Rais Jakaya Kikwete akiangalia moja ya nyumba zilizobomolewa na mvua iliyosababisha mafuriko wiki iliyopita katika Kijiji cha Mateteni, Dakawa, wilayani Kilosa alipotembelea maeneo hayo jana. Picha na Juma Mtanda
Morogoro. Rais Jakaya Kikwete ameikataa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kuhusu waathirika wa mafuriko na waliokosa makazi na kumpa siku moja kukaa na timu yake kuandaa nyingine inayoendana na hali halisi ya janga hilo.
Eneo la Dumila, Morogoro lilikumbwa na mafuriko makubwa na kusababisha wakazi wake kupoteza makazi na mali huku mamia ya magari yakiwamo mabasi yanayosafirisha abiria kukwama baada ya kubomoka kwa Daraja la Magole linalounganisha Barabara ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mvua hizo zilizonyesha kwenye Wilaya ya Kilosa, ndizo zilisababisha kufurika kwa Mto Mkundi unaopita kwenye eneo hilo.
Taarifa ya Bendera
Bendera alitoa taarifa ya mafuriko kwa Rais Kikwete kwa niaba ya viongozi wa mkoa, wakiwamo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa taasisi mbalimbali akisema wananchi 12,472 wamepoteza makazi. Alisema pia kuwa nyumba 1,141 zilibomoka na 2,551 ziliingiliwa na maji huku kaya 2,759 zikiathiriwa na mafuriko. Bendera alisema misaada ya mahema na vyakula imeanza kutolewa pamoja na dawa za kukabiliana milipuko ya magonjwa endapo itatokea.
Alisema pia kuwa tayari baadhi ya miundombinu imeanza kurejea kama kawaida huku huduma za majisafi zikitolewa na magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha Zimamoto Morogoro na Kampuni ya China ya High Quality Consulting and Development Solutions. Bendera alisema pia kuwa jumla ya Sh53.7milioni zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya muda ya waathirika hao.
JK aikataa taarifa
Rais Kikwete aliyekuwa akikatizakatiza taarifa hiyo ya Bendera kwa maswali na ufafanuzi, alizikataa takwimu hizo akisema hazionyeshi uhalisia. Akizungumza na wananchi wa eneo hilo wakiwamo waliokuwa kwenye kambi iliyoko Sekondari ya Magole, Rais Kikwete aliwahakikishia upatikanaji wa vyakula, dawa na majisafi na salama.
Pia aliviagiza viwanda vya magodoro kuzisaidia haraka iwezekanavyo, familia zilizoathirika na kuahidi kuwa Serikali italipa baadaye ili kuwaepusha wakazi hao na hasa watoto na athari za kiafya.
Alisema kazi ya ujenzi wa makazi ya muda itafanywa JWTZ na si makandarasi kuepusha baadhi ya viongozi kujinufaisha kwa mafuriko hayo. Rais Kikwete aliwataka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuangalia uwezekano wa kutoa magogo yaliyoziba katika makaravati na kuzibua mifereji ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi.
Akizungumzia ripoti hiyo Rais Kikwete alisema: “Mmeshindwa kufafanua watu walioathiriwa na mafuriko hayo ni wangapi na wanasaidiwa vipi hasa katika mahitaji mbalimbali na muhimu ya kimsingi kama chakula.
“Taarifa yenu inanitia shaka. Sasa ninawataka viongozi wa mkoa pamoja na Mkuu wa Mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote wa halmashauri kurudia upya kumbukumbu zenu na kupata idadi kamili ya waathirika ili kujua namna ya kuwasaidia. “Ninyi kama viongozi na mnashughulikia maisha ya watu, mnatakiwa kuwa na kumbukumbu zenye usahihi wa majina na kama hamna uhakika wa majina mnaomba vyakula kwa ajili ya nani? Misaada mingine kwa wahisani ya nini?
“Tunataka tujue wanasaidiwaje, kina mama ni wangapi na kina baba, watoto, tutoe misaada kadri inavyostahiki. Sasa kwa takwimu hizi mnafahamu hawa watu wako wapi? Tutawasaidiaje? Wameathirika kwa kiasi gani?.” Rais Kikwete alisema kiongozi mzuri hupimwa wakati wa kipindi cha matukio na matatizo au majanga yanapotokea. Aliwataka viongozi hao kujipanga kwa kuwatambua watu walioathiriwa na mafuriko kwa kuwa na majina sahihi na idadi yao.
Miundombinu
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Injinia Doroth Mtenga alisema ofisi yake itatumia kiasi cha Sh400 milioni kukamilisha matengenezo ya eneo la tuta la Daraja la Magole katika Mto Mkundi lililozolewa na maji na kusababisha mafuriko makubwa.
Fedha hizo zitatumika kurekebishia makaravati na madaraja mengine madogo katika eneo hilo kutoka Wami Dakawa hadi Daraja la Mkundi, Magole ambayo huathiriwa mara kwa mara pindi mto huo unapojaa. Mtenga alisema kuwa ujenzi huo unakusudiwa kukamilika ndani ya wiki ya kwanza ya Februari na kama hali ya hewa itaendelea kuwa nzuri, ukarabati huo unatarajiwa kuendelea na kukamilika taratibu na magari yataweza kupishana kama ilivyokuwa awali.
Wakati hayo yakifanyika, mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wameanza kazi ya kurudishia nguzo na nyaya za umeme zilizoharibiwa na mafuriko hayo huku wataalamu wa Kampuni ya Matrac Telecom, wakirekebisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenda Mkoa wa Dodoma ambao pia uliharibiwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani amekabidhi kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro vifaa tiba, magodoro 100 na dawa mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh80 milioni.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment