ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 13, 2013

BARAZA KUU LA USALAMA LAIONGEZEA UWEZO MISHENI YA KULINDA AMANI SOMALIA

Sehemu ya wanajeshi wanaouhudumu katika Misheni ya Umoja wa Afrika ( AMISOM) wakiwa katika majukumu yao ya kulinda amani nchi Somalia. Misheni hiyo imeongezewa uwezo wa muda na Baraza Kuu la Usalama wa Umoja wa Mataifa, katika mkutano wake uliofanyika siku ya jumanne uwezo huo ni pamoja na kuongeza idadi wa wanajeshi zaidi ya 4,000, upelekezaji wa helkopta pamona na vifaa vingine lengo likiwa kuiwezesha misheni hiyo kukabiliana vilivyo na vitisho vya wapiganaji wa Al-Shabaab
Na  Mwandishi maalum
Katika kuhakikisha kwamba Misheni ya  Umoja wa Afrika inakabiliana  vilivvo na kundi la wapiganaji  la Al-Shabaab, Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,  jana jumanne ,limepitisha kwa kauli moja  Azimio linaiongezea uwezo  muda   Misheni  hiyo.
Kupitia Azimio hilo  Misheni ya   Umoja wa  Afrika  katika Somalia kwa kifupi kama  AMISOM  inaongezwa   wanajeshi zaidi ya  4, 000 pamoja na misaada ya vifaa ili iwe   na uwezo  mkubwa  wa kukabiliana  vilivyo na ongezeko la vitisho kutoka  Al-Shabaab.

Aidha Azimio hilo ambalo lilipitishwa kwa kauli moja na wajumbe 15 wanaounda    Baraza  Kuu la Usalama,  pia limeongeza muda wa  mamlaka ya misheni hiyo  hadi  Octoba 31, 2014. Misheni ya Umoja wa Afrika  ya kulinda amani   nchini Somalia iliundwa mwaka 2007
Azimio hilo pia linaiomba  Umoja wa   Afrika  kuongeza nguvu ya jeshi hilo kwa maana  ya kuongeza  wanajeshi Zaidi kutoka 17,731 waliopo sasa  hadi kufikia 22, 126, na pia limeazimia kupanua   misaada yake ya kilojistiki  inayotolewa na Umoja wa Mataifa kwa Misheni hiyo  .
Aidha    Baraza Kuu la Usalama  kupitia azimio hilo, linasisitiza kwamba,  uamuzi huo wa kuiongezea nguvu  Misheni ya   Umoja wa Afrika    unalenga katika kuimarisha uwezo wa  kijeshi wa  AMISOM katika kipindi cha miezi 18 hadi 21  na kwamba baada ya  kipindi hicho tathimini itafanyika  kuangalia kama  kutakuwa na   haja ya kupunguza  nguvu ya   Misheni hiyo.
Taarifa  Zaidi zinaeleza kwamba  Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa na  Umoja wa  Afrika hivi karibuni kwa pamoja  walipendekeza kuimarishwa kwa  Misheni  hiyo ya AMISOM ikiwa ni pamoja na  kupelekewa helkopta  na  zana nyinginezo, kwa lengo la kukabiliana  na vitisho vya aina yoyote  katika pembe ya Afrika.
Vilevile kupitia  Azimio hilo Baraza  Kuu la Usalama   pia limepokea taarifa  kuhusu pendekezo la   Katibu  Mkuu  wa Umoja wa Mataifa la kutaka kupeleka  kikosi maalum cha kulinda  majengo yaUmoja wa  Mataifa nchini Somalia (UNSOM) ambayo ilianzishwa mweji Juni  kwa lengo  la  kuisaidia  Serikali  na wananchi wa  Somalia katika juhudi zao za kuleta usalama na ustawi.
Baraza pia  limetoa wito wa  kuongezea ushirikiano kati ya AU, Umoja wa Mataifa na Serikali ya Shirikisho ya Somalia, ikiwa ni pamoja   na utekelezaji wa  mpango  mpana wa amani, usalama na maendeleo.

No comments: