KWELI huu ni unyama wa wanaume hata kama si wote! Wanawake wawili wakazi wa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, wamepoteza maisha kufuatia madai ya kuuawa na waume zao. Inauma sana na Uwazi ndilo lenye mkasa mzima!
Matukio yote mawili yametokea jijini Dar es Salaam na kuacha vilio kwa ndugu na jamaa wakiwa hawaamini kilichowakumba wapendwa wao.
Wanawake waliojulikana kwa majina ya Mwanahamisi na mwenzake Waisiko Robert Mtundi ndiyo waliodaiwa kuuawa na waume zao, kisa kikubwa kikidaiwa ni hofu ya wanaume hao kusalitiwa katika mapenzi.
WANAODAIWA KUTENDA
Juma Shaban, mkazi wa Manzese Kwamfuga Mbwa na Samuel Gesire Mlimi, mwenye makazi yake Msongola, maeneo yote hayo yapo Dar ndiyo wanaodaiwa kutekeleza ukatili huo wenye kutoa machozi mpaka basi.
MWANAHAMISI ALIVYOUAWA
Ilikuwa saa tatu usiku, Septemba 21, mwaka huu, kila familia ya eneo la Kwamfuga Mbwa ilikuwa ndani kwa chakula cha usiku au maandalizi ya kulala, ndipo waliposikia zogo kutoka ndani ya chumba cha kwa wanandoa hao.
ZOGO NA MANENO
Kwa mujibu wa majirani hao waliozungumza na gazeti hili baada ya tukio, zogo hilo liliambatana na maneno ya shutuma kutoka kwa Juma kwamba mkewe huyo si mwaminifu ndani ya uhusiano wao.
Majirani walisema shutuma za Juma ziliambatana na kelele za Mwanahamisi kuomba msaada akisema ‘nauawa jamani! Nauawa mwenzenu!’
Wakasema baada ya kama saa moja ya mzozo ulipita ukimya, ndipo kila jirani alitoka nje na kuulizana nini kinaendelea ndani ya chumba cha Mwanahamisi na mumewe!
“Baada ya dakika kumi, tulimwona Juma akitoka chumbani kwake huku akiwa anabofyabofya simu yake ya mkononi na kutokomea kusikojulikana,” alisema jirani mmoja huku macho yakiwa yamevimba kwa sababu ya kumlilia Mwanahamisi ambaye wakati huo alikuwa chini ameshakata roho.
Akaendelea: “Baada ya Juma kuondoka tulipatwa na wasiwasi, tukaenda kumwangalia Mwanahamisi chumbani na kumkuta hajitambui, amelala kifudifudi, ana majeraha sehemu mbalimbali za mwili huku akiwa ametapakaa damu. Alikuwa akipumua kwa mbali.
“Alikuwa hawezi kuongea vizuri, mimi nilimsikia akisema hana uhai tena, tumwombee mtoto wake. Ndani ya chumba tuliona viroba vya pombe kali na kisu kikiwa kimelowa damu, nahisi ndicho alichotumia Juma kufanyia ukatili wake.
“Tuliamua kumwahisha hospitali Mwanahamisi lakini kutokana na hali yake tuliona ni vizuri kuwasiliana na polisi ambao walifika baada ya muda.
“Lakini siku yake Mwanahamisi ilitimia kwani wakati polisi wakijiandaa kumchukua kumkimbiza hospitali aliaga dunia.”
KUMBE NI MWEZI MMOJA BAADA YA KUHAMIA
Wengine waliozungumza na gazeti hili siku ya tukio huku wakitoa machozi, walisema Juma ambaye alitoroka baada ya ukatili huo, alihamia kwenye nyumba hiyo mwezi mmoja nyuma lakini walipata umaarufu mtaani hapo kutokana na tabia yao ya kupigana mara kwa mara.
MJUMBE WA MTAA NAYE ANENA
Akizungumza na gazeti hili katika eneo la tukio, Mjumbe wa Nyumba Kumi, Techla Tesha aliwalaumu majirani na wapangaji wa nyumba hiyo kwa kushindwa kumpelekea taarifa mapema huku wakijua mtuhumiwa alikuwa na tabia ya kumpiga mkewe mara kwa mara.
WAISIKO ALIVYOUAWA
Awali ya yote, inadaiwa Waisiko ni mke mkubwa, mke mdogo jina lake halikupatikana mara moja.
Siku ya tukio, saa tatu usiku inadaiwa Samuel alikwenda nyumbani kwa Waisiko ambapo si mbali sana na nyumbani kwa mke mdogo na kuangusha timbwili zito.
“Samuel aliingia ndani na kuanza kumpiga mkewe mkubwa huku akionya majirani kuwa asiwepo mtu wa kwenda kuamua ugomvi wao.
“Sisi kama majirani tuliogopa kwa sababu Samuel alikuwa akitishia kuwa atakayeingia atamchoma kisu.
“Licha ya vitisho hivyo, tulisimama nje ya chumba chao huku vitisho vikiongezeka lakini namna ya kutoa msaada tulishindwa. Hatukujua chanzo cha ugomvi wao.
“Kauli za mwanamke kila wakati ziliashiria alichokuwa akitendwa kwa wakati huo, mfano kuna wakati tulimsikia akisema anavunjwa mgongo, akasema anang’olewa kucha. Pia kuna muda alilalamikia kuvunjwa mkono. Jamani, marehemu aliteswa sana kabla ya kufariki dunia,” alisema shuhuda mmoja.
NI MATESO YA USIKU KUCHA!!
Shuhuda huyo aliongeza: “Mateso ya mwanamke huyo huenda yalikuwa ya usiku kucha kwani nakumbuka mpaka alfajiri ndipo tukasikia sauti ya mwisho ya Waisiko akisema Samuel umeshaniua, nimalizie kabisa basi. Baada ya hapo hatukusikia tena sauti wala vurugu.
SERIKALI YA MTAA YAZUNGUMZA
Makamu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msongola, Juma Chacha alipohojiwa kuhusiana na mauaji hayo, alisema ana taarifa lakini mtuhumiwa alikimbia baada ya kutenda unyama huo na anatafutwa na polisi.
UWAZI LABAINI KISA
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa mapenzi kwani ilidaiwa kuwa Samuel alikuwa akimhisi mkewe huyo kutoka nje ya ndoa.
Chanzo chetu kilisema siku ya tukio, Samuel aliwachukua baadhi ya marafiki zake na kwenda nao baa ambako aliwaambia kuwa anahisi mkewe huyo ana jambo kwani akimuuliza kitu anamjibu jeuri.
Mtoa habari wetu alisema Samuel akiwaambia marafiki hao kwamba siku hiyo akirudi nyumbani, mwanamke huyo atamtambua.
POLISI WALIVYOIKUTA MAITI
Polisi walipofika na kuichunguza maiti waliikuta imevunjwa mkono wa kushoto na kung’olewa kucha za miguu huku uti wa mgongo nao ukiwa umevunjika.
Habari zinasema mara baada ya mtuhumiwa kufanya mauaji hayo, alikwenda kwa mkewe mdogo na kumtaka akamuone mke mwenzie, alipokwenda yeye nyuma akatoroka.
Polisi Mkoa wa Ilala tayari wamemfungulia jalada mtuhumiwa huyo lenye namba STK/RB/10058/2013 MAUAJI.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Marietha Minangi amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo.
2 comments:
Tano Ladies na jumuia ya Wa-Tanzania,
Mmesoma kisa hik? Kinamhusu kila M-Tanzania. Kama siyo yeye binafsi, ana ndugu au rafiki aliyepitia vitisho au vitendo kama hivi. Upo umhimu wa kutoa elimmu kwa watoto wetu, wake kwa waume kutambua dalili za maonevu kama haya na kuchukua tahadhari mapema. Hili lazima lijadiliwe.
Ana Mukami
Ni kweli mama, kwani mambo haya yapo dunia nzima si Tanzania tuu!Afadhali huku watu wanaogopa kupigiwa 911. Lakini yapo.
Post a Comment