Sunday, November 24, 2013

ZITTO KABWE, DKT. KITILA MKUMBO WAFUNGUKA KUHUSU KUVULIWA MADARAKA CHADEMA


*Zitto Asema Hatoki Chadema, Dk. Kitila Akiri Kuandaa Waraka wa Siri.
 'Waliokuwa Naibu Katibu Katibu Mkuu  na Makamu Mwenyekiti' wa Chadema, Zitto Kabwe (kulia) akizungumza kwa hisia wakati alipokuwa akitoa tamko rasmi kuhusu 'maamuzi magumu', yaliyochukuliwa na chama chake kwa kuvuliwa madaraka ya ndani ya chama hicho kwa kile kilichoelezwa kuihujumu Chadema.
 Na Joachim Mushi, Dar
MBUNGE wa Chadema na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe amesema hawezi kufanya maamuzi magumu ya kutoka ndani ya chama hicho kwa kile kilichotokea ndani ya chama hicho. Amesema yeye atakuwa wa mwisho kutoka Chadema na si vinginevyo.

Zitto ameyatoa hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alipokuwa anazungumzia maamuzi ya Kamati Kuu ya Chadema ya kumvua nafasi zake zote za uongozi yeye pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Dk. Kitilla Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha Samson Mwigamba.

Zitto Kabwe na Kitila Mkumbo wakiingia Ukumbini katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, mchana huu kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Zitto amekana kuhusika wala kuujua waraka wa siri ambao ndiyo uliosababisha kumvua madaraka baada ya uamuzi wa Kamati Kuu ya chama kuunasa waraka huo.

"Mimi nimeusikia ule waraka kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu na nilisikitika sana kwanini hukunifikia haraka kwani ningeanza kutekeleza mara moja." alisema Zitto akizungumza.


Huenda leo watu walitegemea nitafanya maamuzi magumu ya kuondoka kwenye chama; "Mimi bado ni mwanachama wa Chadema na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiyari yangu, nitafanya taratibu zote za chama kuhitimisha jambo hili mimi sitoki kwenye chama hiki labda wanitoe wao," alisema Zitto.


Zitto alisema anaumia sana anapotuhumiwa kwa kuwa yeye ni binadamu. "...ninapotuhumiwa naumia ninapoambiwa naujumu chama hiki naumia kwa kuwa nakipenda chama na nimekitumikia muda mrefu. Aidha aliwataka viongozi wa Chadema kuacha siasa za uzushi ili kujenga chama himara na kuwakomboa Watanzania.

"...Sisemi kama mimi sina makosa ni binadamu nimefanya mambo mengi kwa chama changu, lakini kinachoendelea kwa sasa ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia na ni mapambano ya wanaotaka mabadiliko na wasiopenda mabadiliko ndani ya chama...mapambano ya wawajibikaji na wasiopenda kuwajibika ni mapambano ya wanaopenda demokrasia na wanaokwaza demokrasia." alisema Zitto huku akionesha kusikitishwa.
Zitto Kabwe (kulia) na Dk. Kitilla Mkumbo, wakisikiliza kwa makini maswali yaliyokuwa yakiulizwa na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.
 Umakini katika kusikiliza maswali.
Zitto Kabwe, akiagana na baadhi ya waandishi wa habari wakati akiondoka ukumbini.

VIDEO YA MKUTANO HUU NA TAMKO LA ZITTO NA KITILA ITAWAJIA PUNDE.

Picha na habari kwa hisani ya Sufiani Mafoto

No comments: