ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 9, 2013

Tamko la Vyombo vya Habari

TAMKO LA WADAU WA HABARI WALIOKUTANA KUJADILI MUENDELEZO WA SERIKALI WA KUFUNGIA VYOMBO VYA HABARI ,KATIKA HOTELI YA SERENA,JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 9 OKTOBA ,2013.
Wadau wa habari waliokutana jijini Dar es Salaam leo, tarehe 9 Oktoba 2013, wamesikitishwa na hatua ya serikali ya kutosikiliza kilio cha wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri, waandishi, taasisi za vyombo vya habari, wasambazaji wa magazeti na watu wengine wa kawaida, juu ya kuyaondolea adhabu magazeti matatu yaliyofungiwa na serikali ya MwanaHALISI, MTANZANIA na MWANANCHI.
Aidha, wadau wamesikitishwa na hatua ya serikali ya kupuuza kilio chao cha kuomba kusitishwa kwa sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976; na kudhoofisha mchakato wa kuibadilisha sheria hiyo iliyotajwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992 kuwa ipo kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile, tumesikitishwa na hatua ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene ya kudharau na kufanya uamuzi wa kuyafungia magazeti hayo bila kuyasikiliza na kupotosha umma juu ya jambo hilo.
Kwa msingi huo, wadau wameazimia yafuatayo:
1. Kusitisha kuandika, kutangaza na kupiga picha, shughuli zozote zitakazowahusisha au kuratibiwa na Mheshimiwa Fenella Mukangara na Assah Mwambene hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo. Adhabu hiyo inaanza mara moja kuanzia leo.
2. Wadau wa habari tutaendelea kupinga sheria ya magazeti ya mwaka 1976 kwa kupigia kelele kufutwa kwa sheria hiyo na kuongeza nguvu ya kisheria mahakamani kwenye kesi iliyofunguliwa na kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd, mwaka 2009 inayopinga sheria hiyo.
3. Tunaowamba wananchi wote watuelewe kwa kuchukua hatua hii.
Uamuzi huu umefikiwa leo na wadau wahabari, kutoka taasisi zifuatazo:
1. Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari (MOAT).
2. Jukwaa la Wahariri (TEF).
3. MISA Tan
4. Baraza la Habari Tanzania (MCT).
5. Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)
6. Dar City Press Club (DCPC)
7. Tanzani Human Rights Defenders (THRDC)

No comments: