Advertisements

Thursday, November 7, 2013

Kibadeni: Nitatimuliwa Simba

Yaichapa Ashanti 4-2, Mombeki atupia 2, Coastal yalala
Mshambuliaji wa Simba,Amis Tambwe,akijiandaakupiga shuti mbele ya beki wa Ashant United, Jaffari Gonga,wakati wamchezo huo. Picha na Habari Mseto

Simba imefunga mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuifunga Ashanti United kwa mabao 4-2, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni 'King' amesema hana uhakika wa kuendelea kukinoa kikosi hicho katika raundi ya pili itakayoanza Januari 25, mwakani.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana na kuchezeshwa na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani, Kibadeni alisema vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuwa atatimuliwa na kwamba hilo linaweza kutokea.


Alisema lengo lake lilikuwa kuijenga Simba na si mbio za ubingwa msimu huu, lakini uvumilivu umekosekana na anaonekana hafai wakati timu inapotokea kufanya vibaya.

"Lisemwalo lipo, hivyo kinachoripotiwa na vyombo vya habari huenda kikatokea, kwa sababu hawawezi kuandika pasipo kuambiwa," alisema kocha huyo ambaye msimu uliopita aliinoa Kagera Sugar.

Akitoa utabiri wake kwa upande wa timu itakayoweza kutwaa ubingwa huo, Kibadeni alisema Yanga ina nafasi kubwa ya kuutwaa ubingwa huo, huku Azam FC ikifuatia katika mbio hizo.

Katika mechi hiyo ya jana ambayo mwamuzi Shamba alimtoa kipa wa Ashanti, Amani Simba kwa kadi nyekundu katika dakika ya 90 baada kushika mpira nje ya 18 kwenye harakati za kumzuia Ramadhani Singano asifunge, Kibadeni alieleza kutofurahishwa na kiwango cha wachezaji wake licha ya kushinda.

Mabao ya Ashanti yalifungwa na Hussein Sued dakika ya 44 na Said Maulid (53'), wakati kwa upande wa Simba, Singano alianza kufungua milango dakika ya nane, Amisi Tambwe (47'), Betram Mombeki (49' na 63).

Baada ya mchezo huo, Kocha wa Ashanti, Nicholaus Kiondo alisema tumecheza vizuri lakini tumefanya makosa makubwa yatakayoweza kutugharimu kwa timu kubwa yenye uzoefu, huku akisifu safu yao ya ushambuliaji kwa kuonyesha kubadilika.

Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa jana Ruvu Shooting ilitoka sare ya 2-2 na Mtibwa Sugar. Mabao ya Ruvu yalifungwa na Elias Maguli dakika ya 31na, 69 kwa njia penalti), Mtibwa (Juma Liuzio dk.19, Shabani Kisiga dk. 40)

JKT Ruvu waliichapa Coastal bao 1-0 mfungaji akiwa Bakari Kondo dakika ya 35, wakati Kagera Sugar ikiichapa Mgambo JKT 2-0, mabao yakizamishwa kimyani na Themi Felix dakika ya 44 na Selemani Kibuta (61').
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: