Advertisements

Thursday, November 7, 2013

Kompyuta ya Mvungi yazua hofu

  Huenda ikawa na taarifa nyeti za Katiba Mpya
  Ahamishiwa Milpark Afrika Kusini kwa matibabu zaidi
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengodo Mvungi ambaye alicharangwa mapanga akihamishiwa hospitali ya Milpark Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Wakati Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengodo Mvungi ambaye alicharangwa mapanga akihamishiwa hospitali ya Milpark Afrika Kusini kwa matibabu zaidi, bado tukio la kujeruhiwa kwake limezingirwa na maswali mengi miongoni mwa jamii wakihoji inawezekana kuna jambo ambalo limejificha nyuma yake.

Jana Dk. Mvungi alisafirishwa kwenda Johannesburg kwa matibabu baada ya madaktari kushauri apelekwe nje kwa matibabu zaidi kutokana na kuendelea kuwa katika hali ya kutokujitambua tangu Jumapili alipojeruhiwa.

Deogratious Mwarabu, mototo wa kaka yake Dk. Mvungi, ambaye alisafiri naye kwenda Afrika Kusini jana, alisema kuwa wamemwamishia Milpark kwa kuzingatia ushauri wa madakari wa Moi wambao wamekuwa wanamuhudumia tangu Jumapili.

“Tunakwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi kwa kuzingatia ushauri wa madaktari. Hadi leo (jana) Dokta bado hajazungumza, kwa maana hiyo matibabu zaidi ni muhimu,” alisema Mwarabu.

Mwanasheria huyo mkongwe wa masuala ya katiba akihamishiwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi, bado kuna dhana zinazojengwa juu ya mkasa uliomkuta.

Kuna dhana kwamba huenda jamii inaamini kuwa wajumbe wa Tume wanalipwa fedha nyingi na hivyo kulikuwa na uwezekano wa kuwa na fedha nyingi nyumbani kwake.

“Inawezekana majambazi wale walijua kuwa Dokta (Mvungi) alikuwa na fedha nyingi nyumbani, ndiyo maana wakamvamia na kudai wapewe fedha,” alisema mmoja wa watu walio karibu na Dk. Mvungi.

Hata hivyo, pamoja na hisia hizo, kuna hofu miongoni mwa wadau wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa huenda taarifa muhimu na nyeti kuhusu rasimu ya Katiba Mpya zikawa mikononi mwa watu wasiostahili.

Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba miongoni mwa vitu vilivyoporwa nyumbani kwa Dk. Mvungi, Mbezi Msakuzi baada ya kupigwa mapanga na majambazi hao na kupoteza fahamu usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita, ni kompyuta yake mpakato (laptop) ambayo ni moja ya nyenzo zake za kazi.

Hofu hii inaelezwa kutanda ndani ya Tume kwa kuwa mbali ya kuwako na uwezekano huo, Dk. Mvungi kitaaluma ni mwanasheria aliyebobea katika masuala ya katiba kwa maana hiyo alikuwa nguzo muhimu sana kwa Tume hasa katika kipindi hiki cha mwisho cha kuandaa rasimu ya mwisho ya Katiba Mpya.

“Unajua Jumapili ile walifika viongozi wengi pale hospitalini. Wengi walionyesha kusikitishwa na unyama aliotendewa Dokta, lakini pia walionyesha wasiwasi wao juu ya wizi wa laptop yake… huenda taarifa za Tume zikawa ndani yake,” alisema rafiki huyo wa karibu wa Dk. Mvungi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, juzi aliliambia NIPASHE kuwa laptop aliyoporwa Dk. Mvungi bado haijapatikana licha ya kukamatwa kwa watu sita ambao wanashukiwa kuhusika na tukio hilo.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema jana pia kuwa laptop hiyo haijapatikana.

Kamishna Kova alisema kwa kuwa Dk. Mvungi alikuwa mjumbe wa Tume, kompyuta hiyo inaweza kuwa na kumbukumbu muhimu na kuahidi kuwa polisi watahakikisha wanaitafuta kwa udi na uvumba ili ili ipatikane.

Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, alisema tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa Dk. Mvungi siyo la kawaida na kwamba inawezekana limesababishwa na mambo kadhaa.

Alisema mojawapo ni tamko lililotolewa Bungeni ambalo halikuzingatia hali halisi ya nchi kwa kueleza kuwa wajumbe wa Tume hiyo wana fedha nyingi wanazolipwa na hivyo jamii ikawa imetafsiri kuwa wajumbe hao ni matajiri.

Profesa Baregu alisema wajumbe wa Tume hiyo wanavitegemea vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza suala hilo kubaini sababu za kuvamiwa kwa Dk. Mvungi.

“Hadi sasa tunaamini ni tukio la kijambazi, lakini tukio hili pia linaweza kuwa na hisia za kisiasa. Hata hivyo, tunaviamini vyombo vya ulinzi vitafanya kazi ya kuchunguza,” alisema.

Alisema tukio lililompata mwenzao haimaanishi kuwa litawatia hofu katika kutekeleza majukumu ya Tume kwani matukio ya kinyama ya aina hiyo yamekuwa mengi nchini.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray, alisema kuna wasiwasi wa jinsi vyombo vya ulinzi na usalama vinavyoshughulikia tukio hilo kutokana na kufanya kazi kwa kukurupuka bila kufanya uchunguzi wa kina.

“Watu wa upelelezi wazame chini siyo kukimbilia kukamata watu hovyo, ukamataji wa aina hiyo ni wa siasa za polisi, kimsingi usalama wa Watanzania kwa sasa haupo katika hali nzuri,” alisema.

Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha APPT Maendeleo, alisema tukio hilo linatia shaka na kwamba huenda kuna jambo limejificha nyuma yake hasa ikizingatia kuwa limempata mtu ambaye ni mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Dk. Mvungi alivamiwa na kujeruhiwa kwa mapanga Jumapili iliyopita na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwake Mpiji-Magohe, jijini Dar es Salaam.

Dk Mvungi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi alipelekwa kwenye Taasisi ya Mifupa Hospitali ya Muhimbili (Moi), ambako amelazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maaalumu (ICU).

Wakati huo huo, matokeo ya kipimo cha Control CT – Scan alichofanyiwa Dk. Mvungi, juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), yalionyesha kuwa hali yake bado siyo nzuri.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Mawasiliano wa Taasisi ya Magonjwa ya Mifupa na Fahamu (Moi), Almas Jumaa Dk. Mvungi anaendelea vizuri ingawa bado mpaka sasa hajapata fahamu.

“Vipimo vya Control CT – Scan ambacho alifamyiwa juzi Muhimbili, yanaonyesha kuwa kitabibu anaendelea vizuri, pamoja na kwamba bado hajapata fahamu mpaka sasa,” alisema Jumaa jana.
CHANZO: NIPASHE

No comments: