ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 4, 2013

MULUGO "HATUJAFUTA ALAMA SIFURI MATOKEO YA MITIHANI "

Dodoma.Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema Serikali haijafuta daraja sifuri katika matokeo ya mitihani taifa ya shule za sekondari na kwamba ilichokifanya ni kuondoa mrundikano wa madaraja.

Mulugo aliyasema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM).
Magige alitaka kufahamu kama kushusha madaraja ni suluhisho la kuwaokoa vijana waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.

Mapema katika swali lake la msingi, Magige, alitaka kufahamu kama Serikali ina mkakati wa kuanzisha mpango maalumu hasa wa ufundi kwa wanafunzi waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.
Akijibu swali hilo, Mulugo alisema hawajashusha madaraja wala kuweka viwango tofauti na ilivyokuwa awali.

“Tumeongeza madaraja ili kuwatambua watoto, kulikuwa na mrundikano katika daraja moja. Serikali haijafuta division ziro na wala hakuna division V, ipo division I, II,III, IV na ziro kama kawaida,” alisema.

Alisema uamuzi wa kushusha madaraja, hauna lengo la kuwaokoa wanafunzi wanaofanya vibaya na badala yake, unalenga katika kuondoa mrundikano wa alama katika daraja moja.

Alitoa mfano wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kuwa lilikuwa linapanga daraja F kuanzia alama 0 hadi 34.

Alisema kulikuwa hakuna ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi kama kanuni inavyosema kuwa lazima kuwe na ufuatiliaji wa asilimia 50 kwa 50 .

Alisema kanuni hiyo inataka kutunzwa kwa alama 50 katika ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi na katika mtihani ya kumaliza shule asilimia 50.

Alisema wameanza kuyaweka madaraja kwa kutofautiana kwa alama 10 kila daraja.

Alisema bado daraja la ufaulu litaendelea kuwa 40 ama alama C.


ata hivyo, baada ya kumaliza kujibu swali hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliiagiza Serikali kupeleka bungeni kauli ya waziri kuhusiana na suala hilo.

“Naibu Waziri nenda mtuletee kauli ya Serikali kuhusiana na utaratibu huo ili kupata majibu yanayoridhisha,” alisema

Kuhusu wanafunzi waliofanya vibaya mwaka jana katika mitihani yao, Mulugo alisema Serikali haitaanzisha mpango maalumu wa ufundi kwa vijana hao.

Alisema badala yake, Serikali inawashauri wazazi kuwashawishi watoto kurudia mtihani wa kidato cha nne.

Kwa mujibu wa Mulugo, kwa mwaka huu, jumla ya watahiniwa 60,507 wa kujitegemea wamejisajili kufanya mtihani wa kidato hicho.

No comments: