ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 6, 2013

YANGA YAIBAMIZA MTIBWA 2-0

Wachezaji wa Yanga, mfungaji wa bao la kwanza Mrisho Ngasa (katikati) Hamis Kiiza (kulia) na Simon Msuva, wakishangilia baada ya Ngasa kuifungia timu yake bao la kwanza kati ya mawili, yaliyoiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, leo jioni. Bao la pili lilifungwa na Didier Kavumbagu, huku mabao yote yakifungwa katika kipindi cha kwanza. Picha na Bin Zubeiry Blog

TIMU ya Yanga SC leo imefikisha jumla ya Pointi 12 na kupunguza pengo la pointi dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kupanda hadi nafasi ya pili baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-0 katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Simba SC inaendelea kushikilia usukani wa Ligi hiyo ikiwa na pointi 15, baada ya timu zote kucheza mechi saba.

Pasi ndefu ya Athumani Iddi ‘Chuji’ ilimilikiwa vyema na Mrisho Khalfan Ngassa, ambaye kama kawaida yake alimzidi maarifa beki Salvatory Ntebe kabla ya kufumua shuti na kumchambua kipa Hussein Sharrif ‘Casillas’ dakika ya sita.

Mrisho Ngassa tena alimtoka vyema beki wa pembeni wa Mtibwa, Paul Ngalema na kutia krosi maridadi iliyounganishwa vyema na Didier Kavumbangu dakika ya 24 na kuandika bao la pili.

Kipindi cha pili, Mtibwa walirudi wakiwa imara zaidi na kuonyesha upinzani kwa Yanga, wakijitahidi kuwadhibiti vizuri washambuliaji wa timu hiyo na pia kushambulia.

Hata hivyo, uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga iliyoongozwa na mchezaji bora Tanzania, Kevin Yondan uliinyima Mtibwa japo bao la kufutia machozi.

Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul dk77, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan dk59, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza/Said Bahanuzi dk80.
Mtibwa Sugar; Hussein Sharif, Hassan Ramadhan, Paul Ngalema, Salvatory Ntebe/Dickson Daud dk33, Salim Abdallah, Shaaban Nditi, Ally Shomary, Awadh Juma, Mussa Mgosi/Juma Luizio dk66, Shaaban Kisiga na Vincent Barnabas/Masoud Mohamed dk37.

Katika mchezo mwingine, Mgambo JKT imefungwa nyumbani 1-0 na Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga bao pekee la Peter Michael dakika ya 62.

No comments: