Rais Jakaya Kikwete akiwasalimia maelfu ya watu waliojitokeza kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kwenye sherehe za kuazimisha miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania bara. Picha na Fidelis Felix
Dar es Salaam. Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewataka watanzania kuacha tabia ya kuwa na roho ya kulipiza visasi badala yake wawe watu wa kusamehe na kusahau kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuenzi moja kwa moja Rais mstaafu wa Afrika Kusini Marehemu Nelson Mandela.
Rais Kikwete ameyasema hayo mapema leo alipokuwa akiwa hutubia maelfu ya watu waliojitokeza kwenye sherehe za kutimiza miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania bara, sherehe zilizofanyika katika uwanja Taifa jijini Dar es Salaam jambo ambalo si kawaida yake kutoa hotuba
Rais Kikwete amesema mara baada ya Rais Mandela kutolewa gerezani hofu ilitawala Afrika ya Kusini, watu wengi wakitambua kuwa atakapochaguliwa kuwa Rais badala ya kuijenga nchi ataanza kulipiza visasi kwa wale wote waliotumika kwa namna moja ama nyingine kumtesa yeye na watu wa nchi yake.
“Badala yake Mzee Mandela alitoa tamko la kuwasamehe wote waliohusika kuwabagua watu wa Afrika ya Kusini, na kisha aliunda tume maalumu ya maridhiano ili kujenga umoja kati ya watu wenye ngozi nyeupe na wenye ngozi nyeusi, jambo hili ni la ajabu sana” amesema Kikwete.
“Hiki ni kipimo kikubwa cha ukomavu wa kisiasa, yatupasa watanzania na viongozi mbalimbali kuenzi jambo hili la kusameheana na kutokuwa walipiza visasi, hapa tulipo wengine wanasema kabisa nikichaguliwa watanikoma….. lakini nawasihi tumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga mambo mema aliyoyafanya ambayo hadi hivi leo yamechangia kukuza uchumi wa Afrika ya Kusini, “amesema Kikwete.
Amesema tokea enzi za TANU Tanzania imekuwa karibu sana na vyama vya ukombozi wa mataifa mengi Afrika, kikiwemo chama cha ANC ambacho kilikuwa kikiongozwa na Marehemu Mzee Mandela, hivyo aliwasihi watanzania waendeleze umoja huo .
“Kuna jambo moja ambalo hamlijui mwaka wa 1964 Mzee Mandela alikuja nchini na kufikia kwa mweka hazina wa TANU, Siro Swai, alikuwa akielekea kwenye mafunzo ya kijeshi Algeria, aliacha viatu vyake 'pea moja' akieleza kuwa atakaporudi atakuja kuvichukua lakini haikuwa hivyo, nilipokuwa waziri wa mambo ya nje, mke wa Swai alinifuata na kunieleza, nasi tulilazimika kuzirudisha kipindi hicho ambacho Mzee Mandela alikuwa Rais wa nchi hiyo tayari,” Anaeleza Kikwete.
Amesema haya yote yanatafsiri ukaribu na undugu wa hali ya juu kati ya nchi zetu mbili na ndiyo maana katika kumuenzi leo hii kwenye shughuli za kutimiza miaka 52 ya uhuru hatutakuwa na vikundi vya kutumbuiza.
Kwa habari Zaidi ungana nasi baadaye.
Ibada maalumu ya Mandela
Johannesburg. Afrika Kusini, jana ilitawaliwa na ibada na maombi yaliyofanyika katika makanisa mbalimbali kuliombea taifa, baada ya kifo cha Rais wa Kwanza mzalendo, Nelson Mandela.
Rais Jacob Zuma alikuwa miongoni mwa waumini wa Kanisa la Bryanston Methodist, Johannesburg katika ibada ambayo pia ilihudhuriwa na mtalaka wa Mandela, Winnie Madikizela pamoja na mjukuu mkubwa, Mandla.
Ibada za aina hiyo ziliendeshwa kila kona ya nchi, zikiwaweka pamoja Waafika Kusini ambao waliitikia wito wa Rais Zuma wa kuitumia Jumapili kuliombea taifa hilo.
Nyimbo za dini zilisikika katika kumbi za ibada na makanisa, ambako viongozi wa Serikali wakiwamo Naibu Rais wa Afrika Kusini, Kgalema Motlante na Rais Mstaafu, Thabo Mbeki walikuwa miongoni mwa waliopangiwa kushiriki katika ibada hizo.
Katika Kanisa la Baptist, baadhi ya waumini wakiwa katika mavazi rasmi walionekana wakiimba na kucheza, kabla ya Rais Zuma kupewa nafasi ya kuzungumza.
“Kwa nchi yetu, kifo cha Baba Madiba ni hasara ya aina yake. Waafrika Kusini tunapaswa kuomba tukikumbuka mambo mema ya kiukombozi na uhuru, amani, msamaha, haki na kujali ambayo Mandela aliyapigania na kuyasimamia,” alisema Zuma.
Kwa upande mwingine, mamia ya wafuasi wa Chama cha African National Congress (ANC), walifurika katika Ukumbi wa Benki ya Standard, Johannesburg kushiriki katika maombi, wakiitikia wito wa Rais Zuma.
Mwandishi wetu alishuhudia makada wa chama hicho wakiwa katika mavazi rasmi, wakicheza muziki wa Injili na baadaye wakishiriki maombi yaliyowahusisha waumini wa madhehebu ya Kikristo, Kiislamu, Kihindu, Kiyahudi, Bahai na wale wanaoamini katika imani za jadi.
Qunu kimya
Wakati nyimbo na ngoma zikichezwa kwa ajili ya kusifu kazi alizofanya Mandela, katika Kijiji alichokulia Qunu, eneo la Mthatha kuliripotiwa kuwa kimya huku wakazi wake wakikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu kifo cha Mandela.
Wanakijiji hao wameamua kukaa nyumbani wakiomboleza na inaaminika kwamba wengi hawaamini kilichotokea na pengine wanasubiri kushuhudia mwili wa kiongozi huyo utakapofikishwa huko Jumamosi kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumapili.
Hata hivyo, hali ni tofauti katika Kijiji cha Mvezo alikozaliwa Mandela, ambako tangu Ijumaa, wakazi wake wamekuwa wakiamka asubuhi na kushiriki katika ibada na maombi hadi adhuhuri, kisha kurejea tena jioni.
Kitukuu wa Mandela, Mambui alisema hali katika kijiji hicho kilichopo umbali wa Kilometa 25 tu kutoka Qunu ni ya huzuni na kwamba watu wake wamekuwa wakiomboleza kwa kulia machozi hasa wanapokuwa katika nyumba zao.
“Ni machozi ya huzuni na maumivu moyoni, siyo machozi ya furaha hata kidogo,” alisema Mambui alipokuwa akihojiwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Afrika Kusini (SABC), jana asubuhi.
Mwananchi
3 comments:
Maneno bila vitendo ni sawa na.........
Wadanganyika tomezoea propaganda nyingi.
Watanzania sisi ni wanafiki sana - tumuenzi Mandela vipi, Mandela alikuwa amekufa masikini maana hakuchukua hata senti tano ya wananchi wake. Hakuingia madarakani kula kama walivyo viongozi wetu.
Hakuna msamaha - tukichagua vizuri 2015, lazima waangalia jinsi viongozi walivyolumbikiza mabilion yetu, na washitakiwe na kufungwa.
Post a Comment