Wednesday, October 23, 2013

Simba, Yanga hasira zote leo

Wakati  Simba na Yanga zikiwa katika viwanja tofauti leo kwa ajili ya mechi zao kukamilisha raundi ya 10 ya Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, makocha wa timu hizo, Jamhuri Kihwelu 'Julio' na Mholanzi Ernie Brandts wametamba kupata matokeo mazuri leo.

Simba yenye pointi 19 katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi, itajaribu kurejea kileleni wakati watakapocheza dhidi ya Coastal Union ugenini Tanga, huku mabingwa Yanga waliopoteza uongozi wao wa magoli 3-0 katika sare 3-3 dhidi ya Simba Jumapili, watawakaribisha Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Azam wanaongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 20, sawa na Mbeya City, ambazo zimeshacheza mechi zao za raundi ya 10.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kutoka Tanga, kocha msaidizi wa Simba, Julio alisema kuwa wamejiandaa kufanya vizuri na kila mechi kwao ni sawa na fainali.

Julio alisema kuwa kwenye ligi msimu huu hakuna mechi rahisi na kwamba jambo hilo limethibitishwa na matokeo mengi yasiyotarajiwa msimu huu.

Alisema kwamba hawataidharau Coastal Union licha ya kupoteza mechi zake mbili mfululizo zilizopita dhidi ya timu ya mkiani ya Ashanti United na Kagera Sugar kwa sababu mchezo wa soka hautabiriki.

"Tunashukuru hatuna majeruhi wala mgonjwa, tumejipanga kuingia uwanjani kusaka ushindi, hakunamechi rahisi, ingawa tunajua kuna mchezo unafanyika kwenye mechi zetu ila hakuna anayeweza kubishana na Mungu," Julio alisema.
Hata hivyo aliyekuwa kocha mkuu wa Coastal Union, Hemed Morocco, amesema kwamba leo hataongoza timu hiyo kutokana na kumaliza mkataba wa kukifundisha kikosi hicho.

Alisema kwamba leo atakaa jukwaani akishuhudia mchezo huo na anachosubiri kwa sasa ni kulipwa haki zake.
Huenda leo Coastal Union itaongozwa na kocha wa muda, Yusuph Lazaro.

Kocha wa Yanga, Brandts alisema watahakikisha wanashinda mechi ya leo dhidi ya Rhino ili kupoza uchungu wa kupata sare dhidi ya watani wao wa jadi, Simba Jumapili.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mazoezi ya kikosi cha Yanga kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola uliopo Mabibo jijini Dar es Salaam, Brandts alisema matokeo waliyoyapata Jumapili yamemsikitisha yeye, benchi la ufundi, wachezaji, viongozi pamoja na wanachama wa Yanga lakini haikuwa dhamira yao kupoteza mchezo huo waliokuwa mbele kwa 3-0 hadi mapumziko.

"Tulikuwa tunaongoza 3-0 mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, lakini kipindi cha pili wachezaji wetu walizembea sana, hawakucheza kwa umakini na hawakusikiliza maelekezo ya benchi la ufundi hali iliyofanya wapinzani wetu kusawazisha mabao yote matatu," alisema Brandts.

"Tunawaomba radhi kwa wapenzi, mashabiki na wanachama wa Yanga kwa ujumla kwa matokeo ya juzi, tulistahili kushinda lakini kutokuwa makini kwa wachezaji wetu ndiko kulisababisha matokeo hayo kubadilika, kikubwa kwa sasa nimeongea na wachezaji na wameahidi kutorudia makosa katika mechi zinazofuata," alisema zaidi Brandts.

Wakati Yanga wakipanga kupoza uchungu, kocha wa Rhino, Sebba Nkoma aliliambia gazeti hili jana kuwa kikosi chao kilichokuwa kimeweka kambi Pwani kujiandaa kwa mchezo huo dhidi ya Yanga kiko vizuri na wana uhakika wa kupata ushindi katika mchezo wa leo.

"Tunatambua kwamba Yanga wanazihitaji pointi tatu Jumatano lakini sisi tunazihitaji zaidi kuliko wao. Tumepoteza michezo yetu miwili iliyopita dhidi ya Mbeya City na Ruvu Shooting, sasa tunasaka pointi dhidi ya Yanga, alisema Nkoma.

Aidha, mshambuliaji hatari wa Rhino, Saddy Kipanga ametamba kuifunga Yanga katika mechi hiyo ili kumshawishi kocha wa timu ya taifa (Taifa Stars), Mdenmark Kim Poulsen kumjumuisha katika kikosi chake.

Kipanga (23), ambaye ana rekodi ya kuifunga Simba magoli matatu katika mechi tatu mfululizo walizocheza mwaka huu, alisema kuwa kwa sasa yuko Ukanda wa Pwani kwa lengo moja tu la kuifunga Yanga katika mchezo huo.

"Nimewafunga Simba katika mechi zote tulizokutana nao. Sasa nawasubiri Yanga kesho (leo) niwafunge pia ili kumshawishi kocha wa Taifa Stars (Kim Poulsen) aniite kwenye timu yake," alisema Kipanga, ambaye tayari uongozi wa Simba umeshaeleza nia yao ya kumsajili katika kipindi cha dirisha dogo la usajili mwezi ujao.

Kipanga, ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara msimu uliopita, akifunga magoli 12 katika mechi 14, ameifunga Simba mechi tatu mfululizo mwaka huu zikiwamo mbili za kirafiki walizotoka sare ya 1-1 kabla Simba kushinda 3-1 katika mechi ya pili.

Nyota huyo wa zamani wa timu ya Royal FC de Muramvya inayoshiriki Ligi Kuu ya Burundi pia alifunga goli la pili lililoipa Rhino sare ya 2-2 katika mechi yao ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora Agosti 24.

Mzaliwa huyo wa Nzega, Tabora na baadhi ya viongozi wa Rhino Rangers walikuwapo kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili kusoma mbinu za kikosi cha Yanga kilichokuwa kikicheza dhidi ya Simba.

Rhino inakamata nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14 ikiwa na pointi saba baada ya kucheza michezo tisa ikifunga magoli nane huku Kipanga akifunga magoli manne peke yake.

Mechi nyingine itakayochezwa leo ni kati ya Prisons watakaoikaribisha Kagera Sugar kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: