ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 27, 2013

TFF yawazuia Kaseja, Dilunga kusajili Yanga

Kaimu Katibu Mkuu wa TFF,Boniface Wambura
Wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufungwa Desemba 15, mwaka huu, Shirikisho la Soka nchini(TFF), limezikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni na kuzingatia muda uliowekwa.

Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura alisema jana kuwa kitendo cha klabu kupeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine hakutoi nafasi ya kusajili mchezaji mpya.

Tamko hilo la TFF lina maana kwamba, Yanga ambayo kwa sasa tayari imeingia mikataba ya kuwasajili kipa Juma Kaseja aliyekuwa huru na kiungo Hassan Dilunga kutoka Ruvu Shooting, haitakubaliwa kumsajili mmoja wa wachezaji hao kwani tayari ilikuwa na wachezaji 29.

"Kama klabu ilisajili wachezaji 30 maana yake ni kuwa, haina nafasi ya kuongeza wachezaji. Kwa upande wa wachezaji wa kigeni (foreign players), tunakumbusha kuwa, kuanzia msimu ujao 2014/2015 watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa," alisema Wambura.

Alisema mpaka jana jioni hakuna klabu hata moja iliyokuwa imeshaingia kwenye mfumo wa TMS kuomba uhamisho wa mchezaji wa kigeni na itakapofika Desemba 15, mwaka huu mfumo huo wa TMS utafungwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: