Yanga licha ya kutia ugumu katika kutotaka mechi zao kurushwa 'live' na Azam TV, kituo hicho kipya cha televisheni nchini kitaendelea kurusha mechi zote za ugenini za mabingwa hao wa soka wa Tanzania Bara.
Ofisa Habari wa shirikisho la soka (TFF), Boniface Wambura aliiambia NIPASHE jana Azam TV itaendelea kuonyesha mechi za Yanga za ugenini kwa sababu haziko katika mamlaka yao.
Yanga walikataa mechi zao kurushwa na Azam TV walionunua haki za matangazo ya televisheni kwa Sh. bilioni 5.6 wakitaka wapewe fungu kubwa kuzidi klabu nyingine kwa madai wana mashabiki wengi zaidi nchini.
Hata hivyo, baada ya kuonekana kwamba Yanga hawana mamlaka na mechi za ugenini, miamba hao wa soka nchini wako tayari mechi hizo zionyeshwe lakini wakibaki na msimamo kwamba za nyumbani hazitaonyeshwa.
Wikiendi iliyopita, hata hivyo, mechi ya Yanga ya nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo Wanajangwani walishinda 2-0 Jumapili, ilirushwa moja kwa moja na Azam TV kupitia kituo cha televisheni cha TBC.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema walishangazwa na kitendo hicho.
"Sisi (Yanga) tulishangaa baada ya kubaini kuwa mechi yetu dhidi ya Mtibwa ilikuwa inarushwa 'live' na Azam TV kinyume cha makubaliano yetu na TFF. Waulizeni TFF kwanini mechi hiyo ilirushwa wakati Yanga haikuwa 'away' (ugenini).
Hata hivyo, mkataba uliosainiwa baina ya Azam Media na TFF ulijumuisha kurusha mechi za timu zote bila ya kujali kama ni Yanga ama timu gani.
Wakati huo huo, timu ya soka ya Azam FC leo itakuwa na fursa ya kuishusha Yanga katika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakati itakapoikaribisha Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi dhidi ya timu hiyo ya Tanga ambayo imepoteza mechi mbili mfululizo za nyumbani zilizopita, utaifanya Azam ifikishe pointi 14, mbili zaidi ya Yanga ambayo itakuwa na mechi moja mkononi.
Mgambo Shooting yenye pointi tano, ikiwa nafasi ya pili kutoka mwisho imeshinda mechi moja tu dhidi ya Ashanti United huku ikipoteza mbili nyumbani dhidi ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Kocha Mohamed Kampira ana kibarua cha kuhakikisha anapata pointi mbele ya Azam.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni Rhino Rangers itakayoivaa timu iliyo kwenye kiwango ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati JKT Ruvu watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utazikutanisha Oljoro JKT na Ruvu Shooting ya Pwani inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment