Friday, November 22, 2013

RAIS KIKWETE KUWA MIONGONI MWA VIONGOZI MBALIMBALI WATAKAOPEWA TUZO

Rais Jakaya Kikwete.

NOVEMBA 23, mwaka huu, viongozi mbalimbai watapewa tuzo za kutambua mchango wao katika kuboresha afya ya mama na mtoto. Tuzo hizo zimeandaliwa na Taasisi ya Madaktari Waliosoma Vyuo Vikuu nchini (THPI), na miongoni watakaopewa tuzo ni Rais Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, mke wa Rais, Salma Kikwete na Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi

Kuhusu THPI, ilianzishwa mwezi Machi, 2009 na madaktari 12, na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Telesphory Kyaruzi, anasema wanaamini wakiwa wengi, watahudumia watu wengi na jamii kubwa zaidi. Anasema, hadi sasa taasisi ina madaktari wanachama zaidi ya 120 ambao wamesambaa nchi nzima. "Lengo kuu la taasisi yetu ni kushiriki katika kuhamasisha uboreshaji huduma za afya nchini na kushiriki kikamilifu katika kutoa huduma bora za afya kwa watanzania,"anaongeza. Madaktari hao ni wale walioamua kubaki nchini badalayakukimbilia nje ya nchi kufanya kazi...kwa kifupi ni madaktari wazalendo.

"Tuliamua kubaki nchini badala ya kwenda nchi za nje kutafuta maslahi mazuri zaidi kwa sababu ya uzalendo juu ya nchi yetu. "Dira ya taasisi yetu, tunaona watanzania wenye afya bora, huduma bora , na miundombinu bora katika kutoa huduma za afya nchini . Katika taasis yetu nguvu yetu ni umoja; wote ni sawa, kila mtu ni muhimu na kila mtu ni kiongozi. Nguvu yetu ni matumaini,"anaongeza.

Dk. Kyaruzi anasema ili kuwa na madaktari wengi sehemu mbalimbali nchini wanaotoa huduma za afya, taasisi imeanzisha Idara ya Uendelezaji Madaktari Vijana inayoratibu Mtandao wa Madaktari Vijana Nchini, ambao ni Madaktari Wanafunzi( Medical Students), Intern Doctors, na Madaktari wanaoanza kazi ili kuwajengea uwezo kitaaluma. Aidha, katika kutatua matatizo ya afya nchini, anabainisha kuwa wanaongozwa na mpango mkakati.

Katika mpango wa mwaka 2011/2014, taasisi imejielekeza katika kutekeleza malengo ya Milenia, lengo la nne na tano, afya ya mama na mototo. Na kufikia lengo la kupunguza vifo vya akina mama kwa 75% ifikapo mwaka 2015. Katika kutekeleza jukumu hili muhimu, taasisi imeanzisha kampeni ya kitaifa ya Saidia Mama Mjamzito Ajifungue salama, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kutokana na taarifa za jarida la umoja wa mataifa , Global Health and Deplomacy, duniani kina mama wajawazito 368,000 wanafariki kila mwaka, nafasi ya mama mjamzito kufa ni mara 100 zaidi katika nchi zenye
idadi kubwa ya vifo vya akina mama vinavyotokana na ujauzito. Akifafanua hilo, Dk. Kyaruzi anasema kuwa ni nchi 21 tu duniani ziko kwenye hatua sahihi katika kufikia malengo ya millennia ifikapo mwaka
2015. "Vifo vya mama wajawazito nchini kwa mwaka 2005 vilikuwa ni 578, kwa vizazi hai 100,000, na kufikia 454 kwa vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2012.

"Pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 122 kwa watoto hai 1,000 mwaka 2004 mpaka 81 kwa watoto hai 1,000 mwaka 2012. Na vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja ilikuwa 68 kwa watoto hai 1,000 kwa
mwaka 2004 mpaka 51 kwa watoto hai 1,000 kwa mwaka 2012,"anasema. Kutokana na juhudi kubwa za wadau, anasema wamefanikiwa kumepunguza idadi ya vifo vitokanvyo na ujauzito na vifo vya watoto wachanga, lakini lazima jitihada za kupunguza vifo vya mama na watoto ziedelee kwa nguvu kubwa zaidi.

Ili kutekeleza kampeni ya Saidia Mama Mjamzito ajifungue Salama, anasema taasisi ilifanya utafiti wa awali, na kubaini upungufu wa damu ni namba moja, ikifuatiwa na kifafa cha mimba, Aidha ni asilimia 50 tu ya wajawazito wanaorudi kujifungua katika vituo vya afya, upungufu wa mindombinu na maambukizi ya Kutoka kwa
mama kwenda kwa mtoto ni changamoto kwa uzazi salama. "Kupitia kampeni tunahamasisha wananchi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wajawazito wanaohitaji kwa dharura na kuhamasisha kina baba
kushiriki katika afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na kuwasindikiza kliniki ili kujua dalili za hatari wakati wa ujauzito na kujiandaa kujifungua.

"Kuongeza uwezo wa miundombinu katika utoaji huduma kwa mama wajawazito ambayo ni matumizi ya simu kufuatilia mama mwenye dalili za hatari kupitia rafiki kliniki mpaka anajifungua salama, kujenga wodi na vyumba vya dharura (ICU) na Upasuaji (Theatres) pamoja na kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,"anaongeza. Akielezea kuhusu tuzo, Dk. Kyaruzi anasema ya Rais Kikwete inatokana na jitihada mbalimbali, na wanatambua kwa kuipa kipaumbele sekta ya afya.

No comments: