, jibu ni moja tu kwamba walikosa uvumilivu. Wewe usiwe katika mkondo huo, kwani nanyi mkishindwa kuvumiliana, mtanyooshewa vidole kwamba mliachana kwa sababu hamkuweza kuvumiliana pale ilipohitajika.

Uvumilivu haufanyi kazi wenyewe, isipokuwa huhitaji kujiuliza na kujisahihisha mara kwa mara. Kuna sauti itakwambia utengane na mwenzi wako lakini wewe jiulize: “Je, nikiachana naye leo nitakuwa mvumilivu?” Bila shaka jawabu litakwambia utakosa sifa hiyo.

Utakapojigundua wewe siyo mvumilivu, maana yake itakupasa ufanye kazi mbili nzuri na za ziada. Mosi; kuujenga uvumilivu ndani yako, maana maisha ya uhusiano hayawezi kwenda bila kuwa na kawaida ya kupiga moyo konde kisha kutazama mbele kwa matumaini.

Pili; wekeza uvumilivu ndani ya moyo wa mwenzi wako. Ukifeli hili hamtadumu, atakuacha mapema sana. Ukifanikiwa katika pointi hii kwa asilimia 100, unaweza kushangaa unamuudhi jambo kubwa lakini badala ya kukugombeza, anakuuliza kwa upole nawe unamuomba msamaha yanaisha.

Yanaitwa mapenzi, kwa sababu ni neno baada ya kupendana. Yana uzuri mkubwa sana pale yanapodumu. Asikwambie mtu, ukiona mtu anatoka na huyu kesho yupo na yule, huumia sana ndani kwa ndani. Wewe usiwe na kama hao wenye staili hizo, hakikisha uvumilivu unakuwa silaha yenu kila siku kwenye uhusiano wenu.

AMINI KATIKA KUFUNDISHA
Utamkuta akiwa na tabia ambazo hazikufurahishi. Kila siku amini katika kufundisha. Mwelekeze kila siku na usichoke. Jitihada zako za mafundisho zitakuletea matunda mazuri sana ambayo utayavuna baadaye. Kuna watu mpaka wanaingia kaburini wanakuwa wameacha msururu wa wapenzi, ni kwa sababu hawakuamini katika kufundisha.

Hawakujua kama kila kinachoelea kimeundwa. Usimuone mpenzi wa mwenzako ana tabia njema ukadhani kila kitu kilikuja kwake kama zawadi, ipo kazi ambayo aliifanya mpaka amekuwa hivyo. Alimfundisha bila kuchoka ndiyo maana maisha yao leo ni mazuri.

Suala la kufundisha linajikita katika kipengele cha uvumilivu, yaani lazima umvumilie mwenzi wako pale unapoona anaonesha vitendo ambavyo hukubaliani naye. Ukitaka ukutane naye leo halafu awe na mwenendo chanya kwa kila kitu kama utakavyo, utasubiri sana.

Lazima aje mtu ambaye yupo tofauti halafu umfundishe kuwa bora. Kipindi unamfundisha atakukosea mara nyingi lakini wewe piga moyo konde. Endelea kumvumilia kwani elimu unayompa, mavuno yake utayapata baadaye, kipindi ambacho utaishi naye kwa raha mustarehe.

Siyo mmegombana kidogo ndiyo muachane, ni sehemu ya mapito ya kimaisha kwa wapenzi. Hayupo katika misingi unayoitaka, kwa hiyo fanya kilicho sahihi kumuelimisha kadiri inavyotakiwa. Vilevile usitarajie kwamba utamfundisha leo halafu siku hiyohiyo abadilike.

Lazima umpe muda, atabadilika taratibu. Kuna maisha mazuri sana baada ya yeye kuelewa mafundisho yako. Zipo faida nyingi kwako wewe ambazo zitakufanya baadaye ukae ukijivunia namna ulivyosimama imara kumbadilisha. Hivyo ndivyo mapenzi yanataka.

KUWA NA MATARAJIO CHANYA
Inaonekana hamuivi leo kwa sababu kuna masuala yanawagombanisha lakini wewe jenga matarajio chanya juu yake halafu pita njia sahihi wakati wa kuishi naye. Anakuudhi, pengine anakufanya mpaka ukose usingizi, swali la kujiuliza ni moja tu; je, mnapendana?

Maudhi na migogoro, haviondoi ukweli kwamba mnapendana. Kichwani weka imani kwamba baada ya migogoro na maudhi kuna maisha mazuri yaliyojaa maelewano ambayo yatatamalaki. Huu ni muongozo ambao ukiushika kikamilifu, utakupa dira sahihi ya maisha yako.

Mtu aliye na matarajio chanya kwa mwenzi wake, hawezi kuyumbishwa na vitu vidogovidogo. Hatakimbilia kutamka maneno mabaya dhidi ya mpenzi wake kwa sababu ndani yake kutakuwa na imani kwamba wanapendana na huko mbeleni mambo yatakaa sawa, isipokuwa sasa kuna mambo tu ya mpito yamejitokeza.

Migogoro ni Shetani, ukiruhusu itawale maana yake uhusiano wenu hauna baraka za Mungu. Hapa namaanisha kwamba kama ni ndoa basi haimpendezi Maulana. Tafakari sasa ni kwa nini ndoa yako haipo kwenye jicho limpendezalo Mungu? Chukua hatua.
Kufukuzana ni tafsiri ya Shetani kushinda, pingana na utawala wa ibilisi katika uhusiano wako kwa kuweka matarajio chanya kwa mwenzi wako.

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: