Mpenzi msomaji, leo tujikite katika eneo lingine kuhusu unyanyasaji wa watoto hasa unaofanywa na wazazi/walezi pasipo kuzingatia malezi bora ya mtoto wa kitanzania. Hebu tujadili ujumbe mfupi wa msomaji wetu kuhusu manyanyaso anayoshuhudia dhidi ya mtoto aliye jirani naye.
Ujumbe unaanza hivi: “ kwa jina naitwa Jerry(siyo jina halisi), naishi Mwanza wilaya ya Ilemela, kata ya Nyakato, Buzuruga. Kuna dada mmoja ameolewa na mbaba mmoja. Huyu dada ana watoto wawili wa kike.
Lakini pia baba huyu anaye mtoto mmoja wa kiume aliyemzaa nje(siyo mtoto wa huyo dada). Cha ajabu ni kwamba kila huyu baba anapotoka nyumbani tu, huyu mama anaanza kumnyanyasa huyo mtoto wa kiume bila sababu, kisa siyo wa kumzaa. Kwa kweli huyu dada amesahau kuwa mtoto wa mwenzio ni wako”, anamaliza ujumbe wake.Naam. Kwanza mpenzi msomaji nikukumbushe tafsiri ya maneno haya mwisho ya msomaji wetu hapo juu kama ambavyo imekuwa ikikaririwa na Mama Salma Kikwete, mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete kwenye mikutano inayohusu malezi ya mtoto wa kitanzania.
Mama Salma:“Tunaposema Mtoto wa Mwenzio ni mwanao tunamaanisha, sote tunapaswa kuwajibika kwa ajili ya ulinzi na ubora wa maisha ya watoto toka wakiwa tumboni hadi wanapozaliwa na kusimamia maadili yao wanapoendelea kukua.
“Watanzania wenzangu,tuache kulaumiana juu ya maadili ya vijana wetu,turejee malezi ya wazee wetu ili kila mmoja awajibike kumuona mtoto wa mwenzake kuwa ni wa kwake na kumrekebisha pale anapokosea.
Mpenzi msomaji, huo ndio utu ambao mzazi/mlezi anapaswa kuupeba kama kweli tumedhamiria kuinua makuzi bora ya watoto wetu popote walipo. Usibague mtoto wako na wa mwenzio kwani wote ni watoto na wanakutegemea kwa ulinzi kamili katika kila jambo.
Tumemsikia mama huyo toka kwenye ujumbe wa jerry hapo juu jinsi anavyomyanyasa mtoto ambaye mumewe alimzaa nje kisha kumleta ndani ya familia ili amlee. Mume huyu kila anapoondoka huamini kuwa watoto wake wanaishi vizuri bila manyanyaso lakini kumbe yule aliyemleta anapata suluba vibaya sana.
Je, mama huyu anao utu katika kuwalea watoto hawa kwa kuwapa haki sawa ya malezi? Pengine mtoto huyu ni mpole siyo mtundu na huko alikokuwa kwa mamake pengine baba aliona amchukue baada ya kuona mamake hajatulia na kadhalika.
Lakini pia inawezekana mama huyu aliyeletewa mtoto wa nje amegundua kuwa anazo tabia ambazo siyo nzuri kama vile udokozi na nyinginezo hivyo badala ya kumsaidia kwa kumrekebisha ili aendane na maadili mema anayofundisha wanae, anamnyanyasa.
Mama huyu anashindwa kuelewa kwamba kwa kumnyanyasa mtoto huyu huku akiona wenzake wanalindwa na kupendelewa, anamjengea mazingira hatari zaidi ya kufanya vitendo vya kikatili kama anavyofanyiwa.
Watoto wengine ambao wananyanyaswa huwa wanatishiwa na mama zao walezi kwamba wakimwambia baba watapata kibano zaidi hivyo kuwa waoga. Hii siyo sawa kabisa.
Wapo baadhi ya kinababa pindi wanapoleta watoto wa nje ya ndoa, huhakikisha kuwa kila baya wanaloambiwa kuhusu mtoto aliyeletwa nje hawakubaliani nalo. Huhisi kuwa mama mlezi hampendi ndio maana anamzushia mambo ili pengine amrejeshe huko alikokuwa.
Wapo kinamama waliojikuta katika mazingira magumu pale wanaponyanyasa mtoto aliyeletwa kutoka nje ya ndoa. Nakumbuka kisa cha mama mmoja rafiki yangu aliyeletewa mtoto wa nje wa kiume miaka 9 ambaye alikuwa ameshindikana huko kwa mamake ili aje amlee.
Mumewe alikuwa kila akiondoka asubuhi hurejea saa tano za usiku hivyo alikuwa haijui vema tabia ya mwanae. Mama huyu yeye alikuwa na mtoto mmoja. Mtoto huyo wa nje akaanza tabia ya udokozi wa chakula au hata hela, uwongo. Kila alipojaribu kumwambia baba yake hakukubaliana na shutuma hizo.
Mwishoni baba akamwambia mkewe kwamba kama anataka amtoe huyo mtoto hapo nyumbani ni bora hata yeye(baba) aondoke. Ilifikia wazi anambagua mwanae wa kike pale anaponunua nguo anamwacha.
Hata hivyo, baada ya kuomba ushauri, aliambiwa awe mvumilivu lakini pia ikiwezekana aombe kiitishwe kikao cha familia pande zote mbili ili suluhisho lipatikane.
Mpenzi msomaji, matatizo kama haya na mengine ndiyo yaliyosababisha serikali yetu kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuanzisha Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania. Sera hii Toleo la Pili la Machi 2008, imeainisha mambo mengi kuhusu ukatili dhidi ya mtoto.
Katika sura ya tano Hoja na Matamko ya Sera, kifungu cha 53 Hoja:ukatili dhidi ya watoto kinasema; Wapo watoto hapa nchini wanaofanyiwa vitendo viovu ambavyo ni pamoja na kutelekezwa, kutupwa, kupigwa, kuchomwa moto, kubakwa, kukeketwa, kutumiwa katika ukahaba, kuuzwa na kusafirishwa ndani na nje ya nchi.
Watoto wanaofanyiwa vitendo huathirika kimwili, kiafya, kiakili, kisaikolojia na ukuaji wao. Kwa mantiki hiyo, sera aiatamka kwamba serikali kwa kushirikiana na jamii na wadau wengine wa masuala ya watoto, iandae mikakati na program zinazolenga kuwalinda na kuwatunza watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.
Aidha serikali iweke utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki ya kulindwa kwa watoto. Serikali kwa kushirikiana na wadau ielimishe na kuhamasisha jamii kuacha ukeketaji wa wananwake na watoto wa kike pamoja na mila zingine zenye madhara.
Pia serikali ielimishe wazazi na jamii kuwa jukumu la kuwalea watoto wao hawa walio chini ya miaka minane ni lao na lisiachiwe watu wengine kama vile mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisis na sghule za bweni zilizo ndani na nje ya nchi.
Katika kifungu za 54 Hoja: Unyanyasaji na udhalilishaji wa watoto. Katika jamii zetu watoto wananyanyaswa na kudhalilishwa kwa kutolewa lugha chafu, kutukanwa, kuvuliwa nguo wakati wa kupewa adhabu kutumwa kufanya mambo yasiyostahili kulingana na umri, kubaguliwa na kusukumwa kwenye mabasi hasa katika maeneo ya mijini na kunyimwa chakula. Halin hiyo inawaathiri watoto kiafya na kisaikolojia.
Mpenzi msomaji, niliona ni muhimu sana nikumegee sehemu muhimu za sera hii kuhusu unyanyasaji wa watoto wetu, jambo ambalo limewaathiri sana katika makuzi yao badala ya kuwajengea uwezo kimaadili kwa maendeleo yao, wengi wao wakazidi kuzama kuwa manunda(watukutu), hivyo kulivuruga taifa tarajiwa la baadaye.
Mpenzi msomaji, ujumbe niliowasilisha awali toka kwa msomaji wetu wa Ilemela, Mwanza unapatiwa majibu ndani ya vifungu vya sera hapo juu.
Unyanyasaji anaofanya mama huyo kisa eti siyo mwanae haukubaliki kama ambavyo serikali imesisitiza ndani ya sera ya maendeleo ya mtoto Tanzania. Kwa leo nikomee hapa na kama unao mchango wa maoni kuhusu wazazi/walezi wanaonyanyasa watoto wa wanawake wenzao, jiachie kupitia anwani hapo chini.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment