ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 8, 2014

Chuji aenguliwa safari ya Uturuki, Mkwasa apangua kikosi Yanga


Athuman Iddi Chuji
Kikosi cha Yanga kikiwa mazoezini Tanganyika Packers jana

Yanga itaondoka na nyota wake wote kwenda kujifua nchini Uturuki isipokuwa kiungo mkabaji, Athumani Idd 'Chuji' aliyesimamishwa kwa utovu wa nidhamu.

Kesho Yanga inatarajia kwenda Uturuki kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Taarifa zilizolifikia NIPASHE jana dakika chache kabla ya kwenda mitamboni, kutoka chanzo chetu ndani ya klabu hiyo, zilieleza kuwa Chuji hataongozana na timu hiyo.
"Tutaondoka na wachezaji wote isipokuwa Chuji, ila subirini kidogo tutawatangazia rasmi kesho," kilieleza.

Yanga kwa sasa inaendelea na mazoezi kwenye viwanja vya Tanganyika Packers kabla ya kesho kupaa Uturuki.

Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alililiambia NIPASHE jana kuwa upinzani umekuwa mkubwa kwenye mazoezi hayo jambo ambalo anaamini litamsaidia kupata kikosi bora.

Mkwasa alisema hana wasi wasi na kikosi chake kwa kuwa wachezaji wote wapo na wanaendelea na mazoezi na kwamba safari ya Uturuki itawasaidia kujiweka fiti zaidi.

Wakati huo huo Kocha wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Boniface Mkwasa, amesema kamwe hatapanga timu kwa kuangalia jina la mchezaji na badala yake atazingatia kiwango na uwezo halisi wa kila nyota ili kuwapo kwenye kikosi cha kwanza na kwamba atatoa nafasi zaidi kwa yosso.

Mkwasa amechukua mikoba ya Ernie Brandts kukiongoza kikosi hicho ambacho kinatetea ubingwa wa Tanzania Bara na pia kitapeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwezi ujao.

Akizungumza na NIPASHE jana katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, Mkwasa, alisema uwezo na juhudi binafsi za kila mchezaji ndiyo silaha ya kupata namba katika timu hiyo.

Mkwasa alisema kuwa kila mchezaji anatakiwa afahamu umuhimu wake na wajibu wake katika timu ndipo mafanikio yatapatikana na hatimaye kutetea ubingwa wao.

"Hakuna kocha atakayekuwa tayari kuona timu yake inafanya vibaya au inapoteza mchezo, nitaangalia nani yuko vizuri na ataisaidiaje timu kwa wakati huo," alisema Mkwasa.

Aliongeza kuwa, anafurahishwa na ushindani kwenye mazoezi ya timu hiyo kwa sasa kwa sababu kila mmoja anataka kuwapo katika kikosi cha kwanza.

Alisema yuko tayari kukabiliana na ushindani kwenye Ligi ya Bara na hana hofu kwa sababu anazifahamu timu zote zinazoshiriki ligi inayoshirikisha timu 14.

SAFARI YA UTURUKI
Mkwasa alisema amefurahia timu yake kupata safari hiyo ya kuelekea Uturuki kwa ajili ya kujiandaa na hatua ya lala salama ya ligi na mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Kocha huyo wa zamani wa Ruvu Shooting alisema ziara hiyo haitawaathiri wachezaji wake na itawafanya wawe imara kwa kukabiliana na changamoto kwenye mechi za ligi zinazotarajiwa kuanza Januari 25, mwaka huu.
"Ziara hiyo haitatusumbua kwa sababu tunaenda kwenye baridi, kama ingekuwa kuna joto kali ndiyo ingetusumbua na kutuathiri, tukirudi tutakuwa tumeiva na mapafu kuwa na nguvu," alieleza Mkwasa.

Aliongeza kuwa, ziara yoyote ya nje ya nchi husaidia kuimarisha timu na kuwaongezea wachezaji uzoefu.

"Kambi yoyote hulenga kuimarisha timu, itatusaidia na itajenga kikosi," aliongeza.
Hata hivyo, Mkwasa alishindwa kuweka wazi ni nyota gani watakwenda Uturuki na watacheza mechi ngapi za kirafiki kutokana na kutopewa taarifa rasmi za safari hiyo.

YOSSO WATACHEZA
Kocha huyo ambaye yuko katika Kamati ya vijana ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) alisema kuwa atatoa nafasi kwa wachezaji yosso katika timu hiyo.

Mkwasa alisema kwamba hataacha kuwatumia wachezaji vijana kama alivyokuwa akifanya Ruvu Shooting kwa sababu ndiyo msingi wa timu na kutoa nafasi kwa yosso hao kutawapa uzoefu na hatimaye kusaidia kupatikana kwa ushindi.

"Mimi ni mtu wa vijana, nitawapa nafasi kila watakapoonyesha uwezo na wako tayari, nitaanza kuwapa dakika 15 au 20, watakachokionyesha ndiyo kitanipa picha ya kuwapa muda zaidi," alisema Mkwasa.

Alisema anafurahia kuona nusu ya wachezaji walioko Yanga walipita katika timu ya Taifa ya Vijana.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: