Advertisements

Monday, January 20, 2014

Kapombe aziita Yanga, Azam

Shomary Kapombe
Beki wa zamani wa Simba ya jijini Dar es Salaam, Shomary Kapombe, amesema yeye sasa ni mchezaji huru na yuko tayari kufanya mazungumzo na klabu yoyote ya ndani na nje ya nchi ambayo itahitaji huduma yake.

Kapombe ambaye kwa sasa yuko hapa nchini, alikuwa akilelewa kisoka Ufaransa katika Klabu ya AS Cannes akiichezea kwa mkopo kwa lengo la kutumia nafasi hiyo kupata uzoefu wa ligi ya nchi hiyo kabla ya kutafutiwa soko.

Simba ilimtoa beki huyo na kumpeleka Ufaransa kupitia wakala wa mchezaji huyo.
Akizungumza juzi jijini, Kapombe, alisema baada ya Klabu ya AS Cannes kusitisha malipo yake ya mshahara na posho, aliamua kuikacha na kutorejea huko kuendelea na timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili.

Kapombe alisema bado ndoto zake za kucheza Ulaya hazijapotea lakini ataangalia maslahi kwanza endapo atapata timu yoyote ya kuichezea hapa nchini. "Mimi niko huru, nilikuwa kwetu Morogoro mzima wala siumwi," alisema beki huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) juzi mara baada ya mechi ya kirafiki kati ya Simba na Mtibwa Sugar iliyochezwa Uwanja wa Taifa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa Kapombe ni mali ya wakala na wakala huyo ndiye anawajibika kwa matatizo yoyote yatakayomkuta mchezaji huyo.

Hanspope alisema wao walichokubaliana na wakala huyo ambaye ni raia wa Ufaransa ni kuhakikisha Kapombe anapata timu ya kucheza huko Ulaya itakayomlipa vizuri na endapo atauzwa rasmi, klabu hiyo ya Msimbazi itapokea malipo ya asilimia 40. Tayari habari ambazo viongozi wa Yanga na Azam wamekataa kuthibitisha ni kwamba wanamhitaji beki huyo ambaye anacheza zaidi ya namba tatu uwanjani.

Mwaka jana Simba ilishuhudia mshambuliaji wake raia wa Uganda, Emmanuel Okwi, akijiunga na wapinzani wao Yanga kiulaini huku wao wakiendelea kuidai timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia Dola za Marekani 300,000.

Kama ilivyokuwa kwa Okwi, Kapombe kabla ya kuondoka alikuwa na mkataba na Simba hivyo klabu hiyo ilihitajika kulipwa kabla ya nyota huyo kuingia mkataba na klabu hiyo ya Ufaransa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: