ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 13, 2013

Korti Kisutu yawaachia huru Hasanoo, wenzake wizi wa shaba

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemwachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (Corefa), Hassan Othman Hasanoo (45).

Pia, mwingine aliyeachiwa ni mfanyabiashara wa madini, Najim Msenga na Wambura Mahega baada ya kuwaona hawana hatia kwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Mashtaka hayo ni, wizi wa shaba yenye thamani ya Sh300 milioni. Baada ya kuachiwa huru kwa washtakiwa hao, ndugu zao waliokuwapo mahakamani waliangua kilio cha furaha

Kwa upande wake, Najim ambaye pia ni mjumbe wa NEC Taifa, aliishukuru mahakama kwa kutenda haki.Akisoma hukumu hiyo, ambayo imeandaliwa na Hakimu Devotha Kisoka, Hakimu Sundi Fimbo alisema washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kuiba na kujipatia mali ya wizi.

Mali hizo ni tani 26.475 za madini aina ya shaba yenye thamani ya Sh333, 467,848.13 zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Zambia kwenda Dar es Salaam, mali ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania Ltd.

Hakimu Fimbo alisema katika shtaka la kula njama mshtakiwa Hasanoo na Najim, ushahidi wa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kama walikula njama.

Pia, hakimu huyo alisema hakuna upelelezi uliowaonyesha washtakiwa hao wakiiba au wakipokea shaba.

Alisema kutokana ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi, mahakama inawaona hawana hatia na wapo huru.

Awali, akiongozwa na Wakili wake, Richard Rweyongeza kujitetea, Hasanoo alidai kuwa mashtaka yanayomkabili ni ya kubambikiwa na kwamba, kesi hiyo imemchafulia jina lake kwa jamii.

Aliongeza kudai kuwa, yeye hafahamu chochote kuhusiana na wizi wa shaba na kukutwa kwa mzigo huo kwenye yadi iliyopo Bahari Beach inayomilikiwa na mshtakiwa Najim.
Mwananchi

No comments: