Tisa Desemba ni siku ambayo Watanzania kote duniani wanapata fursa ya kujikumbushia juu ya Taifa lao lilipo tokea. Tanzania ni nchi ambayo ina mengi ya kuikumbuka, na kati ya hayo yapo mazuri na yapo mabaya, na kila watu huamua kulikumbuka taifa hili kwa utaratibu wao wenyewe, na kila mmoja anayo haki na huo utaratibu wake
Katika hali yoyote tutakavyo amua kulikumbukia taifa hili, lakini hatuna budi kukumbuka kwamba sisi ni kizazi muhimu sana katika historia ya nchi yetu hii. Inawezekana kabisa tushindwe kuliona hilo kwa leo au kwa kesho isipokuwa kwa kupitia mianya ya fikra na mifano hai ya mataifa mengine ya zamani.
Kizazi chetu ni kizazi kilicho changanyika na wengi walioshiriki katika kuuleta Uhuru wa taifa hili adhwim, Ima kwa kupigania au kuona ukipiganiwa. Katika matukio ya kukumbukwa, Kwa mfano; Mwanaharakati wa Uhuru Marehemu Kighoma Ali Malima. Aliwacha shule na kwenda kushiriki harakati za kupigania uhuru. Akimwambia mwalimu wake mkoloni wa kizungu, namnukuu “Nataka kusoma, lakini nataka kusoma hali ya kuwa nipo huru, hivyo nakwenda kushirikiana na wenzangu kupigania uhuru wa nchi yangu”. Haya ni maneno ya kishujaa na yasiyostahiki kusahaulika.
Umri wa uhuru wa taifa ni mdogo kuliko ya wengi wakazi wake. Pamoja na ugumu wa mazingira uliowachwa na watawala wake. Taifa hili lilijaa watu wasiojua kusoma wala kuandika, watu masikini wa kutupwa, lakini mazingira hayo haikutosha kulipelekea taifa hili kwenye janga wala kiza. Taifa hili likapigana na kusota, kujijenga na hata kufikia hapa tulipofika.
Pamoja na kwamba safari ndefu ipo mbele ya taifa hili, lakini kuweza kusimamisha mifumo Imara yailiyojengeka kwa misingi ya Amani na Utulivu, mifumo ya uchumi na biashara, mifumo ya uhuru wa kuabudu na demokrasia, mifumi ya elimu na mawasiliano, peke yake sio kazi ndogo. Pamoja na kuzungukwa na nchi zenye vita za kikabila na kidini, hazikuweza kutengua misingi imara ya umoja na ushirikiano iliyojengwa na wazee wetu.
Mungu alijaalie Taifa hili Amani na Upendo wa kudumu maisha. Alijaalie taifa hili liendelee kulinda na keshimu uhuru wa kuabudu na wa kifikra. Mungu alijaalie taifa hili liendelee kutoa vijana wenye siasa safi na wenye nia na nguvu ya kulijenga taifa hili. M/Mungu alijaalie taifa hili watu wake waendelee kujenga shauku na kulipenda taifa lao hili. M/Mungu ajaalie siasa za vyama vingi ziendelee na zikomae kwa faida ya wananchi. M/Mungu ajaalie kila mwenye kulihujumu taifa hili kwa kula rushwa au kwa misingi ya kisiasa basi mtu huyo apate ugonjwa wa kichaa.
MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE
No comments:
Post a Comment