ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 29, 2013

WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI MUSOMA WAANDAMANA WAKIDAI KUDHULUMIWA

KATIKA hali inayoonyesha Haki haiwezi kupatikana pasipo kuandamana,zaidi ya wanafunzi 500 kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari Manispaa ya Musoma wamefanya maandamano hadi kituo cha polisi mjini Musoma na baadae kwenda nyumbani kwa mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kile walichokidai kutapeliwa na mtu wasiye mjua kwa kushirikiana na walimu.
Wanafunzi hao walifanya maandamano mwishini mwa wiki baada ya mtu mmoja wasiyemfahamu kwa jina kupita mashuleni na kuonana na walimu kisha kueleza kutaka kuwafanyisha wanafunzi mitihani ya taaruma pamoja na michezo na kupewa zawadi mbalimbali kwa washindi.


Wakizungumza na Mwandishi wa Blog hii nje ya makazi ya mkuu wa Mkoa walipokwenda kutaka kueleza matatizo yao,wanafunzi hao ambao walianzia kituo cha polisi na kufukuzwa walidai walipewa fomu kwa kununua kwa shilingi elfu moja na elfu moja mia tano lakini yale waliyoahidiwa kufanyiwa hawakufanyiwa.


Mmoja wa wanafunzi hao aliyejitambulisha kwa jina la Leah Sospeter wa shule ya msingi Kamnyonge 'B',alisema mtu huyo baada ya kufika shuleni alionana na walimu kisha kupita kila darasa na kudai atawapa mitihani ya kuwajengea uwezo na kufanya mashindano mbalimbali ambapo washindi wangezawadiwa 'Laptop',baiskel,madaftari makubwa lakini hawakuviona.


"Sisi hatuwezi kukubali kutapeliwa wazazi wetu wameangaika kutupa pesa kwa lengo la kufanyishwa mitihani na michezo tunafika uwanjani hakuna cha mitihani wala michezo na uwanja umefungwa hatukubali tunataka turudishiwe fedha zetu.

"walitutangazia tukutane uwanjani wa karume saa 2 asubuhi tumekaa hadi saa 6 uwanja umefungwa baadae wanatupeleka ukumbi wa MCC wanatupa madaftari ya darasa la kwanza na kutupigia muziki tunataka turudishiwe fedha zetu,"alisema Wambura Simion wa shule ya msingi Kigera.

Wanafunzi hao walidai baada ya kuona wanazurumiwa haki yao walikwenda hadi kituo cha polisi musoma ili kuomba msaada wa kukamatwa kwa watu hao lakini waliambuliwa kufukuzwa na kuchukua maamuzi ya kwenda nyumbani kwa mkuu wa Mkoa baada ya kukuta ofisi yake imefungwa.

Baada ya kukusanyika nje ya makazi ya mkuu wa Mkoa na kufunga barabara kwa kuweka mawe wakitaka wamuone ili waeleza kilichowapeleka kwake,askari wa jeshi la polisi walifika katika eneo hilo na kuwatawanya wanafunzi hao ambapo walitawanyika na kupaza sauti tusipopewa haki yetu itatokea kama Soweto. 

Kutokana na sakata hilo blog hii lilifatilia katika ofisi ya Utamaduni na michezo ili kufahamu kama wanalijua suala hilo na Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Musoma Reuben Ruhende alikili ofisi yao ilitoa kibali cha kufanyika kwa mashindano hayo ambapo waombaji walijitambulisha kama watu wanaosaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu lakini hawakutekeleza kile walichokiombea kibali.

Alisema watu hao baada ya kuwapa kibali walifanya udanganyifu kwa kupita mashuleni na kuwachangisha wanafunzi fedha kwa maelezo ambayo hayakuwepo kwenye kibali chao na waliporigundua suala hilo walilitaarifu jeshi la polisi na kufanikiwa kukamatwa na wanashikiliwa na jeshi la polisi.

"Ni kweli Afisa Michezo alitoa kibali lakini waandaji wamefanya udanganyifu na ndio maana tulichukua hatua ya kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya dola naamini kwa nafasi yao watalifanyia kazi na haki kwa wanafunzi hao itapatikana,"alisema Ruhende.

No comments: