ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 6, 2013

UCHUNGUZI KUHUSU JARIBIO OVU LA KUCHOMA MOTO OFISI ZA CHADEMA ARUSHA

Tarehe 3/12/2013 jaribio baya lilifanyika dhidi ya kuchoma ofisi ya CHADEMA ya Kanda ya Kaskazini na Mkoa wa Arusha .
Hata hivyo Jeshi la Polisi lilifika kwa ajili ya uchunguzi wa awali na Chama kilielekeza Kitengo chake cha Usalama na Ulinzi kuanza kufuatilia jambo hilo kwa kina ili kubaini wahalifu wa jaribio hilo baya . Taarifa ambazo tumepokea mpaka sasa ni taarifa muhimu ambazo tunaamini zitaisadia Jeshi la Polisi katika uchunguzi wake.
Tumepeleka majina ya Watu ambao taarifa zetu za kina zinaonyesha wanahusika na tukio hili takribani wasiozidi watano na ni imani yetu kuwa Jeshi la Polisi litachukuwa hatua muhimu katika uchunguzi wao huku Chama tukiwa tiyari kabisa kutoa ushirikiano wa dhati katika uchunguzi wa kina na wakitaalaamu ambao utaweza kuthibitisha udadisi wetu na uchunguzi wetu ili kuponya Taifa letu .

Hata hivyo Chadema kinalitaka Jeshi la Polisi kutokufanya Siasa katika jambo hili kwani ni muhimu wakaelewa kwamba kupuuza uchunguzi wa jambo hili ni hatari kwa Mkoa wa Arusha na mustakabali wa Amani ya Taifa letu . Chama katika utafiti wake kimebaini kuwa miongoni mwa washukiwa katika tukio hili wamekuwa ni Vijana ambao wamekuwa wakifanya kazi na Polisi katika jitihada za kuhujumu Chadema na hivyo kunaleta mashaka makubwa juu ya uchunguzi wa jambo hili kama utafanyika kwa ufasaha na weledi wa hali ya juu kwa majina ambayo Chama imemkabidhi Kamanda wa Polisi Mkoa .
Hata hivyo katika uchunguzi wake Chadema inasikitishwa sana na kitendo cha Serikali kumpatia mmoja wa washukiwa umiliki wa silaha aina ya bastola wakati Mtu huyo akiwa na rekodi ya kuwa na kichaa cha mara kwa mara .
Chadema Kanda ya Kaskazini inawataka Wanachama wake na wafuasi watulie kimya bila kutafakari aina yeyote ya kisasi kwa jaribu hili baya ili kutoa fursa njema kwa Viongozi wao na Jeshi la Polisi ili kuwabaini Watu hawa waliotaka kuteketeza Ofisi ya Chama kwa moto . Lakini pia Chadema inamshukuru sana na kumpongeza mmiliki wa nyumba hiyo kwa kutambua majaribu ambayo tumepitia wakati huu kwa kukubali kurekebisha nyumba ambayo ni ofisi yetu kwa gharama zake mwenyewe kama sehemu ya kuheshimu jitihada za kushinda hofu na woga unaotaka kupandikizwa miongoni mwa jamii yetu .

NANYARO E.J.
Mwenyekiti Wilaya
4/12/2013

No comments: