ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 20, 2014

MGOGORO WA SUDAN YA KUSINI UNATISHA -BAN KI MOON

Wawakilishi wa Kudumu kutoka nchi 193 wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon wakati alipolizungumza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa. Alitumia fursa hiyo, kuainisha vipaumbele vyake vya mwaka 2014, mafanikio na changamoto zinazoukabili Umoja wa Mataifa ikiwamo migogoro inayoendelea huko Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati na kwingineko Duniani. Akatahadharisha kwamba kama Jumuiya ya Kimataifa haitakuwa makini kuna hatari kubwa ya kutokea mauaji makubwa ya raia kama ambavyo imeshawahi kutokea huko nyuma.

Na  Mwandishi Maalum
Kufuatia   machafuko na  migogoro inayoendelea katika nchi za  Sudani ya Kusini,  Afrika  ya  Kati , Mali na maeneo mengine  duniani,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwa makini na kuchukua  tahadhari ya  juu.
Amesema  kuna ukiukwaji mkubwa  wa haki  za binadamu katika maeneo hayo jambo analosema hali ikiendelea kama ilivyo sasa kuna  hatari kubwa ya kutokea mauaji makubwa ya raia kama ambavyo  dunia imeshuhudia  katika miaka iliyopita.
 Ban   Ki Moon, ametoa tahadhari hiyo, mwishoni mwa wiki, wakati alipolizunguza  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa  .  Ambapo  alitumia fursa hiyo kuainisha  malengo  na vipaumbele vyake na Umoja wa Mataifa kwa ujumla kwa mwaka huu wa 2014.
“Kuna mambo ambayo tunapashwa kuwa   makini nayo na kuchukua tahadhari kubwa,  mgogoro unaoendelea  katika Sudan ya Kusini  umefikia  kuwango cha kutisha. Kuna  ukiukwaji  mkubwa wa haki za binadamu “ akasema Ban Ki Moon

Na kuongeza kwamba kufuatia  mgogoro huo   Umoja wa Mataifa  ulifungua  milango ya Kambi ya Kulinda Amani katika Sudan ya Kusini ( UNMISS) na kuwahifadhi maelfu ya raia waliokuwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha yao.
“ Wengi wao leo hii wako hai ni kwasababu tu, waliwahi kukimbia kwa wakati na  kufika kwenye  makambi yetu. Tunajitahidi kadri tuwezavyo pamoja na uwezo wetu mdogo kuwa hudumia, lakini hali ni mbaya na mazingira ni ya kutisha” akasisitiza.
Pamoja na kuendelea  na  jukumu la utoaji wa misaada kwa raia ambao wameyakimbia  makazi yao, Mkuu huyo wa Umoja wa mataifa anaeleza kwamba, jitihada za kutafutu suluhu ya kisiasa kwa mgogogo huo  inaendelea.
Akatumia fursa hiyo kuwashukuru  viongozi wa nchi za IGAD ( Intergovernmental Authority for Development ) na  Umoja wa Afrika ( AU) kwa  juhudi zao za kusimamia mazungumzo ya kutafuta   suluhu.
Aidha  katibu Mkuu amezitaka pande  zinazohusika kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazugumzo na kuonya kwamba Ofisi ya Kamishna  ya Haki za Bindamu inafuatilia kwa karibu sana kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu  katika  nchi hiyo .
Kwa upande wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,  Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa,  ameelezea wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa mambo  unavyoendelea yakiwamo mauaji holela ya raia.
Akazishukuru nchi zinazounda Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika ya Kati ( ECCAS) pamoja na Ufarasa kwa juhudi zao  za kuwasaidia raia wa  nchi hiyo pamoja na kurejesha hali ya amani na utulivu. Nakuonya kwamba wale wote wanaouhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu lazima watawajibishwa.
Kuhusu  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC)  Katibu Mkuu ameeleza kuwa  uwepo wa Brigedi Maalum ( FIB) katika eneo la Mashariki ya Nchi hiyo,  kumesaidia sana katika  kuweka sawa mambo ikiwa ni pamoja na kupunguza  kujirudia kwa machafuko ya mara kwa mara.
Akasisitiza kwamba     Jumuiya ya Kimataifa inapashwa  kutumia hali ya utulivu iliyopo hivi sasa katika eneo hilo, kutekeleza Mpango  Mpana  wa Umoja wa  Mataifa kuhusu siasa, amani na maendeleo katika DRC na  Maziwa  Makuu.
Pamoja na kuzungumza  migogoro inayoendelea katika baadhi ya nchi za Afrika,  Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alielezea wasi wasi wake kuhusu  sintofahamu zinazoendelea katika   baadhi ya nchi za  Asia na  Ulaya  hususani  muendelezo wa  chuki na uhasama kwa kimsingi ya tofauti za dini, na  ukabila.
Akagusia pia  migogoro inayoendelea katika Mashariki ya Kati hususani  katika nchi za Syria,  Misri na mgogoro kati ya  Israel na Palestina
Katika  hatua nyingine,  Katibu Mkuu  Ban Ki Moon, amesema  Umoja wa Mataifa,  haupashwi  kuziomba  au kuzibembeleza  nchi wanachama  pale unapohitaji kupatiwa  wanajeshi, polisi au vifaa   wakati ambapo raia wasiokuwa na hatia wakiendelea kuteseka na kupoteza maisha.
Akasisitiza kwamba Umoja wa Mataifa ni chombo  muhimu  ambapo maamuzi mengi yamekuwa yakifanyika lakini akasema anatiwa shaka  na baadhi ya  misimamo ya  viongozi au nchi zenye ushawishi   mkubwa.
Pamoja na kuelezea matatizo ya kisiasa na kiusalama na changamoto zake, pia aliainisha  baadhi ya mafanikio ya chombo hicho katika mwaka uliopita na kazi kubwa iliyombele yake na hasa   likiwamo  jukumu ya utayarishaji wa  malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.

No comments: