Wednesday, November 20, 2013

UNATARAJIA KUINGIA KWENYE NDOA AU NDOANO?-2

KUJIFUNZA hakuna mwisho marafiki zangu...ndiyo sababu nipo hapa kwenye All About Love. Mada inayoendelea hapa ni juu ya kutambua mwenzi ambaye ni sahihi zaidi katika maisha ya ndoa.

Kama mtakumbuka, wiki iliyopita tuliona kuhusu mwenzi ambaye unatarajia kuwa naye kwenye ndoa kama ndiye yule uliyemtarajia kabla ya kukutana naye. Ni wa ndoto zako?
Ana sifa ulizokuwa ukitarajia? Maana unaweza kukurupukia ndoa ili na wewe uonekane tu umeolewa au umeoa, lakini akawa si chaguo lako la ndani.

Matokeo yake ni kwamba, ndoa itakuwa iliyojaa migogoro kila kukicha - ndoano. Hakutakuwa na amani na ni mwanzo wa mmoja wao kuwa msaliti. Hii ni kwa sababu mnakuwa mmeingia kwenye muunganiko usiyo sahihi. Muunganiko usiotarajiwa.

Kuna lingine tuliona; kasoro. Kila binadamu ana kasoro zake. Ukiwa makini kumchunguza mtu yeyote ambaye uko naye karibu ni rahisi sana kuona kasoro zake. Jambo kubwa na la msingi kwako kujiuliza ni kama kweli utaweza kuvumilia kasoro zake. Hebu sasa tuendelee na darasa letu.

MWENYE MAPENZI HASA
Sifa nyingine muhimu ya kumwangalia mwenzi anayefaa kuwa naye kwenye ndoa ni pamoja na yule mwenye mapenzi ya kweli hasa. Mapenzi ya kweli huonekana haraka sana. Penzi la dhati halijifichi. Hujitokeza hadharani, wakati mwingine bila hiyari.
Mwenye sifa hii ni msikivu (kwa wanaume na wanawake), muelewa na anayetoa kipaumbele kwa mwenzake. Kama anakupenda kwa dhati ni lazima akupe kipaumbele katika mambo yake.

Si msiri na hutoa nafasi kwa mwenzake kutoa mawazo yake katika mambo yanayomhusu. Hatua hii hutokana na namna anavyomuona mwenzake kama sehemu ya maisha yake.

DALILI ZA MPENZI ASIYEFAA
Unaweza kuwa na mpenzi na mkapanga mipango mbalimbali ya baadaye ikiwemo ndoa lakini akawa na kasoro kubwa zilizojificha. Wakati mwingine kasoro hizo unaweza kuziona lakini usijue kama ni kubwa na zinazoweza kuwa tatizo kubwa katika maisha yenu ya ndoa.

Mara nyingi kasoro za mwingine zinaweza kufichwa na mapenzi ya dhati yaliyopo ndani ya mtendwa. Mathalani wewe una mpenzi wako, kwa vile ndani yako kuna mapenzi ya dhati, mwenzako anaweza kuwa anakosea tena makosa makubwa sana, lakini ukajikuta unavumilia, kudharau au kupuuzia!
Zipo dalili nyingi za mpenzi asiyefaa, lakini hapa angalia zile za muhimu zaidi;

Usaliti; katika makosa makubwa kabisa kwenye uhusiano ni pamoja na kusaliti. Kama mwenzi wako anakusaliti na una ushahidi wa kutosha (kama umemfumania) ni dalili mbaya kwenye ndoa.
Kiburi/dharau; hii nayo ni dalili mbaya. Mwenzi mwenye dharau na kiburi hawezi kuwa sahihi, maana huko ndani ya nyumba kutakuwa ni majibizano yasiyo na maana. Mwenzi sahihi anapaswa kuwa msikivu, mwenye kupima kila kinachotoka kwenye ulimi wake.

Kipigo; tabia hii zaidi ipo kwa wanaume. Kosa dogo tu anamwangushia mwenzake kipigo. Kupigana si mapenzi marafiki zangu. Kama bado mpo kwenye uchumba tu, kosa dogo kipigo, vipi mkiingia kwenye ndoa? Tafakari jambo hili utaona ni kasoro kubwa sana.
Mbinafsi; hili ni tatizo lingine. Kama mnahitaji kuwa katika muunganiko wa ndoa, ubinafsi ni sumu kabisa. Mwenzi mwenye tabia ya lake linakuwa lake mwenyewe na lako lenu hafai kwenye ndoa.

Asiyejitoa; hili nalo ni tatizo. Unaweza kuwa na tatizo kubwa kabisa na kwa kulitazama unaamini kabisa kwamba mwenzako anaweza kukusaidia, lakini hataki tu. Mathalani unaumwa, anaweza kushindwa hata kufika kukujulia hali tu. Hata kama unampenda kwa kiwango gani, huyu hafai kabisa kuwa nawe kwenye ndoa.

WENGI WANASAHAU KUHUSU UMRI
Je, wewe una umri gani? Ni msichana mwenye zaidi ya umri wa miaka 20 au mvulana unayezidi miaka 23? Kama ndivyo, tunaweza kuendelea na mada hii. Najua kuna watu wananishangaa baada ya kuandika umri huo hapo juu.
Ni kweli umri unaotambulika kiserikali wa kijana kuingia kwenye ndoa ni kuanzia miaka 18 lakini msichana anaweza kuolewa hata akiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi wake.

Je, inamaana kwamba kijana mwenye miaka 18 hapaswi kuoa au kuolewa? La hasha. Sina maana hiyo. Ndugu zangu, wengi huingia kwenye ndoa na baadaye hugeuka majuto. Uwezo wa ubongo wa binadamu kufikiri umegawanyika katika makundi.
Kuna kipindi binadamu huwa na mawazo ya zimamoto. Anawaza kwa kuongozwa na hisia, lakini ubongo wake ukikua anabadilika. Ukweli ni kwamba, angalau msichana mwenye zaidi ya miaka 20 (hasa kuanzia miaka 22 hivi) angalau anaweza kuwa na uamuzi/uchaguzi sahihi wa nani awe mumewe.

Wavulana ndiyo kabisaaa! Hawa wanahitaji muda wa kutosha kufanya uamuzi wa nani awe mke wake wa ndoa. Wengi hujidanganya na hisia za machoni, lakini baadaye anakuja kugundua alifanya uchaguzi wa kimakosa.

Inaamika kuwa angalau kijana aliyefikisha miaka 25 na kuendelea ndiye mwenye uwezo (angalau) wa kufanya uchaguzi wa mke wa maisha yake. Kwa ambao hawana umri huu, wanaweza wasikubaliane na ukweli huu.
Darasa bado linaendelea, subira yako ni jambo la msingi zaidi rafiki yangu. Tafadhali tukutane tena wiki ijayo, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: