Wednesday, October 23, 2013

Mkuu Polisi Upelelezi acharangwa mapanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Luteni (mstaafu) Chiku Gallawa kulia akimjulia hali askari aliyejeruhiwa na mapanga wakati wa vurugu zilizotokea wilayani Lushoto mkoani Tanga hivi karibuni

Vurugu kubwa zimetokea katika kijiji cha Viti kata ya Shume Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ambazo zimesababisha Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai wilayani humo (OCCID), Ufoo Maanga, kucharangwa mapanga na wananchi naye kujihami kwa kumuua mmoja na kumjeruhi mwingine kwa kuwapiga risasi.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Majid Mwanga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia juzi wakati askari ambao idadi yao haijajulikana walipokwenda usiku wa manane kwa ajili ya kumkamata mtuhumiwa mmoja kijijini hapo katika mgogoro wa ardhi.

Mwanga ambaye hakueleza kwa undani juu ya tukio hilo, alisema upelelezi wa tukio hilo umeanza ili kubaini chanzo chake na kuwataka wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mikononi.

“Polisi walikwenda pale kufanya kazi yao ya kumkamata mtuhumiwa katika kesi ya mgogoro wa ardhi, walipofika kijijini hapo wakapokewa kwa kushambuliwa kwa mapanga na wanakijiji,” alisema Mwanga.

Aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika tukio hilo amefahamika kwa jina la Khamis Seif na aliyejeruhiwa ni Athumani Abdallah Mngazija ambaye amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto akiendelea na matibabu.

Aidha, OCCID aliyejeruhiwa kwa kucharangwa mapanga na wanakijiji kichwani na kwenye vidole alihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Bombo kutoka Hospitali ya Wilaya ya Lushoto alikokuwa amelazwa awali.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe, alisema kufuatia tukio hilo mtu mmoja amekamatwa na kwamba uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea.

Hata hivyo, Kamanda Massawe, hakumtaja kwa jina mtuhumiwa aliyetiwa mbaroni.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Viti, Samuel Shelukindo, akizungumza na NIPASHE kwa simu, alisema juzi askari kadhaa walifika kijiji hapo mapema asubuhi na baadaye walikwenda kijiji cha Mtae.

Alisema ilipofika usiku saa 5:00 askari hao wakiongozwa na OCCID walifika kijijini hapo bila kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji, kitongoji wala kata na kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa katika kesi ya mgogoro wa ardhi aliyetajwa kwa jina la Mohamed Khamis na kumgongea mlango ili afungue.

Mohamed Khamisi ameshitakiwa na Athuman Rajabu maarufu kwa jina la Komba katika Baraza la Ardhi Wilaya ya Korogwe katika kesi namba 189/2013. Komba alipotafutwa katika simu yake hakupatikana.

Mwenyekti huyo alisema Khamis (mtuhumiwa) alikataa kufungua mlango wa nyumba yake na ndipo askari hao waliamua kuuvunja na kuingia ndani na watu waliokuwa wamelala ndani ya nyumba hiyo walipiga kelele kuomba msaada kutoka kwa majirani.

Shelukindo alisema baadaye majirani walitoka na kwenda katika nyumba hiyo na ndipo zikazuka vurugu ambazo zilisababisha OCCID kufyatua risasi kutoka katika bastola yake kujihami na kuua mtu mmoja na kujeruhi mwingine.

Alisema waliopigwa risasi ni Khamis Seif na Athuman Mngazija ambao usiku huo Mtendaji wa Kata ya Shume, Jamar Karanga, akisaidiana na wanakijiji waliwapeleka majeruhi hao katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.

Hata hivyo, usiku huo mmoja wa majeruhi hao ambaye ni Khamis Seif alifariki dunia akiwa hospitali kutokana na kuvuja damu nyingi.

Shelukindo alisema wanakijiji hao baada ya kuona wenzao wamepigwa risasi walipandwa na hasira na kuanza kumjeruhi OCCID kwa kumpiga ambaye aliokolewa na askari wenzake waliomchukua na kumwingiza katika gari yao na kuondoka kijiji hapo.

Aliongeza kuwa majeruhi katika tukio hilo ambaye bado anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto yupo chini ya ulinzi wa polisi na amefunga pingu ingawa hali yake bado ni mbaya.

Shelukindo alisema kitendo cha polisi kuvamia kijiji bila kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji husika siyo kizuri kwani wananchi wanategemea walindwe na polisi lakini kama wao ndio wanageuka kuwa wauaji siyo kitendo kizuri

“Mimi kama kiongozi wa kijiji nalaani kitendo cha polisi, watu wanategemea polisi kulinda raia na mali zao, lakini wao ndio wanaua,” alisema Shelukindo.

Mwenyekiti huyo alisema katika hali ya kushangaza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Lushoto haijafika kijijini hapo tofauti na matukio mengine.

Shelukindo alisema katika vurugu hizo mtu mmoja ambaye inadaiwa ndiye alikwenda polisi kulalamika amechomewa nyumba zake nne na wananchi wenye hasira.

Taarifa ambazo zimeifikia NIPASHE jana jioni zilieleza kuwa OCCID aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa Bombo ameruhisiwa baada ya hali yake kuimarika.
SOURCE: NIPASHE

No comments: