
Madiwani wa Chadema katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, hatimaye sasa ndiyo wengi katika Baraza la Madiwani na hivyo kuwa na nguvu ya kiuamuzi.
Kuongezeka kwa madiwani hawa, kumetokana na kuapishwa kwa diwani mpya wa viti maalumu, Magreth Olotu takriban miezi minne tangu kumalizika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne za Jiji la Arusha.
Katika uchaguzi huo, Chadema walifanikiwa kushinda kata zote, nne ambazo ni Kaloleni, Elerai, Kimandolu na Themi.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011, baada ya Chadema kuwatimua wanachama wake waliokuwa madiwani Estomih Mallah (Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles Mpanda (Kaloleni).
Ushindi wa madiwani hao wanne, ndiyo uliotoa nafasi kwa chama hicho kujiongezea kiti kimoja cha viti maalumu, huku bado uchaguzi wa kata moja ya Sombetini ukiwa haujafanyika. Uchaguzi huo utafanyika kutokana na aliyekuwa diwani, Alfonce Mawazo kujivua udiwani CCM na kujiunga Chadema.
Madiwani walioshinda ni Welance Kinabo Kata ya Themi, Katika Kata ya Elerai alishinda, Mhandisi Jeremiah Mpinga, Kata ya Kaloleni alishinda, Kessi Lewi na Katika Kata ya Kimandolu, alishinda Rayson Ngowi.
Mwenyekiti wa madiwani wa Chadema katika halmashauri ya Jiji, Isaya Doita anasema kwa sasa, chama hicho kina madiwani 15 kikifuatiwa na CCM chenye madiwani 14 na TLP diwani mmoja.
Anasema idadi hiyo ya madiwani, inajumuisha na wabunge watatu wa Chadema waliopo katika Jiji la Arusha na pia kwa CCM inajumuisha wabunge wao watatu.
Doita anasema Wabunge wa Chadema ambao wanashiriki baraza hilo, ni Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema na wabunge wa viti maalumu Grace Mukya na Rebecca Mngodo wakati CCM, ina wabunge Catherine Magige, Namelok Sokoine na Mary Chatanda.
Faida ya wingi wa madiwani ngazi ya Halmashauri
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Mkoa wa Arusha, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Levolosi Ephata Nanyaro, anasema, wingi wao sasa unatarajiwa kuleta mabadiliko katika utendaji ndani ya Jiji la Arusha.
Nanyaro anasema kuwa chama hicho, sasa kimefanikiwa kuongoza kamati mbalimbali za halmashauri na hivyo kuweza kusimamia miradi na mipango tofauti ya Jiji la Arusha.
“Sasa tunajipanga kuwa na mabadiliko makubwa katika na kuwa na msimamo wa pamoja katika uamuzi wetu ndani ya Jiji,” anasema Nanyaro.
Washinda nafasi ya Naibu Meya Arusha
Nanyaro anaeleza kuwa wingi wao, kwa mara ya kwanza ulifanikisha kuwezesha kuchaguliwa kwa diwani wa Chadema, Prosper Msofe kuwa Naibu Meya wa Jiji la Arusha, baada ya kuwabwaga madiwani wa CCM.
Katika uchaguzi huo, Msofe alichaguliwa baada ya kupata kura 28 huku CCM wakipiga kura tatu za kimpinga baada ya kushindwa kusimamisha mgombea.
Katika kikao hicho, Diwani Doita pia alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya Elimu, Afya na Uchumi.
Waanza kuwabana watendaji wabadhirifu
Kikao hicho cha kwanza kwa Chadema kuongoza, kilipitisha uamuzi wa kutoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Jiji, kutoa taarifa zilipo fedha taslimu kiasi cha Tsh8.5 milioni na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Tsh 6 milioni vilivyochangwa kwa ujenzi wa mahakama za Jiji.
Awali hoja hiyo, ilitolewa na Diwani Doita na kuungwa mkono na madiwani wote wa Chadema, ambaye alitaka kujua ziko wapi fedha na vifaa vya ujenzi walivyochangishwa wakazi wa jiji tangu mwaka 2004.
Licha ya Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Afwilile Lamsy kutoa maelezo kuwa fedha hizo, zilipotea kwenye akaunti na kuomba wapewe muda zaidi wa kuchunguza madiwani walipinga na kutoa siku 30 kupata taarifa kamili ya fedha na vifaa hivyo vilipo.
Wakielezea juu ya hoja hiyo, madiwani wa Chadema Kinabo na Mpinga walifafanua kuwa, kitendo cha wakazi wa Jiji la Arusha kuchangishwa fedha na baadaye fedha kupotea katika mazingira ya kutatanisha kinawakatisha tamaa kuchangia tena.
Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, anasema sasa umefika mwisho wa wabadhirifu katika halmashauri ya Jiji hilo.
Lema anasema lazima wote waliohusika kukusanya michango hiyo, wajulikane na waitwe kuhojiwa na waeleze zilipo fedha na vifaa vya ujenzi.
“Wingi wetu katika baraza hili nawahakikishia wakazi wa Jiji la Arusha, kuwa utakuwa na manufaa makubwa na kamwe hatutafanya kazi ya kumuonea mtu yoyote”anasema Lema.
Licha ya kurejeshwa fedha hizo, madiwani hao kwa wingi wao, pia walikubaliana kuwaita waliokuwa watendaji wa jiji, walioingia mkataba katika sekta ya afya ambao walieleza kuna upungufu mkubwa.
Diwani mteule asema vipaumbele vyake
Diwani Mteule wa viti maalumu, Magreth Ulotu anasema, moja ya mikakati yake ni kushirikiana na madiwani wenzake kuhakikisha jiji la Arusha halipati tena haiku chafu.
“Nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha jiji linapata hati safi kwa kupambana na ufisadi, pia tutahakikisha huduma muhimu ambazo zipo chini ya jiji zinatolewa kwa wananchi” anasema Olotu.
Ulotu anafafanua pia masuala ya kinamama na watoto, yatapewa kipaumbele katika halmashauri ya Jiji kwa kuhakikisha mikopo kwa akina mama na vijana inatolewa kama ambavyo serikali imekuwa ikiagiza.
Mussa Juma ni mwandishi wa gazeti la mwananchi mkoa wa Arusha na Manyara anapatikana Email Mussasiwa@gmail.com 0754296503.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment