.jpg)
Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Edward Lowassa.
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema juhudi za kusuluhisha mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania hadi sasa hazijafanikiwa licha ya Tanzania kutoa kiasi cha Dola za Marekani 387,336.96 sawa na asilimia 50.9 wakati Malawi imechangia Dola za Marekani 50,000 tu sawa na asilimia 6.6.
Akisoma taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa kipindi cha Machi hadi Novemba, 2013, bungeni jana kwa niaba ya mwenyekiti wake, Edward Lowassa, Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), alisema mgogoro huo kwa sasa upo kwenye Jukwaa la Marais wastaafu wa nchi za SADC kwa ajili ya usuluhishi.
Alisema ili kugharamia usuluhishi, kila nchi iliombwa ichangie Dola za Marekani 761,016.96.
“Uchambuzi zaidi wa kamati ulibaini kuwa Tanzania imechangia kiasi ambacho ni karibu mara nane ya kiasi cha mchango kilichotolewa na Malawi.
“Zaidi ya hivyo, nchi ya Malawi imeendelea kuonyesha nia yake ya kutaka kuharakisha kuwasilisha suala hili kaitka Mahakama ya Kimataifa,” alisema.
Alisema kamati ilijulishwa kuwa msimamo wa Tanzania ni kutoa muda wa kutosha na fedha za kukamilisha kazi ya msuluhishi.
Mtangamano wa Afrika Mashariki Alisema hali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inategemea kwa kiasi kikubwa uhusiano miongoni mwa Rwanda, Uganda, Kenya, Burundi na Tanzania.
Alisema kamati ilitaka kujua mambo mbalimbali kwa lengo la kujiridhisha kuhusu nafasi ya Tanzania katika jumuiya hii hususan, kuhusu mikutano ya utatu na athari yake na kubaini kuwa;
“Mikutano hiyo pamoja na mambo mengine imeamua kuwa nchi hizo ziendelee kutekeleza makubaliano yaliyopo katika ngazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika kutathmini, kamati imebaini kuwa makubaliano ya nchi hizo yanaathiri kwa kiasi kikubwa majadiliano kuhusu himaya moja ya forodha katika ngazi ya jumuiya.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Ha! taarifa inasomwa na mbunge wa Kondoa Kusini lakini inawekwa picha ya Lowassa. Upuuzi gani huu?
Post a Comment