ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 1, 2013

Mahakama kuamua ombi la Sheikh Ponda leo

Kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, inatarajiwa kusikilizwa tena leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro na kutolewa  uamuzi wa ama kumfutia shtaka la kwanza linalomkabili au kulihamisha katika Mahakama Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo inatokana na Wakili wa Sheikh Ponda, Juma Nassoro, kuwasilisha ombi lingine mahakamani hapo Septemba 17, mwaka huu, akitaka shitaka la kwanza la kutotii amri halali linalomkabili mteja wake lifutwe.


Wakili Nassoro anadai kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza shitaka hilo, vinginevyo lifunguliwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

 Nassoro, ambaye anaongoza jopo la mawakili wenzake wawili kumtetea Sheikh Ponda, aliwasilisha ombi hilo, baada ya mahakama hiyo kumnyima dhamana mteja wake.

Sheikh Ponda anakabiliwa na mashitaka matatu; ambayo ni kutokutii amri halali, kuharibu imani za dini na kushawishi kutenda kosa.

Alinyimwa dhamana na Hakimu Richard Kabate baada ya kupitia vifungu vya sheria na kukubaliana na ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) lililowasilishwa mahakamani, Agosti 28, mwaka huu, kupitia Wakili wa Serikali, Bernard Kongola.

Katika ombi hilo, DPP aliiomba mahakama kutompa dhamana Sheikh Ponda kwa sababu ya maslahi ya nchi pamoja na usalama wake.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: