
Mshambuliaji wa Simba, Ramadhani Singano akishangilia bao lake kwa kupiga sarakasi, baada ya kufunga katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Chuoni katika Kombe la Mapinduzi Zanzibar, kwenye Uwanja wa Amaan. Picha na Michael Matemanga.
Zanzibar. Wawakilishi wa Tanzania, Azam na Simba leo watakuwa na kibarua kizito mbele ya timu za Uganda, URA na KCC wakati wa mechi za nusu fainali za Kombe la Mapinduzi zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mabingwa watetezi Azam wenyewe watashuka uwanjani hapo saa 10 jioni kuikabili KCC, wakati Simba watawakabili URA saa 2 usiku na kuifanya fainali ya mwaka huu kuwa na uwezekano wa kuzikutanisha timu zote za Tanzania au Uganda.
Azam iliyofanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kuibanjua vibonde Cloves mabao 2-0 itajiuliza kwa KCC ya Uganda, inayoonekana tishio kwenye michuano hii kutokana na kutopoteza mchezo hata mmoja tangu michuano hii ianze Januari Mosi hali kadhalika kwa Azam.
Hata hivyo, Azam itawakosa wachezaji wake John Bocco ‘Adebayo’ na beki Erasto Nyoni ambao ni wagonjwa na Joseph Kimwaga majeruhi.
Kocha msaidizi wa Azam Kalimangonga Ongola alisema, “Azam ndio mabingwa watetezi, mchezo utakuwa mgumu kwa vile ni mtoano, ila sisi tumejiandaa vizuri naamini tutafanya vizuri, na kuchukua ubingwa.
Kocha wa KCC, George Nsimba alisema “Tunaenda kucheza Ligi ya Mabingwa, kikosi changu hakikufanya mazoezi, mechi ya kwanza tuliyocheza hapa ndio yalikuwa mazoezi yetu ya kwanza, michuano hii imesaidia sana.
“Azam ni timu ngumu tunaifahamu, tunaangalia kuhakikisha tunacheza nusu fainali ili tupate mazoezi mazuri zaidi ya kujiandaa na mashindano yetu.”
Usiku uwanjani hapo mashabiki watawashuhudia Ramadhani Singano ‘Messi’ na Amis Tambwe wakiiongoza Simba kuwakabili URA ya Uganda katika nusu fainali ya pili.
Simba inajivunia ukuta imara, safu nzuri ya kiungo, lakini haina makali sana katika safu yake ya ushambuliaji, tatizo ambalo kocha Mcroatia Zradvok Logarusic ana kazi ya kufanya leo ili kuivunja mapema ngome ya URA.
Simba ilifuzu kwa hatua hiyo baada ya kuichapa Chuoni mabao 2-0 katika robo fainali iliyochezwa usiku wa kuamkia jana.
Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola akizungumzia mchezo wao na URA alisema, “Mechi itakuwa ngumu, timu zote zinazocheza mashindano haya tunaziheshimu hakuna timu ya kubeza si unaona hata hawa watoto (Chuoni) tungewadharau wangetuaibisha, lakini sisi lengo letu ni moja tu, kuchukua ubingwa.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment