Wednesday, October 23, 2013

Magufuli anuna

  Hakuna kilichofanyika agizo la Pinda
  Ni kumaliza mvutano usafirishaji malori
Agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, la kuundwa kwa timu ya kusaka mwafaka wa mgogoro baina ya Serikali na wadau wa usafirishaji ndani ya mwezi mmoja bado limekwama.

Wasafirishaji ambao ni Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) na Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa) waliogoma kwa siku kadhaa wakipinga serikali kufuta msahama wa ongezeko la tozo ya asilimia tano katika mizani kuanzia Oktoba 1, mwaka huu, hadi jana walisema hawajapata maelezo yoyote kutoka serikali juu ya utekelezaji wa maagizo ya Pinda.


Mgomo huo ulitokana na tangazo la kufutwa kwa msamaha huo lilitolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na kusababisha malalamiko kutoka kwa Tatoa na Taboa na baadaye kugoma.

Oktoba 10, mwaka huu, Waziri Pinda alitoa mwezi mmoja kwa Wizara ya Ujenzi kukutana na wadau mbalimbali kwa kwa ajili ya kupitia hoja zote zinzolalamikiwa na washafirishaji hao.

Pinda aliingilia kati ili kumaliza mgomo wa malori ambao ulikuwa umedumu kwa zaidi ya wiki moja tangu kuanza kutekelezwa kwa amri ya Waziri Magufuli.

Wadau hao ni Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taboa na Tatoa.

Hata hivyo, hadi kufikia jana takribani wiki mbili baada ya agizo la Pinda, hakuna kilichofanyika ikiwamo kuwajulisha wadau hao lini wanatakiwa kuhudhuria vikao vya kusaka mwafaka.

Msemaji wa Tatoa, Elias Lukumay, akizungumza na NIPASHE kuhusu hatua iliyofikiwa ya kuundwa kwa timu hiyo, alisema hadi sasa hawajapewa taarifa yoyote ya kuitwa au maelekezo juu ya kuundwa kwa timu hiyo.

Alisema kwa upande wao wameshamwandaa mwakilishi atakayekwenda kuwawakilisha katika vikao hivyo, lakini wanashangaa kuona siku zinakwenda bila kupewa taarifa yoyote ya kuitwa.

“Toka siku ile Waziri Mkuu alipotoa lile agizo hadi leo (jana) hatujaona barua wala wito wowote wa kutakiwa kuhudhuria katika timu ingawa sisi tumeshajiandaa,” alisema Lukumay.

Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alipotafutwa alisema hawajapata taarifa yoyote ya kuitwa katika timu hiyo na hawajui kinachoendelea.
Alisema Serikali inatakiwa kuwa makini katika jambo hilo bila kulipuuzia kwa kuwa linaweza kuleta athari kubwa zaidi za kiuchumi.

Alisema Serikali haiwezi kufanya maendeleo yoyote katika sekta ya usafirishaji bila kuwashirikisha wadau wa usafirishaji.

Mrutu alisema ni jambo la kushangaza hadi sasa hakuna sera ya usafirishaji na serikali imekaa kimya bila kuchukua hatua zozote.

Ofisa Habari katika Waziri Mkuu, Augustin Tendwa,  alipoulizwa hatua iliyofikiwa katika uundwaji wa timu hiyo, alisema Ofisi ya Waziri Mkuu inatakiwa kupokea taarifa ya kuundwa kwa timu hiyo kutoka katika Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi.

Alisema ni vigumu kufahamu kama mrejesho umepelekwa ofisini hapo kwa kuwa Waziri Mkuu na wahusika wakuu wa kuyatolea majibu hayo wako nje ya nchi kikazi.

KWA MAGUFULI KIMYA
NIPASHE lilipomtafuta Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, simu yake haikupatikana.

Hata hivyo, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema hafahamu lolote juu ya maendeleo ya kuundwa kwa kamati hiyo kwa kuwa yuko Mkoani Tabora katika ziara ya Waziri Magufuli.

Alisema anatarajia kurudi Dar es Salaam wiki ijayo, na kumtaka mwandishi asubiri hadi atakaporudi ndipo atapata majibu sahihi.

Msemaji wa Wizara ya Uchukuzi, William Budoya, alipotafutwa alisema muda uliopangwa na Waziri Mkuu bado haujaisha na kumtaka mwandishi awe mvumilivu hadi kipindi kilichowekwa kitakapomalizika.

“Be patient (kuwa mvumilivu) mwezi ukikamilika tutawaeleza, kwa sasa ni mapema sana,” alisema  Budoya.

Oktoba 9, mwaka huu mabasi yaendayo mikoani yaligoma kwa muda wa saa sita baada ya kugomea maamuzi yaliyofanywa na Waziri Magufuli ya kufuta msamaha wa tozo ya asilimia tano kwa wasafirishaji wa malori na mabasi kwa uzito unaozidi. Tangazo la Waziri Magufuli lilisababisha vilio kutoka kwa wasafirishaji na kufuatiwa na mgomo huo.

Hali hiyo ilimlazimisha Waziri Mkuu kuingilia kati na kutengua maamuzi ya Waziri Magufuli na kuagiza kuundwa kwa timu ya kumaliza mgogoro huo.
Mvutano kati ya Wizara ya Ujenzi na wadau wa usafirishaji ulisababishwa na kanuni ya 7 (3) ya Sheria ya usafirishaji ya mwaka 1973 ambayo Waziri Magufuli aliitumia kufanya maamuzi hayo.

Pinda wakati akitangaza uamuzi wa kusitisha tangazo la Waziri Magufuli, alisema sababu ya mgogoro huo ilikuwa ni barua ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba, ambayo aliiandika mwaka 2006 ya kutoa msamaha kwa tozo kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubaliwa kisheria.

Hata hivyo, alisema Waziri Magufuli aliamua kutumia sheria kwa kuwa mwongozo wa Mramba haukuwa wa kisheria.

ATHARI ZA MGOMO

Mgomo wa wasafirishaji ulisababisha Bandari ya Dar es Salaam kuelemewa kutokana na kuzidiwa mizigo.

Takribani tani 23,165 za mbolea ambazo zilikuwa zimeshushwa bandari hapo zilikwama kutokana na kutokuwapo kwa malori.
Sambamba na hilo, takribani meli tisa za mizigo zilikwama kushusha na kupakia mizigo bandarini.

Kadhalika, uwezo wa kushusha makontena katika bandari hiyo ulishuka kutoka makontena 800 kwa siku hadi 300.
CHANZO: NIPASHE

No comments: