Jembe la Jangwani: Khamis Kiiza ni hatari sana, ukimuachia na kutoweka mikakati ya kumkaba lazima ulie na leo katupia 2. (PICHA NA BIZ ZUBEIRY)
Katika mechi nzuri ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyowakutanisha watani wa jadi kwa mara ya kwanza msimu huu, Yanga iliamini kwamba ingeweza kulipa kisasi cha mwaka jana cha kufungwa magoli 5-0 wakati ilipoenda mapumziko ikiongoza kwa magoli 3-0, mawili kutoka mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza na moja la Mrisho Ngasa.
Hata hivyo, Simba waliwanyang'anya Yanga utawala wa mechi hiyo katika kipindi cha pili na kurejesha magoli yote matatu kupitia kwa Betram Mwombeki, Mganda Joseph Owino na Mrundi Gilbert Kaze.
Licha ya Yanga kumaliza mechi hiyo kiujumla ikiwa imekaa na mpira kwa asilimia 51 dhidi ya za Simba 49, ilikuwa ni Simba iliyotawala kipindi chote cha pili baada ya Yanga kutawala cha kwanza cha mechi hiyo ambayo udhaifu katika ulinzi kwa pande zote mbili ulishuhudia magoli mengi ya kifungwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Azam TV iliyorusha moja kwa moja mechi hiyo kupitia televisheni ya taifa (TBC), Simba ilipiga mashuti nane yaliyolenga lango na sita yaliyoenda pembeni na hamna aliyeotea, wakati Yanga walipiga mashuti sita yaliyolenga lango, sita yaliyoenda kando na waliotea mara mbili.
Matokeo hayo yaliifanya Simba ifikishe pointi 19 na kubaki katika nafasi ya tatu, nyuma ya vinara Azam FC na Mbeya City zenye pointi 20 kila moja. Yanga ni ya nne ikiwa na pointi 16. Hata hivyo, Simba na Yanga zimecheza mechi moja pungufu.
Ulinzi uliimarishwa ndani na nje ya uwanja. Kulikuwa na magari ya maji yaliyokuwa yakizunguka nje ya uwanja na hapakuruhusiwa mtu kuingia na vitu, hata chupa ya maji.
Kikosi cha Yanga kilitangulia kuingia uwanjani saa 8:36 mchana kikipitia lango kuu ambalo wenyeji wa mchezo Simba walilikwepa.
Simba waliingia uwanjani saa 8:40 mchana wakipitia kwenye mlango wa Kaskazini kunako jukwaa la Simba, kisha kwenda kwenye vyumba vya kuvalia. Kipindi hicho mechi ya utangulizi kati ya vikosi vya vijana wa timu zote ilikuwa inaendelea.
Katika mechi hiyo ya utangulizi ya vikosi vya U20, Yanga iliyocheza pungufu (wachezaji 10) tangu kipindi cha kwanza, ililazimisha sare ya 1-1 dhidi ya vijana wa Simba.
Saa 9:16 mmoja wa 'vigogo' wa Yanga aliyekuwa amefuatana na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga alifika jukwaa la VIP A akasimama na kuanza kuwapungia mikono mashabiki wa Yanga huku akiwaonyesha ishara ya kuinuka kushangilia. Hali hiyo ililipua shangwe kwenye jukwaa la Yanga.
Dakika mbili baadaye, yaani saa 9:18 alasiri, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe alisimama kwenye jukwaa hilo hilo la VIP A kujibu mapigo kwa kuwapungia mikono mashabiki waliokuwa wamefurika kwenye jukwaa la Simba.
Yanga pia walikuwa wa kwanza kutoka vyumbani kupasha misuli moto saa 9:19 alasiri wakiongozwa na kiungo Nizar Khalfan aliyefuatwa na beki wa pembeni Juma Abdul, nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro', mchezaji 'kiraka' Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima 'Fabregas' kisha wachezaji wengine waliotoka kwa pamoja huku winga hatari Mrisho Ngasa akiwa wa mwisho kuingia uwanjani.
Dakika moja baadaye, yaani saa 9:20 alasiri, kikosi cha Simba kilitoka kupasha moto mwili kikiongozwa na kiungo 'fundi' Haruna Chanongo aliyefuatwa na kiungo mwingine hatari Ramadhani Singano 'Messi' kisha wachezaji wengine wakaingia uwanjani kwa pamoja.
Hadi saa 9:52 alasiri, Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kuketisha watazamaji 57,558 ulikuwa umefurika watu hadi kwenye korido huku eneo dogo upande wa Kaskazini Mashariki likisalia na viti vichache vilivyokuwa wazi kutokana na jua kali.
Baada ya refa mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) Israel Nkongo kupuliza kipenga kuanzisha mchezo saa 10:05 alasiri, Yanga walimiliki mpira kwa dakika mbili wakipiga pasi zao za 'Kituruki' bila mpira kuguswa na wachezaji wa Simba hadi pale Ramadhani Singano 'Messi' alipomnyang'anya mpira kwa nyuma beki wa kushoto wa Yanga, David Luhende.
Dakika ya tano Ngasa aliingia na mpira ndani ya boksi akatoa krosi kali lakini ikampita kwa nyuma mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu na kutoka nje. Ngasa alikuwa amepenyezewa pasi ndefu na kiungo fundi Mnyarwanda Haruna Niyonzima.
Dakika ya 10 mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza alikosa goli la wazi akiwa amebaki na kipa Mganda mwenzake Abel Dhaira alipopewa pasi murua ndani ya sita na Cannavaro lakini akapiga shuti nje kwa mguu wa kulia.
Dakika ya 15 winga hatari wa timu ya taifa (Taifa Stars), Ngasa aliifungia Yanga goli la kwanza akimalizia kwa mguu wa kulia krosi murua ya Mganda Kiiza aliyepokea pasi kutoka kwa Mrundi Kavumbagu, akakimbia pembeni kabla ya kutoa pande safi kwa mfungaji aliyekuwa ndani ya sita.
Goli hilo la Ngasa lilikuwa la tatu kwa mchezaji huyo wa zamani wa Kahama United, Kagera Sugar, Azam na Simba, katika mechi nne alizoichezea Yanga msimu huu baada ya kutoka kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi sita.
Mzaliwa huyo wa Mwanza alifunga pia goli la kwanza katika mchezo uliopita walioshinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba Oktoba 12 na amepika pia mabao mawili katika mechi hizo nne.
Dakika ya 23 Kavumbagu alikosa goli la wazi alipopenyezewa pasi na Chuji, akakokota mpira hadi ndani ya boksi lakini akajisahau mpira ukadakwa na kipa Dhaira miguuni mwake.
Kiungo Jonas Mkude wa Simba alilimwa kadi ya njano na refa Nkongo baada ya kumchezea rafu kiungo Frank Domayo wa Yanga katika dakika ya 32.
Kiiza alifunga goli la pili kwa Yanga akimalizia kwa mguu wa kulia mpira wa kurusha kama kona wa Mrwanda mwenye asili ya DRC Mbuyu Twite uliomparaza kichwani Didier Kavumbagu kabla ya kumfikia mfungaji katika dakika ya 36. Kiiza alifunga goli pia katika mchezo wa mzunguko wa pili msimu uliopita ambao Yanga ilishinda 2-0 dhidi ya Simba Mei 18.
Katika dakika ya pili ya majeruhi kipindi cha kwanza, Kiiza alipachika bao la tatu kwa Yanga akimalizia kwa mguu wa kulia pasi murua ya Kavumbagu aliyewalamba chenga mabeki Owino na Kaze baada ya kupokea mpira kutoka kwa Twite.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Simba wakibadilika kwa kiasi kikubwa na kufanikiwa kurudisha goli la kwanza dakika ya 54 kupitia kwa mshambuliaji Mwombeki aliyesajiliwa msimu huu akitokea Pamba ya Mwanza inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza.
Mwombeki alipenyezewa mpira na Mrundi Amisi Tambwe aliyekuwa ameanguka katikati ya Yondani na Cannavaro nje kidogo ya boksi.
Dakika ya 57 beki wa kati Owino aliifungia Simba goli la pili kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyochongwa na Ramadhani Singano 'Messi' baada ya kuruka peke yake bila ya ulinzi.
Wakati matokeo yakiwa 3-2, Ngasa angeweza kuifanya Yanga iongoze 4-2 alipobaki na kipa Abel Dhaira tu lakini Mganda huyo alipangua shuti la kulengwa la Ngasa katika dakika ya 65. Ngasa alikosa goli la wazi baada ya kuwalamba chenga mabeki wawili wa Simba.
Beki Mrundi Gilbert Kaze aliandikia Simba goli la tatu kwa kichwa akimalizia mpira wa 'fri-kiki' uliopigwa na nahodha Nasoro Masoud 'Chollo' baada ya Luhende kumchezea rafu Messi nje kidogo mwa boksi katika dakika ya 85.
Baada ya mechi hiyo kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema: "Yanga walicheza vizuri kipindi cha kwanza kwa kuachiwa mno nafasi na baadhi ya wachezaji wetu.
Tuliporudi kipindi cha pili tukacheza mpira baada ya kuwatoa waliotuangusha. Tulistahili ushindi mkubwa zaidi."
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts alisema: "Wachezaji wetu walichemsha kutokana na kusikiliza kelele za mashabiki wetu nje. Ni jambo la kusikitisha kukosa ushindi katika mechi mnayomaliza kipindi cha kwanza mkiwa mnaongoza 3-0."
Kibwagizo: Namba 17 Simba inavaliwa na Mrundi Amisi Tambwe wakati Yanga inavaliwa na mzaliwa wa Mwanza, Mrisho Ngasa.
Mashabiki zaidi ya sita wa Yanga walianguka na kupoteza fahamu wakati timu yao ikifunga magoli mfululizo na baadaye mashabiki wengine 11 wa Simba walipoteza fahamu wakati Simba ikisawazisha mfululizo.
Vikosi vilikuwa: Simba: Abel Dhaira, Nassoro Masoud 'Chollo', Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano 'Messi', Abdulhalim Humud/ Said Hamisi (dk.49), Betram Mwombeki/ Zahoro Pazi (dk.90), Amisi Tambwe, Haruna Chanongo/ William Lucien (dk.49)
Yanga: Ali Mustafa 'Barthez', Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athuman Idd 'Chuji', Haruna Niyonzima 'Fabregas', Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa, Hamis Kiiza/ Simon Msuva (dk.62).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment