ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 14, 2013

Uchumi unapoendelea kuimarika milioni 4.2 wapo taabani

Naibu Mtendaji mkuu, Ofisi ya Rais anayeshughulikia majanga, Peniel Lyimo.

Wakati serikali imesema inaweka usawa katika mgawanyo wa utajiri wa rasilimali za nchi, watu milioni 4.2 wanaishi katika hali ya umasikini wa kupindukia.

Katika ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia na kusomwa na Jacquesset Moriseet ambaye ni mchumi Mkuu wa benki hiyo kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi, watu hao maisha yao yanategemea kuchukua maamuzi magumu kwa watoto wao ikiwamo kuendelea na masomo au kuachishwa ili kuzitunza familia zao.

Hata hivyo, Moriset alisema uchumi wa Tanzania unaendelea kukua na kufikia asilimia 7 kwa mwaka huu hadi 2014, ambapo sekta zinazoongoza kwa kuongeza kasi ya uchumi ni mawasiliano, uchukuzi, ujenzi na biashara rejareja.


Ripoti hiyo inahimiza kuongeza juhudi katika kilimo na kuongeza ajira nje ya sekta hiyo.

"Pamoja na hali hiyo, bado haitoshi kumfanya mtu aondoke kwenye umasikini, uzoefu unaonyesha hata kama uzalishaji wa kilimo utaongezeka, familia masikini huachwa nyuma," alisema Morisset.

Aidha, Benki ya Dunia imesifu mpango wa uhamishaji wa pesa kwenda katika familia masikini unaoendeshwa na Mfuko wa TASAF, kwa kuonyesha matokeo mazuri katika kushughulikia mahitaji kwenye kaya masikini.

Kulingana na mpango huo, kaya masikini zinawezeshwa kwa kupewa pesa kidogo kila mwezi kwa ajili ya kununua mahitaji muhimu pamoja na kuwahudumia shuleni.

Kwa upande wa Naibu Mtendaji mkuu, Ofisi ya Rais anayeshughulikia majanga, Peniel Lyimo, alisema serikali inajitahidi kuweka mgawanyo ulio sawa katika mapato yatokanayo na rasilimali ili kila sehemu ya nchi kunufaika.

Alisema, utajiri wa rasilimali asilia ikiwamo gesi na madini, utaweza kunufaisha Watanzania, endapo kutakuwa na ongezeko la wawekezaji watakaoweza kubadilisha rasilimali hizo kuwa bidhaa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: