ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 15, 2013

Stewart Hall aula rasmi Tanzania

Aliyekuwa Kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall

Aliyekuwa Kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall ameteuliwa kuwa Meneja wa Kituo cha Michezo na 'Akademi' ya Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam inayoanzishwa kwa ushirikiano wa Klabu ya Sunderland ya England, Kampuni ya Kufua Umeme ya Symbion Power na Serikali ya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Symbion Power Tanzania, uteuzi huo umefanywa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Peter Gathercole.

Hall, mwenye leseni ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) ya ukocha na mkufunzi wa shirikisho hilo, amepewa kazi hiyo baada ya mafanikio yake akiwa kocha wa Azam FC, timu ya Taifa ya Zanzibar na Birmingham City alipokuwa mkurugenzi wa akademi ya klabu hiyo ya Uingereza.

Kabla ya hapo, Hall, ambaye kwa makubaliano na uongozi wa Azam, Novemba 7, mwaka huu alisitisha mkataba wa kuinoa timu hiyo mara baada ya mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, alikuwa kocha wa timu za Taifa za Saint Vincent na Grenadines na Klabu ya Pune ya India.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Hall alisema: “Mradi huu hakika utasaidia kuinua soka la vijana kwa viwango vyote, timu za taifa na klabu. Vijana wadogo watafundishwa ufundi, mbinu na kupewa maarifa ya soka la kisasa.”

Ujenzi wa kituo hicho cha michezo cha kisasa ni matunda ya ziara ya Rais Jakaya Kikwete ‘JK’ katika Akademi ya Klabu ya Sunderland nchini Uingereza Juni mwaka huu ambako walifikia makubaliano na uongozi wa klabu hiyo na Kampuni ya Symbion Power Tanzania juu ya mradi huo.

Hall amefanikiwa kuiacha Azam ikiwa nafasi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kufikisha pointi 27 sawa na Mbeya City lakini kiwa juu kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mbali na hilo ameweka rekodi Azam kwa kuiwezesha kumaliza mzunguko wa kwanza bila kupoteza mchezo wowote kama ilivyo kwa Mbeya City ambayo huu ni msimu wake wa kwanza kushiriki ligi hiyo.

Kadhalika misimu miwili mfululizo iliyopita aliiwezesha kumaliza nafasi ya pili na hivyo kukata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho barani Afrika, Caf.

Hall pia aliipa Azam ubingwa wa Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Januari mwaka huu, ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya kuipa ubingwa wa michuano ya Kombe la Hisani nchini DR Congo.

Mbali na hayo, Hall pia amechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa Akademi ya Azam iliyopo Chamazi jijini Dar es Salaam. Pia ameiwezesha timu hiyo kutoa upinzani mkubwa kwa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga.

Katika mechi za msimu huu, Hall alikiwezesha kikosi chake kuichapa Yanga 3-2, huku kikiinyuka Simba 2-1.
CHANZO: NIPASHE

No comments: