ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 9, 2013

Simba yaongoza kupewa penalti Ligi Kuu Bara



Timu ya Simba inaongoza kwa kupewa penalti nyingi kuliko timu nyingine kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea.
Kwa mujibu wa takwimu zetu, tayari zimeshatolewa penalti 10 kwenye Ligi Kuu, huku Simba ikibahatika kupata nne kati ya hizo.

Na hakuna penalti iliyokoswa kati ya nne hizo za Simba. Kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Bara, Mrundi Amissi Tambwe, ambaye ana magoli nane baada ya mechi saba za ligi, amefunga penalti tatu huku nyingine moja ya Wekundu wa Msimbazi ikifungwa na Jonas Mkude.

Wastani huo mzuri wa Simba kupata penalti, huenda unatokana na safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kuwa kali, kiasi cha kuwafanya mabeki wa timu pinzani ama kucheza madhambi kwenye eneo la hatari au hata kukamata kwa mikono.

Wakati Simba ikiwa ni vinara wa kuzawadiwa penalti, Coastal Union na Azam FC zinafuatia kwa kubahatika kupata penalti mbili kila timu.

Nazo pia zimekwamisha wavuni penalti zote hizo kupitia kwa kiungo wao Jerry Santo aliyefunga mbili katika mechi mbili tofauti, huku Kipre Tchetche na Aggrey Morris nao wakiifungia Azam.

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya penalti 10 zilizopatikana kwenye ligi, nane zimewekwa wavuni na mbili zimekoswa.
Timu nyingine zilizopewa penalti ni JKT Ruvu na JKT Oljoro, lakini wachezaji wao walikosa.

Stanley Nkomola aliikosesha timu yake ya JKT penalti, wakati pia Babu Ally aliikosesha JKT Oljoro penalti siku ambayo ilicheza dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, mjini Arusha ambapo kipa Mganda Abel Dhaira alidaka 'tuta' hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: