ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 1, 2013

Wadau Pemba wataka marekebisho sera ya elimu

Pemba. Wadau wa elimu katika Shehia ya Tondooni na Makangale Wilaya ya Micheweni, wameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuifanyia marekebisho sera ya elimu ili iweze kuwanufaisha na wanafunzi wa shule  za vijijini .
Walisema sera hiyo ilipotungwa  ililenga zaidi mazingira ya shule za mijini kuliko yale ya shule za vijijini, jambo ambalo limeifanya kuwa ngumu kuitekeleza .
Wakizungumza kwenye mdahalo wa kuimarisha kiwango cha elimu katika shehia zao , walisema sera ya kuanzishwa kwa skuli za maandalizi inawalazimisha watoto kutembea umbali wa masafa marefu kutoka majumbani kwao.
Wamesema  sera hiyo kwa watoto wa mijini ni rahisi kutekelezeka kutokana na kuwepo na usafiri wa uhakika,pamoja na maeneo ya shule kuwa karibu zaidi na makazi yao .
Hata hivyo,baadhi ya washiriki wa mdahalo huo wameeleza kwamba kushuka kwa kiwango cha elimu katika shule hizo  zaidi kumechangiwa na wazazi kukosa umoja katika kudhibiti wimbi la utoro kwa wanafunzi .
Akichangia katika mdahalo huo , Eliza Andrea alisema baadhi ya wazazi wanashindwa kuwakemea na kuwahimiza watoto kuhudhuria masomo darasani hali ambayo inawafanya watoto kuendelea kujihusisha na vitendo vya ajira zisizo rasmi .
 Akitoa ufafanuzi wa nini kifanyike kuboresha kiwango cha elimu katika shehia hizo , Katibu wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Msitu wa Ngezi na Ufukwe wa Vumawimbi (Ngenareco),Mohammed Nassor Salim aliwataka wazazi kushirikiana na walimu , wanafunzi pamoja na kamati za shule kuhakikisha wanafunzi wote wanahudhuria masomo yao .
Alisema ili kufanikisha azma hiyo , kila mzazi anapaswa kuifanya familia yake kuwa  kituo cha elimu , kwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.

No comments: