ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 9, 2013

Madilu: Ninatamani kuondoka mtaani

Dar es Salaam. Wiki iliyopita nilibahatika kuhudhuria Tamasha la Watoto wa Mitaani ambalo liliandaliwa na Shirika la ‘Hope for the Children’ maalumu kwa ajili ya kutafuta vipaji vya uimbaji na uigizaji.
Ilikuwa ni sherehe ya aina yake kati ya zile ambazo nimewahi kuzishuhudia. Kutokana na shauku ya kutaka kujua mengi kutoka kwa watoto hawa kwanza nilivutiwa zaidi na aliyeonekana kuwa mdogo kuliko wote.
Kwa kuwa tamasha hilo lilikuwa linafanyika katika eneo la wazi na kulikuwa na kelele nyingi, nilimwomba mhusika mmoja katika maeneo hayo aniruhusu niingie ukumbini kwa ajili ya kuzungumza na mtoto huyu.
Mtu huyo aliniambia ‘dada ningependa sana kukuruhusu ufanyie mazungumzo humu ndani, lakini hawa watoto hawaamiiki wanaweza kuiba kitu chochote hivyo ninachoweza kukusaidia ni kukupa viti tu, lakini mazungumzo mkafanyie nje’.
Ukiuliza hadithi za watoto wa mitaani kila mtu atakwambia anayoifahamu, zipo za kusikitisha, kufurahisha na kufundisha na hii ni moja kati ya hizo.
Katika maisha ya kawaida inapofika saa 11:00 alfajiri, familia nyingi huanza siku kwa kuamka na kujitayarisha tayari kukabiliana na pilika za siku nzima. Wazazi au wasaidizi wa ndani huwaamsha watoto kwa ajili ya kujiandaa kwenda shuleni.
Watoto huandaliwa kifungua kinywa wakati mwingine hulazimishwa kula ili washibe kwa kuwa shibe ni moja ya nguzo muhimu katika kutafuta elimu.
Kupata elimu, kulindwa, kutotumikishwa na kuthamini ni haki za msingi ambazo watoto wote duniani wanapaswa kuzipata na anapozikosa hizi ndiyo mwanzo wa kuzaliwa kwa watoto wa mitaani.
Nilizungumza na mtoto huyu aitwaye Madilu Ngonyani (12) ambaye katika umri huo pamoja na kuishi mtaani ana jukumu zito la kuitunza familia yake.
Swali la kwanza nililomuuliza ni kwa nini yupo mtaani kwa kuwa katika umri wake alipaswa kuwa shuleni, naye alinijibu akisema hajui kwa nini mpaka wakati huo mjomba wake hajamwanzisha shule ingawa mara kwa mara amekuwa akimpa ahadi hizo.
Ananisimulia sababu ya kuwa pale katika kundi la watoto wa mitaani akisema kuwa baba yake alimwacha kwa mtu ambaye ndiye sasa anayemwambia kuwa ni mjomba wake.
Hakumbuki lini alianza kuishi mitaani isipokuwa anasema baba yake anayemtambulisha kwa jina moja tu la Ngonyani alimwacha kwa mtu huyo akisema anarudi kijijini kwao mkoani Ruvuma kulima.
Hana kumbukumbu yoyote kuhusu mama yake na hajui kwa nini baba yake aliamua kumwacha kwa mtu huyo ambaye sasa ndiye ndugu pekee aliye naye hapa jijini Dar es Salaam.
“Zamani baba alikuwa ananipeleka Feri, akanifundisha kuuza samaki wale wanaoletwa kutoka baharini, alivyoondoka mimi nikaendelea kwenda Feri na ndiyo mpaka sasa ninafanya kazi hiyo,” anasema Madilu.
Siku ya Madilu haianzi kama zile za watoto wengine, yake huanza kama baba ambaye hulazimika kuacha nyumba ikiwa katika hali nzuri katika eneo ambalo anaishi Mwenge jijini na baadaye huondoka kwenda kutafuta riziki.
“Mjomba huwa ananiamsha asubuhi sana, nikiamka ninafagia uwanja, naosha vyombo halafu ninampikia chai ndiyo ninaondoka kwenda Feri,” anasema Madilu.
Anasema kwa kawaida anatakiwa awe ameshafika Feri jijini Dar es Salaam saa 12:00 asubuhi ili awahi kufanya udalali wa samaki na hulipwa Sh2,000 kwa siku.
“Nikifika Feri huwa nanunua chai ya Sh200 ambayo ninapata na maandazi mawili, baada ya hapo ninaanza kazi ya kuuza samaki ,” anasema Madilu.
Kazi yake huwa ni kuuza samaki kwa kuwanadi kwa wanunuzi mpaka pale watakapokwisha wote ndipo hulipwa ujira wake ambao haujawahi kuzidi kiasi hicho cha pesa.
Mwenyewe hafahamu kama wenzake hulipwa zaidi, lakini anachojua yeye akifanya kazi hiyo kwa siku lazima alipwe kiasi hicho cha pesa.
Jukumu lake haliishii hapo, kwani nyumbani ana kibarua cha kuhakikisha kila siku anampa mjomba wake Sh1,500 kutoka katika pesa anazozipata kwa siku.
“Mjomba aliniambia kila siku niwe nampa Sh1,500, kwa hiyo kwenye hela yangu ninabakiwa na Sh500 ambayo asubuhi ninaitumia kama nauli na ya kununulia chai kwa mama ntilie,” anasema Madilu.
Hajui mpaka sasa ameshampa shilingi ngapi mjomba wake huyo, lakini anasema anaendelea kumpa amuwekee ili aweze kumsomesha.
“Nilimwambia mjomba nataka kwenda shule kama watoto wengine, akaniambia atanipeleka ila niendelee kumpa pesa kila siku,” anasema Madilu.
Mtoto huyo anaongeza kuwa kuna wakati huwa wanafukuzwa Feri hali ambayo humlazimisha kufanya vibarua vya kubeba mchanga kutwa nzima na hapo hulipwa Sh3,000 kama ujira wake.
“Nikifukuzwa Feri huwa ninakwenda Tegeta kubeba mchanga, kwa siku ninalipwa Sh3,000,” anasema.
Pamoja na kupata pesa nyingi katika kibarua cha kubeba mchanga, mwenyewe anasema anapenda kazi ya kuuza samaki Feri, kwani ni nyepesi ukilinganisha na kubeba ndoo za mchanga kutwa nzima.
Akizungumzia uwepo wa watoto hao Meneja wa Soko la Samaki Feri, Charles Kapongo amekiri kuwaona watoto hao wakiranda katika maeneo hayo, lakini amekanusha kutumika kama madalali.
Kapongo amesema soko hilo lina madalali wanaotambulika, hivyo watoto hao hafahamu wanatumika vip,i kwani ni kinyume na taratibu zao.
“Sijawahi kumwona mtoto yeyote akifanya kazi ya udalali, hata hawa wanaozurura ovyo huwa tunawafukuza ingawa wamekuwa wakirudi mara kwa mara katika maeneo haya,” anasema Kapongo.
Kapongo ameongeza kusema kuwa Serikali inapaswa kutafuta suluhu ya kuwaondoa moja kwa moja katika eneo hilo na mitaa mingine kwa kuwa wanastahili kuwepo shuleni.
Akimzungumzia mtoto huyo na wengine wadogo wanaotumikishwa, mwanzilishi wa Shirika la Hope for the Children linaloshughulikia watoto wa mitaani, Joyce Mang’o anasema wanafanya jitihada za kuwaondoa katika ajira hizo na mitaani.
Joyce anasema kama shirika wanawajua watoto wote na vijiwe vyote wanavyopatikana, lakini wanashindwa kuwaondoa katika ajira au katika mitaa hiyo kwa kuwa hawana uwezo wala mahali pa kuwapeleka.
“Ni kweli wapo watoto wanaotumika katika vibarua, wengine ni wadogo zaidi ya Madilu, tunawakusanya kama hivi ili kuwaunganisha na jamii, lakini lengo letu kubwa ni kuwaondoa kabisa mitaani,” anasema Joyce.
Mwananchi

No comments: