
Dar es Salaam. Uchu wa madaraka na kutokubali kutawaliwa, ndiyo hasa kimekuwa chanzo cha migogoro kadha wa kadha inayoendelea barani Afrika.
Baadhi ya vuiongozi wamekuwa kwa makusudi wakikataa kutoka madarakani, kutoa nafasi kwa wengine kuongoza nafasi hizo.
Tofauti na viongozi wengine Mwalimu Nyerere alitoka madarakani kwa hiyari yake. Kitendo alichokiita kung’atuka, kama alivyokielezea katika moja ya hotuba zake alizozitoa mwishoni mwa mwaka 1985.
Hadi sasa ni viongozi wawili tu barani Afrika walioweza kufanya maamuzi magumu kama hayo ya kuondoka madarakani bila shinikizo, huku katiba ikimruhusu kuendelea na awamu nyingine ya uongozi.
Nelson Mandela anatajwa kuwa kiongozi wa pili baada ya Mwalimu Nyerere kuwahi kuondoka madarakani kwa ridhaa yake, huku sheria ikimruhusu kuendelea na awamu nyingine ya uongozi.
Uongozi bora
Kuzaliwa kwenye familia ya kiongozi peke yake kulitosha kumfanya Mwalimu Nyerere, awe mmoja kati ya viongozi bora barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Licha ya harakati mbalimbali alizofanya katika kupigania uhuru wa Tanganyika, Nyerere alifaulu kuwa kiongozi aliyekubalika kwa wananchi wengi nchini, pia licha ya kupita katika hatua hizo siku zote Mwalimu alihakikisha misingi muhimu ya chama chake inazingatiwa vyema.
Kupiga vita ubepari na unyonyaji wa aina zote pia kudumisha uadilifu na nidhamu ndani ya chama katika ngazi zote. Msingi mwingine ni kudumisha na kutetea muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Pamoja na yote hayo Mwalimu alisimamia usawa wa binadamu kama msingi mkuu. Binadamu wote ni sawa na wanastahili haki sawa, kwa hiyo chama chake hicho kina wajibu wa kupiga vita ubaguzi wa kidini, kikabila na hata kijinsia.
Lakini hatua hizo kwa Mwalimu Nyerere alizingatia kama changamoto, zilizosaidia kumtoa katika hatua moja kwenda kwenye hatua nyingine.
Baada ya kutumikia taifa kwa muda mrefu na kuweka misingi madhubuti katika ustawi wake, Mwalimu Nyerere hakusita kuwaeleza watu wa karibu yake hususani ndani ya Chama chake juu ya dhamira yake ya kupumzika, katika nafasi yake ya uongozi na kuwaachia wengine kuchukua kijiti hicho huku yeye akiwa pembeni kama mwananchi wa kawaida.
Kwa mujibu wa wajuzi wa mambo Nyerere aliweka wazi dhamira yake hiyo mwishoni ya miaka ya sabini, ambapo alibainisha wazi kuwa angestaafu mwaka 1980.
Lakini kabla ya kuikamilisha dhamira yake, nchi ya Tanzania ikaingia kwenye vita kati yake na Uganda.
Vita hiyo ilikuwa kati ya mwaka 1978 na 79. Mwalimu Nyerere akiwa Amiri Jeshi Mkuu aliongoza vita hiyo hadi pale Tanzania ilipoibuka mshindi na kuikomboa ardhi yao, ambayo Uganda ilikuwa na mpango wa kuitaifisha.
Kutokana na ukweli kuwa hali ya nchi haikuwa nzuri kiuchumi na hata kiusalama, hivyo akaombwa aendelee na uongozi kwa miaka mitano zaidi.
Na hapo ndipo alipoendelea na uongozi hadi Novemba 7, 1985, alipoamua kung’atuka rasmi katika nafasi zake zote za uongozi ndani ya Chama na Serikali.
Tukio la kung’atuka kwake kutoka katika nafasi zake hizo limekuwa likitafsiriwa kwa mitazamo tofauti tofauti, licha ya ukweli kuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwake kufikia uamuzi huo.
Awali alishawahi kuachia ngazi katika madaraka yake ya Uwaziri Mkuu mwaka 1962, ili aende akaimarishe chama chake cha TANU.
Mwalimu Nyerere alipoeleza nia yake ya kung’atuka madarakani kama rais na baadaye kama mwenyekiti wa CCM, wananchi wengi sana walionyesha hofu kubwa, na hata baadhi yao walijaribu kumzuia asiondoke madarakani.
Licha ya ukweli huo lakini bado Mwalimu Nyerere alikuwa na sababu zake, zilizomsukuma hadi kufikia uamuzi wake huo.
Je, ungependa kufahamu sababu hizo?
Sababu kuu iliyomfanya baba huyo wa Taifa la Tanzania ang’atuke madarakani, ni pale tu alipoona amekwisha ijenga misingi muhimu na imara.
Misingi hiyo ni pamoja na umoja, amani, upendo, haki, usawa demokrasia uongozi wa nchi na maenedeleo katika nyanja za elimu, uchumi na siasa.
Hivyo aliona nchi iko vizuri na ingekuwa vizuri kuwapa nafasi Watanzania wengine, kuweka nguvu zao katika uboreshaji na uendelezaji wa misingi bora aliyoicha kwa kuendelea na yale yote mazuri yaliyofanya chini ya uongozi wa serikali yake ya Chama Cha Mapinduzi
Sababu za kung’atuka
Sababu hii haikuiweka pembeni ile ya kitendo chake cha kuongoza kwa muda mrefu, kwani alibainisha kuwa ana kila sababu ya kuwaachia uongozi watu wengine, kwani ameshaongoza kwa muda mrefu.
Mwalimu Nyerere mwenyewe anathibitisha hili katika moja ya hotuba zake alizotumia kuwaaga Watanzania
“Mtu baada ya kuongoza kwa muda mrefu wananchi wanakuchoka kwa hivyo, nimeona niachie madaraka huku watu wakiwa bado wananipenda,” anasisitiza.
Si hivyo tu katika hotuba yake hiyo, Mwalimu alielezea kazi atakayokuwa nayo mara baada ya kustaafu.
“Nimeamua kung’atuka ili niwe na kazi moja tu ya kutoa ushauri na maelekezo kwa viongozi vijana na kizazi kipya kwa ujumla,” anabainisha.
Kazi hiyo aliifanya vizuri zaidi kwa ufanisi, aidha nafasi hiyo ilimpa nafasi ya kubaini kasoro katika kipindi kirefu alichokuwa Rais wa nchi.
Mwalimu alitaka pia kutoa mafundisho kwa viongozi wengine wa Afrika ambao aghalabu wakishika madaraka hawataki kutoka, hata ikiwa vipindi vyao vya kutawala vimekwisha watang’ang’ania hata kwa mtutu wa bunduki.
Pamoja na sababu hizo zote mwalimu kama binadamu alihitaji kupumzika baada ya kulitumikia taifa la Tanzania kwa zaidi ya miaka 20. Aliona amefanya kazi ya kutosha kwa ajili ya taifa hili la Tanzania.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment