ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 9, 2014

UNAKUBALI MKEO AVAE NGUO ZA KUBANA, KITOVU NJE! USHAMBA ULIOJE?

WAKATI f’lani niliwahi kuandika makala iliyokuwa inahusu sababu ambazo zinawafanya baadhi ya wanawake kupata usumbufu mkubwa kutoka kwa wanaume wakware. Makala hayo yaligusia mbali na mambo mengine, suala la uvaaji usio wa kiheshima.

Nikasema kwamba, endapo mchumba, mke au mpenzi wa mtu ataamua kuvaa nguo ambazo hazina tofauti na zile wanazovaa wale machangudoa, basi asijisikie vibaya kusumbuliwa kwa kuitwa majina ya ajabu na hata wakati mwingine kushikwa sehemu zao nyeti.

Nilitoa kauli hiyo nikimaanisha kwamba, kufanya hivyo ni kujitafutia matatizo mwenyewe. Ni kweli kila mmoja ana uhuru wa kuvaa vile anavyojisikia lakini wakati mwingine tuangalie tunavaa nini tunapokwenda wapi.

Hivi utakuwa unajitakia mema kweli eti kwa kuwa una uhuru wa kuvaa utakavyo, uende Kariakoo ukiwa ukiwa umevaa kinachoacha wazi mapaja yako nje au taiti ya kulalia? Sidhani kama ni sahihi na kama unaona ni sawa, endelea na uvaaji wako huo na ipo siku utakubaliana na mimi kuwa siyo sawa kuvaa hivyo na ukakatiza mbele za wanaume hasa katika ulimwengu wa sasa.

Lakini sasa, kinachoshangaza wapo baadhi ya wake za watu ambao eti wanajifanya wanakwenda na wakati kwa kuvaa vinguo vya kubana na kukatiza mbele za wanaume huku wakitingisha maungo yao.

Mbali na kuvaa nguo hizo ambazo ni sawa na kuwatega wanaume, wapo wanaokwenda mbali zaidi kwa kuvaa khanga moja, ndani hakuna kitu kisha kwenda gengeni, dukani au sehemu nyinginezo ambako wanapishana na wanaume.

Swali ni je, wanaofanya hivyo wanakuwa na sababu gani? Ni ili kuwatega waume? Kama ni hivyo, wakishawatega? Yaani kweli mke wa mtu na heshima zako bado una mawazo ya kuwatega wanaume wengine? Hivi unaipenda ndoa yako kweli?

Mimi nadhani ifike wakati watu wabadilike. Akivaa nguo za kubana msichana ambaye hana mpenzi wala hajaolewa, watu wanaweza wasishangae sana kwa sababu huenda anatangaza biashara au anatafuta mtu, wewe mke wa mtu unatafuta nini? Au ndiyo unatangaza uzuri wako?

Hebu tujaribu kustaarabika halafu wanaume nao waache ulimbukeni usiokuwa na maana. Kuna baadhi yao huko mtaani wala hawaoni aibu kutembea na wake zao wakiwa wamevaa kihasara. Eti wanaona sifa!

Ni ushamba ulioje kukubali mkeo avae kitopu au khanga moja kisha awatingishie wanaume wenzako? Unampenda kweli huyo mkeo au unapitisha tu muda naye?
Mkeo anatakiwa kujiheshimu na kujiweka mbali na vishawishi vya wanaume. Kuvaa nguo za ajabu wakati yuko ndani ya ndoa ni kujidhalilisha yeye na mumewe pia.

Unavaa taiti kisha unatingisha makalio yako tena wakati mwingine kwa makusudi, huku si kujitafutia kubakwa? Hata kama unatembea ndani ya gari lakini kumbuka utashuka na kuingia dukani, utawapa matatizo bure watu wenye mfadhaiko.

Jamani, hili suala la uvaaji wa stara hasa kwa wake za watu au wale wenye wapenzi wao lizingatiwe. Tuachane na ile dhana ya kwenda na wakati, huku kwenda na wakati huku kutatufanya tudhalilike, tuaibike na tupewe sifa ambazo hazistahili.

GPL

No comments: