
Ubora ni pamoja na kumpa mwenzako sababu ya kuwa na wewe tu na si mwingine. Yaani umfanye asione sababu ya kuwa na patna mwingine kwa sababu kila kitu anakipata kutoka kwako.
Kama mtakumbuka vizuri, wiki iliyopita tuliishia kwenye mfano wa jamaa aliyemdanganya mpenzi wake wakati wa kuanzisha uhusiano kuwa ana fedha na kazi nzuri.
Mwenzi wake alipohitaji vitu vya thamani, alimchenga!
Hebu jiulize; kama angekuwa mkweli kwa mwanamke wake, angesumbuliwa kiasi kile? Inawezekana yule mwanamke alikuwa na mapenzi ya kweli lakini kichwani alikuwa akijua kuwa mpenzi wake mambo safi...sasa alikuwa na kosa gani kutaka manunuzi ya gharama kubwa?
Hana kosa kwa sababu anajua jamaa yake anazo, kumbe ilikuwa longolongo. Tuendelee kujifunza.
KUBALI MAISHA YAKO
Itakuwa kichekesho kama utasema unampenda mpenzi wako wakati wewe hujipendi! Huwezi ukasema unamthamini mpenzi wako wakati thamani yako mwenyewe huitambui.
Kama unashindwa hata kuoga na kubadilisha nguo safi, nani atakayekupenda? Huwezi kuwa wa kisasa kama huzingatii usafi, jithamini. Mwingine anaweza kukuta anajichukia bila kujua. Unaweza ukamkuta mtu anajitoa kasoro. Siyo sawa. Jipe nafasi ya kwanza. Jiamini.
Acha kujitoa makosa. Jipe moyo, wewe ni mzuri kuliko mwingine. Kikubwa zaidi ni kwamba, utakuwa mzuri zaidi kwa yule anayekupenda tu. Ndiyo ukweli ulivyo marafiki zangu. Kujikubali ni silaha kubwa sana katika kuupa nguvu uhusiano wako na si uhusiano pekee, bali hata maisha kwa jumla.
UNAONEKANAJE?
Mwonekano wako unaweza kukuainisha jinsi ulivyo kwa wanaokutazama. Wakati mwingine inawezekana ukatafsirika tofauti na ulivyo kutokana na jinsi unavyovaa na tabia zako nyingine.
Lazima uwe kijana wa kisasa, kwa kuzingatia hilo unapaswa kuwa makini kwa kila kitu kinachoonekana kwa wanaokutazama. Jenga mazoea ya kutambua aina ya nguo na mahali ulipo, usivae nguo za ufukweni ofisini au nguo za mtaani ukavaa ofisini.
Wanaokuangalia wanapata taswira ya jinsi ulivyo kutokana na mavazi yako. Vaa nguo safi kila wakati, labda kama unafanya kazi ambayo inakulazimisha kuwa mchafu, ila baada ya hapo unapaswa kuwa msafi.
Kama huna mpenzi hii ni nafasi nzuri kwako, huenda uliumizwa na mpenzi wako aliyetangulia, jiweke katika mwonekano mzuri utakaowavutia wengine, huenda ukapata atakayekupenda.
Jiangalie vizuri ulikosea wapi katika uhusiano uliotangulia, huenda mwonekano wako ulimchukiza mpenzi wako bila wewe kufahamu hilo. Vaa nguo za heshima kila wakati ili uonekane unajitambua na mwenye kujiheshimu. Mavazi nayo yanazungumza!
Kama tayari una mpenzi, unapaswa kutumia nafasi hiyo vizuri sana, utakapovaa kisasa, nguo safi za kupendeza, hata utakapotembea na mpenzi wako, atajisikia huru kuwa na wewe na atajiona yupo na mpenzi makini unayemvutia yeye na wengine wanaokutazama.
UCHAGUZI WA MANUKATO
Unapozungumzia suala la mavazi, unatakiwa pia kuwa mwangalifu katika uchaguzi wa manukato. Lazima uwe mwangalifu kuchagua ‘perfume’ nzuri ambayo haitasumbua pua za mpenzi wako.
Kunukia vyema kutakufanya uwe rafiki wa kila mtu. Achana na manukato yenye harufu kali, kwa kawaida huwa yanakera. Pengine linaweza kuonekana jambo dogo au la kawaida tu lakini ni ukweli kwamba, wakati mwingine ukikosea katika manukato, huweza kusababisha kutoa harufu mbaya. Baadhi ya manukato, huwa yanaonekana kuwa na harufu nzuri, kali na ya kuvutia lakini baadaye jua likiwaka sawasawa, hubadilika na kuwa kero kwa wengine.
Vipi sasa kwa mwenzi wako? Nani atapenda kuwa na mtu anayetoa harufu mbaya. Hapa naomba nisisitize zaidi, si manukato pekee bali hata mafuta ya kawaida ya kupaka mwilini, baadhi huwa yanakera.
Wiki ijayo, nitamalizia mada hii, usikose!
GPL
No comments:
Post a Comment