Friday, November 22, 2013

SI KILA NDOA NI NDOANO, KUBALINI KUNA MAMBO MNAKOSEA!-2

Wiki iliyopita nilianza kuzungumzia mada hii, lengo ni kuhakikisha kila anayeingia kwenya ndoa anadumu na anapata furaha aliyoitarajia. Utakumbuka niliishia kuzungumzia kipengele cha kila mwanandoa kujitahidi kuwa mpole lakini si kuwa zoba. Nikasema kila mmoja ajitahidi kuwa mpole kwa mwenza wake, anyenyekee pale inapobidi lakini asiwe zoba wa kukubali kupelekeshwa katika jambo ambalo anaona wazi siyo sawa.

Wapo baadhi ya wanawake wanataka kuonekana wako juu ya waume zao. Yaani wanataka waonekane wao ndiyo wenye sauti ndani ya nyumba. Matokeo yake wasiambiwe jambo, wanakuja juu kama moto wa kifuu.

Kwenye mambo ambayo wanatakiwa kukubali, wanakuwa wabishi na kutaka katika kila jambo waonekane washindi. Hii ni mbaya sana! Kuwa mwanamke kwa maana halisi ya mwanamke. Mwanamke kamili ni yule mpole kwa mumewe, msikivu na asiye na ubishi wa kijinga.Lakini hili liwe hivyo hivyo kwa wanaume. Mwanaume kama unampenda mkeo, hutapenda kumkwaza, kwa maana hiyo utakuwa na lugha nzuri kwake, hata kama kakosea, utatumia lugha ya upole kumuelekeza na siyo kuwa mkali eti kwa sababu wewe ni mwanaume.Tukumbuke kila mmoja kuna wakati anakosea. Inapotokea umefanya kosa halafu unabisha kwamba hukufanya, ni hatari sana. Kama umefanya kubali kosa na omba msamaha.
Wazazi wetu wametufundisha kwamba kumbishia mtu aliyekuzidi umri ni dalili za kutokuwa na heshima. Hivyohivyo kwa wanandoa, unapombishia mwenza wako inadhihirisha humheshimu tabia ambayo inaweza kusababisha nyufa katika ndoa yenu.

Yapuuzie maneno ya watu
Maneno ya watu ndiyo yamekuwa yakibomoa ndoa nyingi. Hata hivyo sikushauri kwamba usiyasikilize kabisa yale unayoambiwa na watu, kuna mengine ambayo unaweza kuambiwa na watu yakawa ya maana sana katika maisha yenu.
Lakini sasa kuna maneno ambayo yanaonekana wazi yanalenga kuwaharibia ndoa yenu. Maneno ya umbeya! Wapo watakaokuja kukuambia mumeo/mkeo siku hizi anatoka na mtu fulani.

Maneno kama haya yanaweza kukuchoma sana lakini ni vyema ukayapokea na kuyafanyia kazi kabla ya kulipuka. Wapo watakaokuletea maneno ya uchochezi tu ili waone mnakorofishana, sasa akili kichwani mwako. 

Kabla ya kumalizia mada hii niseme kwamba kumekuwepo na malalamiko ya mara kwa kwa wanandoa ambao wote wanafanya kazi juu ya uaminifu.
Tunafahamu kwamba ikitokea bahati mkaoana wote mnafanya kazi, uvumilivu wa hali ya juu unahitajika, bila uvumilivu ndoa itavunjika. 

Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.
GPL

No comments: